Kisa Vinicius, Madrid yaanza kumwinda Nico Williams

Muktasari:
- Williams ambaye dirisha lililopita la majira ya kiangazi alihusishwa sana na Barcelona kwenye mkataba wake kuna kipengele kinachomruhusu kuondoka ikiwa timu inayohitaji huduma yake italipa Pauni 51.8 milioni.
MABOSI wa Real Madrid wanaangalia uwezekano wa kumsajili winga wa Athletic Bilbao na timu ya taifa ya Hispania, Nico Williams dirisha lijalo la majira ya kiangazi kama mbadala wa Vinicius Jr ikiwa Mbrazil huyo ataamua kuondoka mwisho wa msimu huu.
Williams ambaye dirisha lililopita la majira ya kiangazi alihusishwa sana na Barcelona kwenye mkataba wake kuna kipengele kinachomruhusu kuondoka ikiwa timu inayohitaji huduma yake italipa Pauni 51.8 milioni.
Madrid ina wasiwasi kwamba Vinicius huenda akachukua uamuzi wa kutaka kuondoka kutokana na ofa nono ambayo waarabu wa Saudi Arabia wameiweka tangu dirisha lililopita la majira ya kiangazi.
Kwa mujibu wa ripoti, matajiri hao wapo tayari kumpa Vinicius mshahara unaofikia Euro 200 milioni kwa mwaka kiasi ambacho inaonekana kuwa ngumu kwa staa huyo kukikataa.
Hata hivyo, ili kumpata Nico kama mbadala wake Madrid itatakiwa kushinda vita dhidi ya wapinzani wao Barcelona ambao dirisha lililopita walikuwa wakitumia ushawishi wa Lamine Yamal ambaye ni rafiki mkubwa wa mshambuliaji huyo.
Trent Alexander-Arnold
BEKI wa Liverpool na timu ya taifa ya England, Trent Alexander-Arnold, 26, amefikia makubaliano na Real Madrid ya kujiunga nao dirisha lijalo la majira ya kiangazi na mkataba wake na Majogoo utakuwa unamalizika. Ripoti zinaeleza, Trent amekubali kusaini mkataba wa miaka mitano wa kuwatumikia wababe hao wa Hispania.
Casemiro
MANCHESTER United inataka kuruhusu zaidi ya wachezaji 10 ikiwemo mshambuliaji wao wa kimataifa wa England anayecheza kwa mkopo Aston Villa na kiungo Mbrazil, Casemiro kuondoka katika dirisha lijalo. Mpango wa kuruhusu mastaa hao inataka kufanywa ili kujenga upya kikosi hicho kwani mabosi wa timu hiyo wanaamini mastaa wengi waliopo sasa hawana viwango vya kuipa timu mafanikio.
Yusuf Akcicek
BEKI wa kati wa Fenerbahce na timu ya taifa ya Uturuki, Yusuf Akcicek, 19, yupo katika rada za timu mbalimbali barani Ulaya ikiwamo Tottenham Hotspur, Bayern Munich, Atletico Madrid, Napoli na RB Leipzig zinazohitaji kumsajili dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Maskauti wa timu hizi wanadaiwa kuonekana mara kwa mara katika mechi za Fenerbanhce kwa ajili ya kutazama maendeleo ya beki huyo.
Sandro Tonali
BARCELONA inataka kumsajili kiungo wa Newcastle na timu ya taifa ya Italia, Sandro Tonali, 24, dirisha lijalo la majira ya kiangazi na staa huyu anadaiwa kutaka kuondoka ili kutafuta changamoto mpya sehemu nyingine. Awali timu za Italia ikiwemo Juventus ndio zilikuwa zikipewa nafasi kubwa ya kuipata saini yake.
Jarrad Branthwaite
EVERTON bado inafanya mazungumzo na beki wao raia wa England, Jarrad Branthwaite, 22, ili kumshawishi asaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia timu hiyo kwa muda mrefu baada ya vigogo kibao ikiwemo Manchester United na Liverpool kuonyesha nia ya kutaka kumsajili. Jarrad ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027, amekuwa akipewa nafasi kubwa ya kutua Man United.
Frenkie de Jong
KIUNGO wa Barcelona na timu ya taifa ya Uholanzi, Frenkie de Jong amewaambia wawakilishi wake kipaumbele chake cha kwanza ni kuendelea kusalia Barca na kusaini mkataba mpya ila ikishindikana ndio ataangalia timu nyingine zinazomhitaji. De Jong mwenye umri wa miaka 27, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwakani lakini hivi karibuni amekuwa akikumbana na upinzaji mkubwa kutoka kwa mashabiki wa Barcelona ambao hawaridhishwi na kiwango chake.
Jorrel Hato
REAL Madrid imeungana na Arsenal, Liverpool na Chelsea katika vita ya kuiwania saini ya beki kisiki wa Ajax na Uholanzi, Jorrel Hato dirisha lijalo. Hato mwenye umri wa miaka 19, anaonekana kuzivutia timu nyingi kubwa kutokana na ubora wake aliouonyesha kuanzia timu ya taifa na ndani ya Ajax. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2028. Msimu huu amecheza mechi 42 za michuano yote na kufunga mabao matatu.