Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Paraguay yalipa kisasi cha mwaka 2002, yaitupa nje Ujerumani kwa matuta

Muktasari:

  • Usiku wa kuamkia leo ule msemo wa soka wa Ukuta Mwekundu (Pared Roja) ulithibitika kuwa sio hadithi za vijiweni baada ya Paraguay kuwakata kilimi Wajerumani kwa kuwatoa kwa mikwaju ya penalti 4-3 kufuatia sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 120 za jasho na damu.

KAMA ulijua Wajerumani wangetembea kifua mbele kwa wabishi wa Amerika Kusini, Paraguay, basi mashindano ya Kombe la Dunia 2026 yamekupa jibu.

Usiku wa kuamkia leo ule msemo wa soka wa Ukuta Mwekundu (Pared Roja) ulithibitika kuwa sio hadithi za vijiweni baada ya Paraguay kuwakata kilimi Wajerumani kwa kuwatoa kwa mikwaju ya penalti 4-3 kufuatia sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 120 za jasho na damu.

Ushindi huo wa hatua ya 32 bora sio tu kwamba unaipeleka Paraguay kwenye hatua ya 16 bora kwa mara ya tano katika historia yao, bali ni kisasi kitamu kilicholipwa baada ya miaka 24. Kumbuka mwaka 2002 kule Korea Kusini na Japan, Wajerumani waliwatoa Paraguay hatua kama hii kwa goli la jioni la Oliver Neuville. Safari hii, Paraguay wakasema yaishe!

Takwimu za mchezo zinaonyesha Ujerumani ilikuwa na kila kitu uwanjani isipokuwa bahati na ufungaji.

Vijana wa Julian Nagelsmann walitawala mpira kwa asilimia 60, wakipiga jumla ya pasi  zilizokamilika 755 dhidi ya pasi 162 tu za Paraguay.

Wajerumani walifanya mashambulizi 21 huku sita yakilenga lango na kupata kona 16, lakini kila wakisogeza kwenye lango la Paraguay walikutana na mabeki bora waliozua mashambulizi hayo.

Paraguay ilitangulia kupata bao kupitia Julio Enciso, kabla ya mashine ya Arsenal na Ujerumani, Kai Havertz kusawazisha, dakika 90 zikaisha kwa sare ya 1-1, zikaongezwa 30 kufanya 120 nazo zikaisha kwa sare. Hatimaye timu zikaenda katika mikwaju ya penalti. 

Kwenye hatua ya penalti, presha ilihamia kwa Wajerumani ambao kawaida yao huwa hawakosi kizembe. Safari hii mambo yalikuwa tofauti. Washambuliaji Kai Havertz, Nick Woltemade na beki kisiki Jonathan Tah walishindwa kuziona nyavu kwa kukosa mikwaju yao.

Kwa upande wa Paraguay, licha ya Antonio Sanabria na Fabián Balbuena kukwama, kijana José María Canale alipiga penalti ya mwisho kwa utulivu na kuipeleka Paraguay hatua ya 16 bora ya michuano hiyo.

Hii inakuwa ni mara ya 5 kwa Paraguay kutinga hatua ya 16 Bora tangu ilipofanya hivyo miaka ya 1986 (Mexico), 1998 (Ufaransa), 2002 (Korea Kusini na Japan), na ile robo fainali yao ya kihistoria ya mwaka 2010 kule Afrika Kusini chini ya kipa Justo Villar.

Paraguay inamsubiri mshindi kati ya Ufaransa na Sweden, ambao watapepetana kuitafuta hatua ya robo fainali Kombe la Dunia 2026.

Mlolongo wa Penalti ulivyokuwa:

Ujerumani (3): Kai Havertz ❌ | Joshua Kimmich ✅ | Jamal Musiala ✅ | Nick Woltemade ❌ | Nadiem Amiri ✅ | Jonathan Tah ❌

Paraguay (4): Mauricio ✅ | Gustavo Gómez ✅ | Matías Galarza ✅ | Antonio Sanabria ❌ | Fabián Balbuena ❌ | Jose Canale ✅