Leao aendelea kuitesa Man United, ikipanga kuvunja benki
Muktasari:
- Kwa sasa Leao anaweza kupatikana kwa ada ndogo zaidi baada ya AC Milan kushindwa kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini kinachoweza kuleta ugumu ni suala la maslahi kwa sababu anahitaji mshahara wa zaidi ya Pauni 200,000 kwa wiki.
MANCHESTER United imeweka jina la winga wa AC Milan na Ureno, Rafael Leao (26), kwenye orodha ya wachezaji inaowahitaji kwa udu na uvumba, ikiwa ni siku chache baada ya kuelezwa kwamba klabu nyingi zimetua mezani kwake zikiitaka huduma yake kwa ajili ya msimu ujao.
Kwa sasa Leao anaweza kupatikana kwa ada ndogo zaidi baada ya AC Milan kushindwa kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini kinachoweza kuleta ugumu ni suala la maslahi kwa sababu anahitaji mshahara wa zaidi ya Pauni 200,000 kwa wiki
Inaelezwa kwamba Inter Milan, Manchester City, Real Madrid na Atletico Madrid zinapambana kupitia wawakilishi wake ili kuweka mambo sawa kwa sababu mwenyewe hayupo Italia kwa sasa, na kwamba tayari yupo kikosini Marekani na timu ya taifa ya Ureno.
Vita ya vigogo aliyoianzisha nyota huyo aliyefunga mabao tisa na asisti tatu Ligi Kuu Italia inatokana na taarifa zilizovuja mwanzoni mwa mwaka huu alipodai kuwa anafikiria kupata changamoto mpya katika kikosi kinachotaka ubingwa wa Ulaya. Leao anatarajiwa kumaliza mkataba wake Milan ifikapo Juni 30, 2028.
Bernado Silva
KIUNGO wa kimataifa wa Ureno, Bernardo Silva (31), anayeondoka Manchester City mwishoni mwa mwezi huu kwa uhamisho wa bure ameendelea kuzivutia timu mbalimbali, ingawa tayari ameshapewa ofa na Atletico Madrid na Benfica. Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, nyota huyo anapendelea kuhamia Barcelona ambako pia kocha Hans Flirk amekuwa akimhusudu muda mrefu na ni miongoni mwa wachezaji waliopo katika orodha ya mahitaji yake msimu ujao.
Dino Toppmoller
KOCHA wa Mjerumani Dino Toppmoller ambaye aliondoka Eintracht Frankfurt Januari mwaka huu, ni miongoni mwa makocha wanaowania nafasi ya kuifundisha Crystal Palace iwapo Oliver Glasner ataondoka. Zipo taarifa zinazoeleza kuwa uongozi wa Palace unasubiri tu Glaner aondoke ili wamtangaze kwa sababu kila kimeshakubaliwa kwenye meza ya mazungumzo baina ya pande hizo mbili. Vilevile Toppmoller ana ofaa kadhaa kutoka timu za madaraja ya chini Ufaransa na England.
Lamare Bogarde
ASTON Villa inadaiwa kwamba inaendelea na mazungumzo ya kumuongezea mkataba kiungo wa kimataifa wa Uholanzi, Lamare Bogarde (22), ili aendelee kubaki klabuni hapo. Taarifa za Bogarde kuongezwa mkataba zimekuja wakati ambapo rada za timu mbalimbali England zimeshatua Villa zikitaka kumng'oa nyota huyo wa kimataifa wa Uholanzi ambaye amekuwa katika kiwango bora miezi ya karibuni. Msimu huu amecheza dakika 1,048 Ligi Kuu England.
Jean-Matteo Bahoya
MSHAMBULIAJI wa Eintracht Frankfurt na timu ya vijana chini ya miaka 21 ya Ufaransa, Jean-Matteo Bahoya (21), anawindwa na klabu kadhaa za Ulaya na Saudi Arabia, huku taarifa za ndani zikidai kwamba mwenyewe anapendelea kufunguliwa mlango ili akasake malisho mapya. Taarifa zinadai Frankfurt imeshaeleza kwamba haitapenda kumuona akiondoka dirisha lijalo kwa sasa ina malengo naye. Msimu huu ameishezea mechi 27 za Bundesliga akifunga maba matatu na asisti nne.
Josko Gvardiol
BARCELONA na Bayern Munich zinadaiwa kuonyesha nia ya kumsajili beki wa Manchester City na Croatia, Josko Gvardiol (24), ambaye mustakabali wake Etihad uko shakani hasa baada ya kauli yake hivi karibuni kwamba atazungumzia suala la kubaki au kuondoka baada ya fainali za Kombe la Dunia 2026 zinazofanyika Marekani, Mexico na Canada. Barca na Bayern Munich zilikuwa miongoni mwa timu zilizomtaka nyota huyo 2023 alipokuwa RB Leipzig. Mkataba wake Man City unamalizika Juni mwakani.
Tijjani Reijnders
ATLETICO Madrid inajiandaa kuwasilisha ofa kwa ajili ya kumsajili kiungo wa Manchester City na timu ya taifa ya Uholanzi, Tijjani Reijnders (27), ambaye alijiunga na klabu hiyo majira ya joto mwaka jana. Nyota huyo aliyekuwa kipenzi cha mashabiki wa AC Milan kabla ya kutua Man City kwa sasa hana uhakika wa kuanza katika kikosi cha kwanza. Mkataba wa Tijjani na Man City unatarajiwa kumalizika Juni 30, 2030.
Marco Palestra
NEWCASTLE United imemuweka beki wa kulia wa kimataifa wa Italia na Atalanta, Marco Palestra, kama chaguo la kwanza la usajili wa majira ya kiangazi yajayo kutokana na hofu ya kukimbiwa na nyota wake wa eneo hilo. Hata hivyo, Newcastle United inaweza kukumbana na ushindani mkali kutoka kwa Manchester City, Arsenal na Inter Milan zinazofuatilia kwa karibu mustakabali wake katika kikosi chake cha sasa.
Palestra amekuwa bora katika eneo hilo akitoka kusugua benchi hadi kujihakikishia namba katika kikosi cha kwanza cha Atalanta. Mkataba wake unamalizika mwisho wa mwezi huu.