Liverpool kwa Alexander-Arnold njia ni hii

Muktasari:
- Alexander-Arnold, ambaye ni mzaliwa wa Liverpool, anatarajiwa kujiunga na Real Madrid mkataba wake utakapomalizika mwishoni mwa msimu huu, huku ripoti zikisema tayari timu hiyo imemwekea mezani ofa ya mshahara wa Pauni 12 milioni kwa mwaka.
LIVERPOOL, ENGLAND: MCHEZAJI wa zamani wa Liverpool, Stephen Warnock anaamini bado kuna nafasi Trent Alexander-Arnold akaendelea kubaki Anfield msimu ujao.
Alexander-Arnold, ambaye ni mzaliwa wa Liverpool, anatarajiwa kujiunga na Real Madrid mkataba wake utakapomalizika mwishoni mwa msimu huu, huku ripoti zikisema tayari timu hiyo imemwekea mezani ofa ya mshahara wa Pauni 12 milioni kwa mwaka.
Hata hivyo, hadi sasa bado dili hilo halijakamilika na Warnock anaamini kuna uwezekano mkubwa wa Majogoo hao kumbakisha ikiwa tu watamfanya kuwa mchezaji anayelipwa zaidi katika kikosi chao.
Akimlinganisha na wachezaji wenzake Virgil van Dijk na Mohamed Salah, ambao mikataba yao inamalizika mwisho wa msimu, Warnock alisema kwenye BBC Football Focus:
"Bado nadhani kuna nafasi ya kumbakisha. Nadhani bado kuna kipengele ambacho kinamfanya abaki kwa kumlipa pesa nzuri."
"Kwa sababu ukiangalia Virgil van Dijk na Mohamed Salah, mishahara yao ni ya juu sana kwa sasa. Kwa kuwa Trent ni kijana wa hapa, hawezi kuwa na pesa kama wanazopata wao, mimi naona ni suala la kufanya hivyo tu ili kumpata," alisena Warnock.
"Jambo hilo ni baya kwa sababu mashabiki wa Liverpool wanaumizwa sana na ukweli anaweza kuondoka kwa uhamisho wa bure."
Inaelezwa, mshahara wa sasa wa Alexander-Arnold na Liverpool ni Pauni 9 milioni kwa msimu, wakati Van Dijk akipata Pauni 11 milioni na Salah akipata Pauni 18 milioni.
Bado haijulikani ikiwa Van Dijk au Salah watakubali kusaini mkataba mpya licha ya kuwa karibu kutwaa taji lao la pili la Ligi Kuu msimu huu wakiongozwa na Kocha Arne Slot ambaye ni msimu wake wa kwanza kama kocha.