Gianluigi Donnarumma anyemelewa na vigogo

Muktasari:
- Kipa huyo ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu ujao yupo kwenye mazungumzo na mabosi wa PSG ya kuongeza mkataba, lakini hawajafikia mwafaka wa makubaliano binafsi.
BAYERN Munich, Real Madrid na AC Milan zipo katika vita ya kuwania saini ya kipa wa PSG na timu ya taifa ya Italia, Gianluigi Donnarumma, 26, katika dirisha hili la usajili.
Kipa huyo ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu ujao yupo kwenye mazungumzo na mabosi wa PSG ya kuongeza mkataba, lakini hawajafikia mwafaka wa makubaliano binafsi.
Timu tajwa hapo juu zimeanza kujipenyeza chinichini zikiamini ikiwa PSG itashindwa kumsainisha mkataba mpya itamuuza ili kuepuka kumuuza kwa pesa kiduchu ifikapo dirisha la majira ya baridi mwakani au akaondoka bure mwisho wa msimu ujao.
Donnarumma amezivutia timu nyingi kutokana na kiwango bora alichoonyesha akiwa na PSG hususan katika Ligi ya Mabingwa Ulaya ambako aliiwezesha kushinda taji kwa mchango wake mkubwa wa kusimama vyema langoni.
Anthony Elanga
NEWCASTLE United imeanza mazungumzo kwa ajili ya kumsajili winga wa Nottingham Forest na timu ya taifa ya Sweden, Anthony Elanga mwenye umri wa miaka 23, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Elanga ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika, msimu uliopita alicheza mechi 43 za michuano yote na kufunga mabao sita.
Benjamin Sesko
ARSENAL imewasiliana rasmi na RB Leipzig kuulizia uwezekano wa kumsajili mshambuliaji wa timu hiyo na timu ya taifa ya Slovenia, Benjamin Sesko mwenye umri wa miaka 22, licha ya kwamba hakuna taarifa rasmi iliyotolewa na Leipzig yenyewe. Katika msimu uliopita, Sesko alicheza mechi 45 za michuani yote na kufunga mabao 21.
Bryan Mbeumo
MANCHESTER United imewasilisha ofa ya Pauni 60 milioni Brentford kwa ajili ya kumsajili winga wa timu hiyo na Cameroon, Bryan Mbeumo, 25, baada ya ofa ya awali ya Pauni 55 milioni kukataliwa. Mbeumo mwenyewe amekubali kujiunga na Mashetani Wekundu, lakini Brentford na Man United hadi sasa bado hazijafikia mwafaka juu ya ada ya uhamisho.
Rasmus Hojlund
IINTER Milan imefanya mazungumzo ya awali na Manchester United kujadili mpango wa kumsajili mshambuliaji wa timu hiyo na Denmark, Rasmus Hojlund, 22, anayekadiriwa kugharimu Pauni 40 milioni. Rasmus ni miongoni mwa mastraika waliopata nafasi kubwa kucheza msimu uliopita licha ya kutoonyesha kiwango kilichohitajika Old Trafford.
Rayan Cherki
MABOSI wa Olympique Lyon wamekataa ofa ya kwanza kutoka kwa Manchester City iliyowasilishwa kwa ajili ya kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa Ufaransa, Rayan Cherki mwenye umri wa miaka 21 anayewindwa sana na Man City. Licha ya kukataliwa kwa ofa hiyo ya kwanza Man City haijakata tamaa na hadi sasa mazungumzo bado yanaendelea kati ya timu hizo mbili.
Trevoh Chalobah
MABINGWA wa Ligi Kuu Italia (Serie A), Napoli wanapanga mikakati ya kumsajili beki wa England mwenye umri wa miaka 25, Trevoh Chalobah ambaye aliisaidia Chelsea kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya na kushinda UEFA Conference League baada ya kurejea kutoka alikokuwa akicheza kwa mkopo, Crystal Palace Januari mwaka huu.
Chalobah ambaye pia ameonyesha nia ya kutaka kuondoka, amewaambia Napoli kuwa yupo tayari kujiunga nao lakini kwa mkataba wa kudumu.
Kepa Arrizabalaga
ARSENAL ni miongoni mwa timu zinazoinyemelea saini ya kipa wa Chelsea na Hispania, Kepa Arrizabalaga, 30, ambaye ana kipengele cha kuondoka kwa Pauni 5 milioni katika mkataba wake. Kepa ambaye msimu uliopita alicheza kwa mkopo Bournemouth hayupo katika mipango ya kocha Enzo Maresca, hivyo anataka kujiunga na timu itakayomhakikishia nafasi.