Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Utamu wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, haijaisha mpaka iishe

Ulaya Pict

Muktasari:

  • Jumanne zitapigwa mechi nne na Jumatano zitapigwa nyingine nne kwenye mchakato huo wa kusaka timu nane zitakazoingia kwenye hatua ya 16 bora ya mikikimikiki hiyo ya Ulaya.

LONDON, ENGLAND: TOFAUTI ya bao moja tu ndilo lililoamua matokeo ya mechi sita kati ya nane za mkono wa kwanza kwenye mchujo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kabla ya kuingia kwenye mechi za marudiano wiki hii.

Jumanne zitapigwa mechi nne na Jumatano zitapigwa nyingine nne kwenye mchakato huo wa kusaka timu nane zitakazoingia kwenye hatua ya 16 bora ya mikikimikiki hiyo ya Ulaya.

Kwenye mechi zilizopita, Feyenoord iliichapa AC Milan 1-0, Benfica iliikung’uta Monaco 1-0, Bayern Munich iliipiga Celtic 2-1, Club Brugge ilijipigia Atalanta 2-1, Real Madrid iliipiga Manchester City 3-2 na Juventus iliibonda PSV 2-1, huku matokeo ambayo hakuwa ya tofauti ya bao moja ni yale ya PSG ilipoichapa Brest 3-0 na Borussia Dortmund kuipiga Sporting CP 3-0.

Sasa zitapigwa mechi za marudiano kwenye mchujo huo ili kupata mshindi wa jumla, ambapo timu nane zitakwenda kuungana na nane nyingine zilizopita moja kwa moja kwenye hatua hiyo ya mtoano. Mambo ni moto.

Usiku wa Jumanne, AC Milan itakuwa na kazi ya kupindua meza baada ya kuchapwa 1-0 ugenini kwenye mchezo wa kwanza, itakapokabiliana na miamba ya Uholanzi, Feyenoord. Mashabiki wa soka la Italia wanasubiri kwa hamu mchezo huo kuona kama watakuwa na timu kwenye mtoano.

Kasheshe linaloikabili Milan, ndilo litakalokuwa linawakabili AS Monaco, ambao watakuwa ugenini kukipiga na Benfica. Shida kwa Monaco ni kwamba ilikubali kipigo cha bao 1-0 nyumbani, hivyo itakwenda ugenini ikiwa na kazi ya kujaribu kupindua matokeo ili itinge kwenye mtoano wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Monaco ikishindwa kupenya jambo hilo litaifanya Ufaransa kuwa na timu moja tu kwenye hatua ya 16 bora, kutokana na PSG na Brest, ambazo ni timu nyingine za Ligue 1 kutoana zenyewe. Katika mchezo wa kwanza ambao PSG ilikuwa ugenini ilishinda 3-0, hivyo itajimwaga Parc des Princes kuwakaribisha Brest. Mechi hiyo ni ya Jumatano.

Kipute kingine cha Jumanne, kitaishuhudia Bayern Munich itakayokuwa Allianz Arena, kuendeleza kile ilichokianza kwenye mechi ya kwanza dhidi ya Celtic, ambapo ilishinda 2-1 ugenini. Katika mchezo huo wa kwanza straika Harry Kane alikuwa Mwingereza wa kwanza kufikisha mabao 60 kwenye michuano ya Ulaya.

Atalanta yenyewe itakuwa na kazi nzito kwa Club Brugge itakapojaribu kupindua meza baada ya kipigo cha mabao 2-1 ugenini.

Usiku wa Jumatano, Dortmund itakuwa nyumbani Signal Iduna Park kukipiga na Sporting CP huku ikiwa haina presha yoyote baada ya kushinda 3-0 kwenye mchezo wa kwanza uliofanyika Ureno.

Kasheshe zito litakuwa Bernabeu, ambapo Man City baada ya kukubali kichapo nyumbani Etihad, itakwenda kujaribu kupindua meza mbele ya Real Madrid. Pep Guardiola atafanya maajabu mbele ya Carlo Ancelotti. Mechi hiyo ni ya kujuana baada ya timu hizo kukutana mara nyingi kwa miaka ya karibuni. Madrid iliposhinda mechi ya kwanza ilikuwa mara yao ya 300 kupata ushindi kwenye michuano ya Ulaya, ikiwa ni idadi kubwa zaidi kuwahi kutokea kwenye historia ya michuano.

Juventus itakwenda ugenini kukipiga PSV ikiwa na kazi moja tu ya kulinda ushindi wao wa 2-1 iliyopata kwenye mechi iliyopita ili kukamilisha ndoto ya kukamatia tiketi ya kucheza mtoano.

Timu nane zitakazoshinda kwenye mchujo zitakwenda kuungana na Arsenal, Aston Villa, Atletico, Barcelona, Inter Milan, Leverkusen, Lille na Liverpool kwenye hatua ya 16 bora.

Droo ya hatua ya 16 bora, robo fainali na nusu fainali itafanyika Ijumaa ya Februari 21, huku mechi za kwanza kwenye mtoano huo wa 16 bora zitafanyika kati ya Machi 4 na Machi 5 na mechi za marudiano zitafanyika wiki ijayofuata.