Waziri wa Saudia amtaka Mo Salah

Muktasari:
- Mo Salah mkataba wake huko Anfield utafika tamati mwishoni mwa msimu huu na bado hakuna makubaliano yoyote ya mkataba mpya wa kuendelea kubaki kwenye kikosi hicho kuafikiwa. Al-Hilal inaonekana kuwa mstari wa mbele kwenye mbio za kumsajili Mo Salah, ambaye amekuwa akifanya vizuri sana msimu huu.
RIYADH, SAUDI ARABIA: WAZIRI wa Michezo wa Saudi Arabia ameweka hadharani mpango wa kumsajili Mohamed Salah baada ya taifa hilo kupambana kuhakikisha wananasa huduma ya supastaa huyo wa Liverpool.
Mo Salah mkataba wake huko Anfield utafika tamati mwishoni mwa msimu huu na bado hakuna makubaliano yoyote ya mkataba mpya wa kuendelea kubaki kwenye kikosi hicho kuafikiwa. Al-Hilal inaonekana kuwa mstari wa mbele kwenye mbio za kumsajili Mo Salah, ambaye amekuwa akifanya vizuri sana msimu huu.
Salah amekuwa akiweka wazi hali ya mambo yalivyo huko Liverpool, ambapo aliwahi kusema anavyojitazama anajiona kuwa yupo nje kuliko kuwa ndani kwenye kikosi hicho cha Anfield na alisema: “Hakuna kitu, bado tupo mbali sana, ngoja tusubiri tuone itakavyokuwa.”
Uhamisho wa Mo Salah kwenda Saudi Arabia umekuwa mchakato wa muda mrefu ambapo kwenye dirisha la majira ya kiangazi la kiangazi la mwaka jana, Liverpool inaripotiwa ilikataa ofa ya mkwanja mrefu kutoka kwenye moja ya timu zijazocheza ligi ya Saudi Pro League.
Lakini, sasa kama nchi msukumo umewekwa katika kurudi na ofa nono zaidi huko Anfield ili kumsajili Mo Salah.
Mwanamfalme Abdulaziz bin Turki Al-Faisal anaamini mkali huyo wa Liverpool ataachana na mikikimikiki ya Ligi Kuu England na kufuata nyayo za supastaa Cristiano Ronaldo kwenye kutumia fursa tofauti ya kukipiga huko Mashariki ya Kati.
Mastaa wenye majina makubwa wamekuwa wakihusishwa na mpango wa kwenda kukipiga Saudi Arabia, lakini usajili wa Mo Salah utakuwa mkubwa zaidi kufanywa na taifa hilo tangu Al Nassr ilipofanikiwa kunasa saini ya Ronaldo kutoka Manchester United.
Al-Hilal ina nafasi kwenye kikosi chao baada ya kusitisha mkataba wa Neymar.