Prime
Hauzwi… Amorim kasema ana jambo lake na Bruno

Muktasari:
- Tayari mabosi wa Real Madrid wameshaonyesha nia ya kuhitaji saini yake kutokana na kiwango bora alichoonyesha Mreno huyo tangu atue kwa Mashetani hao wekundu na kuwa tegemeo kikosini.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa Manchester United, Ruben Amorim kwa Bruno Fernandes kwa sasa humwambii kitu na haraka amewaambia vigogo wa timu hiyo, bado anamhitaji sana nahodha huyo katika mipango yake msimu ujao.
Tayari mabosi wa Real Madrid wameshaonyesha nia ya kuhitaji saini yake kutokana na kiwango bora alichoonyesha Mreno huyo tangu atue kwa Mashetani hao wekundu na kuwa tegemeo kikosini.
Bruno alisajiliwa akitokea Sporting Lisbon mwaka 2020 na hadi sasa ameifungia Man United mabao 177, katika mechi 277 za michuano yote alizoichezea timu hiyo.
Kwa mujibu wa tovuti ya Daily Star, Madrid imetuma wawakilishi wake kwenda jijini Manchester kumtazama kapteni Bruno ambaye amefunga mabao 12 na kutoa asisti tisa katika mechi 27 alizocheza chini ya Amorim.
Madrid inamwangalia Bruno kama mbadala wa Luka Modric ambaye umri umeshamtupa mkono na huenda akastaafu hivi karibuni.
Akimzunguzia staa huyu mara kadhaa, Amorim amewahi kusema: "Anakuwepo katika kila tukio muhimu, kuanzia mipira ya kutenga yupo vizuri, pia anaweza kubadilisha nafasi, anaweza kuupeleka mpira mbele, anaweza kufunga mabao, anaweza kufanya mabadiliko, pia ana uwezo mzuri wa kukaba ni nahodha kamili kwa timu yetu na tunahitaji kumsaidia kushinda mataji kwa sababu anastahili mengi."
Mmiliki mwenza wa mashetani hao wekundu, Sir Jim Ratcliffe hivi karibuni alikiri klabu ina wachezaji kadhaa ambao "hawatoshi" na "wanalipwa zaidi," lakini alisisitiza bado wanamhitaji Bruno.
"Wengine hawatoshi na wengine labda wanalipwa zaidi. Lakini ili tuunde timu tunayohitaji kuiona na kujivunia, itachukua muda. Tuna kipindi hiki cha mabadiliko na tunahamia kutoka tulipo kwenda katika zama mpya."
"Kuna wachezaji wazuri katika kikosi kama tunavyojua, nahodha wetu ni mchezaji mzuri. Tunamhitaji Bruno, ni mchezaji mzuri sana," alisema Ratcliffe.
Fernandes alisaini mkataba mpya mwezi Agosti mwaka jana, akifichua alikuwa na fursa ya kuondoka Old Trafford lakini alikubali kuongeza mkataba kwa sababu klabu ilionyesha inamhitaji.
"Klabu ilikuwa inajua kulikuwa na uwezekano wa mimi kuondoka, nilikuwa na ofa halisi," alifichua.
"Lakini klabu ilionyesha inanihitaji mimi, ilikuwa katika kipindi cha mabadiliko na walitaka kufanya mambo kwa njia tofauti kidogo.
"Ninaamini kuna mustakabali mzuri katika klabu hii kwa sababu ya mabadiliko yanayofanyika. Ndiyo maana niliamua kubaki. Kulikuwa na nafasi nyingine ya kuhamia sehemu ambayo ingekuwa na manufaa kwangu. Lakini najisikia vizuri hapa, najisikia kupendwa na najisikia kuwa timu imeniheshimu sana."