Fifa kuijaza mamilioni ya dola Man City
Muktasari:
- Chini ya Mpango wa Manufaa kwa Klabu wa FIFA, klabu zitapokea Dola 11,000 kwa siku kwa kila mchezaji ambaye ameachiliwa kwenda kuichezea timu yake ya taifa katika fainali hizi, kwa kipindi chote ambacho mchezaji huyo atakuwa anashiriki kwenye mashindano hayo.
LONDON, England. Manchester City ni moja ya timu itakayovuna fedha nyingi zaidi kutoka FIFA baada ya kutoa wachezaji wengi zaidi 19, wakaoshiriki katika Kombe la Dunia la 2026 kuanzia Juni 11 hadi Julai 19.
Chini ya Mpango wa Manufaa kwa Klabu wa FIFA, klabu zitapokea Dola 11,000 kwa siku kwa kila mchezaji ambaye ameachiliwa kwenda kuichezea timu yake ya taifa katika fainali hizi, kwa kipindi chote ambacho mchezaji huyo atakuwa anashiriki kwenye mashindano hayo.
Kwa mfano, ikiwa klabu ina wachezaji watano kwenye Kombe la Dunia na timu zao zikafika hadi hatua za mwisho za mashindano, klabu hiyo inaweza kupata mamia ya maelfu ya dola kama fidia kwa kuwaruhusu wachezaji wake kushiriki.
Mpango huu ulianzishwa na FIFA ili kuzisaidia klabu zinazowatoa wachezaji wao kwa timu za taifa, kwa kutambua mchango wao katika maendeleo na maandalizi ya wachezaji hao.
Malipo hayo huhesabiwa kuanzia kipindi cha maandalizi kabla ya mashindano hadi siku ya mwisho ambayo timu ya taifa ya mchezaji husika inabaki kwenye mashindano
Man City inataraji kunufaika zaidi kwa wachezaji hao 19, ambao wameteuliwa katika vikosi mbalimbali vya Kombe la Dunia, wanne wameitwa England.
Kipa James Trafford yumo katika orodha ya wachezaji 26 ya kocha Thomas Tuchel, pamoja na mabeki Marc Guehi, Nico O'Reilly na John Stones.
Kama ilivyo kwa Stones, nahodha wa City, Bernardo Silva ataondoka klabuni humo msimu huu. Silva ni mmoja wa wachezaji watatu wa sasa wa City waliopo katika kikosi cha Ureno cha Kombe la Dunia, wengine wakiwa beki Ruben Dias na kiungo Matheus Nunes.
Uholanzi na Croatia kila moja ina wachezaji wawili wa City katika vikosi vyao. Tijjani Reijnders na Nathan Ake wamo katika kikosi cha Uholanzi, huku Mateo Kovacic na Josko Gvardiol wakiiwakilisha Croatia.
Wengine wanaokamilisha orodha hiyo ni Erling Haaland (Norway), Omar Marmoush (Misri), Rayan Cherki (Ufaransa), Jeremy Doku (Ubelgiji), Rodri (Hispania), Rayan Ait-Nouri (Algeria), Antoine Semenyo (Ghana) na Abdukodir Khusanov (Uzbekistan).
Si tu hii ndiyo idadi kubwa zaidi ya wachezaji kutoka klabu yoyote katika soka la England, bali pia inaifanya Manchester City kuwa klabu yenye uwakilishi mkubwa zaidi katika Kombe la Dunia miongoni mwa klabu zote duniani.
Katika Kombe la Dunia la 2022 nchini Qatar, Manchester City ilikuwa klabu iliyopata fedha nyingi zaidi kupitia Mpango wa Manufaa kwa Klabu wa FIFA.
City iliwaruhusu wachezaji 16 kwenda kuwakilisha timu zao za taifa katika mashindano hayo, jambo lililoifanya klabu hiyo kupokea takribani Dola4.6 milioni.
Manchester United na Chelsea zilifuatia nyuma ya Manchester City katika orodha ya klabu za Ligi Kuu England zilizopata fedha nyingi zaidi kupitia Mpango huo 2022.
Manchester United ilipokea takribani Dola3.33 milioni, huku Chelsea ikipokea Dola 3.25 milioni.
Mwaka huu jumla ya timu 17 zitakuwa na wachezaji 10 au zaidi waliocheza mechi zao za mwisho za klabu kwao kabla ya kwenda kwenye mashindano hayo, huku tano kati ya timu hizo zikiwa kutoka England.
Arsenal ipo nafasi ya tatu kwa pamoja na mabingwa wa Ufaransa, Paris Saint-Germain, ambao waliifunga Arsenal katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Klabu zote mbili zina wachezaji 17 watakaoshiriki mashindano hayo nchini Marekani, Canada na Mexico.
Mabingwa wa Ujerumani, Bayern Munich wako nafasi ya pili wakiwa na wachezaji 18, huku mabingwa wa La Liga FC, Barcelona wakikamilisha tano bora kwa kuwa na wachezaji 15.
Barcelona ndiyo ilikuwa klabu iliyokuwa na uwakilishi mkubwa zaidi katika Kombe la Dunia lililopita nchini Qatar ikiwa na wachezaji 17, wakati Manchester City na Bayern Munich zilifuatia kwa pamoja zikiwa na wachezaji 16 kila moja.
Miaka minne kabla ya hapo nchini Urusi, Manchester City iliongoza kwa kuwa na wachezaji 16, ikifuatiwa na Real Madrid yenye 15 na Barcelona yenye 14.
Wachezaji 17 wa Barcelona katika Kombe la Dunia lililopita waliweka rekodi mpya ya uwakilishi wa klabu moja katika mashindano hayo. Hata hivyo, Manchester City imeweka rekodi mpya mwaka huu, ikisaidiwa pia na kuongezeka kwa idadi ya timu kutoka 32 hadi 48.