Maresca yupo salama Chelsea

Muktasari:
- Maresca aliwasili Stamford Bridge akitokea Leicester City wakati wa majira ya kiangazi mwaka jana na alionekana kuibadili Chelsea baada ya kuonekana kuchuana na Liverpool kwenye mbio za ubingwa.
LONDON, ENGLAND: KOCHA, Enzo Maresca kwa sasa kibarua chake kipo salama huko Chelsea licha ya Mtaliano huyo kuwa kwenye kitimoto kutokana na kushinda mechi tatu tu kati ya 10 za mwisho Ligi Kuu England.
Maresca aliwasili Stamford Bridge akitokea Leicester City wakati wa majira ya kiangazi mwaka jana na alionekana kuibadili Chelsea baada ya kuonekana kuchuana na Liverpool kwenye mbio za ubingwa.
Hilo lilikuja baada ya kushinda kwenye mechi tano mfululizo Desemba, lakini kwa sasa mambo yametibuka kabisa na kuwa kwenye vita kali ya kuwania kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Brighton, Ijumaa iliyopita.
Chelsea kwa sasa ipo nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, pointi moja nyuma ya Manchester City iliyopo Top Four, lakini timu za Bournemouth na Nottingham Forest kwa mwenendo wa soka lao la sasa, zina nafasi kubwa ya kumaliza juu ya The Blues itakapofika mwisho wa msimu.
Hata hivyo, Maresca bado ana nafasi ya kukamatia tiketi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kutokana na Ligi Kuu England kuwa na uwezekano wa kuingiza timu tano msimu ujao.
Kwa mujibu wa Athletic, bodi ya Chelsea inayoondokwa na milionea wa Marekani, Todd Boehly - inafurahishwa na mwenendo wa timu chini ya Maresca. Na wanachodhani, Chelsea itakuwa imevuka malengo yao ya msimu kama itafanikiwa kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kwenye msimu wa kwanza wa kocha huyo.
Maresca amekuwa akifanya vizuri licha ya kuwa na majeruhi wa kutosha kwenye timu yake, akiwamo straika Nicolas Jackson.
Wachezaji wengine majeruhi ni Marc Guiu, Romeo Lavia, Wesley Fofana, Benoit Badiashile, Noni Madueke na Malo Gusto huku Joao Felix ametolewa kwa mkopo na Mykhailo Mudryk amefungiwa.