Refa wa EPL analipwa Sh800m kwa mwaka

Muktasari:
- Kukua kwa mshahara wao kunaonyesha umuhimu wao kwenye mchezo wa soka, ambapo wamekuwa wakichezesha kwa presha kubwa kutokana na mechi za soka kutazamwa katika sehemu mbalimbali duniani.
LONDON, ENGLAND; MSHAHARA wa waamuzi wa Ligi Kuu England umewekwa hadharani na kuonyesha kwamba ni moja ya watu wanaolipwa vizuri kwenye nchi ya England.
Kukua kwa mshahara wao kunaonyesha umuhimu wao kwenye mchezo wa soka, ambapo wamekuwa wakichezesha kwa presha kubwa kutokana na mechi za soka kutazamwa katika sehemu mbalimbali duniani.
Kwa takwimu zilizobainishwa na bosi wa waamuzi wa Ligi Kuu England, Howard Webb kwenye mkutano wake na klabu 72 za England, alifichua kwamba waamuzi wanalipwa mishahara mikubwa kwelikweli.

Namba zinaonyesha kwamba kwa wastani wa mshahara wa mwamuzi wa Ligi Kuu England analipwa kati ya Pauni 170,000 na Pauni 180,000, huku wale waamuzi wakubwa wanalipwa hadi Pauni 250,000 kwa mwaka.
Pauni 250,000 ni zaidi ya Sh853 milioni za Kitanzania.
Waamuzi wa Ligi Kuu England wana mishahara, kisha wanalipwa bonasi kulingana na viwango vya kuchezesha pamoja na ada ya kuchezesha mechi. Mshahara halisi upo kati ya Pauni 72,000 na Pauni 148,000, ukitofautiana kulingana na viwango vya waamuzi na uzoefu kwenye kazi hiyo.
Waamuzi wazoefu kama Anthony Taylor na Michael Oliver, wao wana uhakika wa kulipwa hadi Pauni 250,000 kwa mwaka kutokana na umaarufu wao waliojiwekea kwenye Ligi Kuu England. Na wale waamuzi ambao si wazoefu, isipokuwa wamewekwa kwenye kundi la ‘Select Group 1’, hao wanalipwa hadi Pauni 125,000.