Rashford: Simpo tu uamuzi wa kwenda Aston Villa
Muktasari:
- Fowadi huyo wa Manchester United, Rashford, 27, amekubali kutimkia zake Villa Park baada ya kupoteza nafasi ya kucheza chini ya Kocha Ruben Amorim.
BIRMINGHAM, ENGLAND: STAA Marcus Rashford amesema kujiunga Aston Villa kwa mkopo hadi mwisho wa msimu ni uamuzi mwepesi zaidi kuwahi kuufanya kwenye maisha yake.
Fowadi huyo wa Manchester United, Rashford, 27, amekubali kutimkia zake Villa Park baada ya kupoteza nafasi ya kucheza chini ya Kocha Ruben Amorim.
Aston Villa imewekewa kipangele cha kumnunua jumla mchezaji huyo zao la kutoka akademia ya Man United itakapofika mwisho wa msimu.
Imeelezwa Aston Villa itawagharimu Pauni 40 milioni kunasa jumla huduma ya Rashford itakapofika mwisho wa msimu kwenye dirisha kubwa la usajili.
Rashford aliposti ujumbe wake Instagram akisifia pia staili ya uchezaji ya Aston Villa aliposema: “Ningependa kuwashukuru Manchester United na Aston Villa kwa kulifanya dili hili la mkopo kutokea. Nilikuwa na bahati kutakiwa na klabu kadhaa, lakini kwa Aston Villa ulikuwa uamuzi rahisi sana - napenda namna Aston Villa wanavyocheza msimu huu na mipango ya kocha wao. Nataka kucheza mpira na hilo linanipa mzuka. Namtakia kila mmoja heri huko Manchester United hadi mwisho wa msimu.”
Aston Villa ilitangaza usajili wa Rashford kwa kusema: “Aston Villa inafurahi kutangaza usajili wa mkopo wa Marcus Rashford kutoka Manchester United.”
Uhamisho huo haujaleta athari yoyote ya kifedha kwa Rashford na ataendelea kupokea mshahara wake wa Pauni 325,000 kwa wiki, Man United itachangia asilimia 25 ya mshahara huo hadi mwisho wa msimu.
Licha ya kufunga mabao matatu kwenye mechi mbili za kwanza chini ya Amorim kwenye Ligi Kuu England, Rashford hajaichezea timu hiyo ya Old Trafford tangu Desemba 12. Aston Villa ililazimika kwenda kumsajili kwa mkopo Rashford baada ya kumuuza Jhon Duran kwenda Al-Nassr ya Saudi Arabia kwa ada ya Pauni 64 milioni. Timu nyingine zilizokuwa zikihitaji saini ya Rashford ni Barcelona, Borussia Dortmund, Monaco na AC Milan.