Sababu Billinas kutoboa pua, kuvaa kipini

Muktasari:
- Hata hivyo, kwa sasa aina hii ya urembo imewafikia hata wanaume na baadhi hasa mastaa wameonekana wametoboa na kuvaa kipini.
KWA Tanzania imezoeleka,moja ya urembo kwa wanawake ni kutoboa pua na kuvaa kipini.
Hata hivyo, kwa sasa aina hii ya urembo imewafikia hata wanaume na baadhi hasa mastaa wameonekana wametoboa na kuvaa kipini.
Imeonekana kwa Diamondi Platnumz, Chid Benz, Marioo, S2Kiz na wengine wengi, ambao wamekuwa wakishambuliwa sana mitandaoni kwa kitendo hicho.
Sasa ni zamu ya William Nicholaus Lyimo ‘Billnas’ ambaye ametoboa pua na anavaa kipini.

Dakika 5 Na... lilimtafuta kujua sababu ya kufanya hivyo na hivi ndivyo ilivyokuwa...
Mwanaspoti: Hongera sana naona unamwonekano mpya wa kuvaa kipini. Nilikuona tangu mwaka jana nikajua umebandika tu.
Billinas: Asante sana, nimetoboa pua wala sijabandika kipini. Kuna gharama kubwa sana ambayo siwezi kuitaja.
Mwanaspoti: Unaona ni sahihi kwa mtoto wa kiume kutoga pua?
Billinas: Hiyo siyo nje ya muziki ni sehemu ya sanaa yangu kabisa, ni sehemu ya muziki wangu.
Mwanaspoti: Kuna mtu amekushawishi?
Billinas: Pamoja na mimi kupenda ila mtu aliyeniushauri ni S2kizz, aliniambia nikiwa na kipini puani nitakuwa na muonekano mpya kwa mashabiki zangu.

Mwanaspoti: Umekuwa na tabia ya kila baada ya muda kubadilisha muonekano wako hii imekaaje?
Billinas: Ni kweli na hii ni moja ya sehemu ya muziki, kama ulivyoona kipindi cha nyuma nilinyoa upara na hii fasheni ya upara ikabamba sana.
Mwanaspoti: Hongera kwa ngoma yako mpya ya ‘Boda’ uliyoshirikisha Mbosso naona inaendelea kufanya vizuri siku hadi siku, unazungumziaje mapokezi ya ngoma yako hiyo?
Billinas: Asante sana, Nashukuru sana Mungu kwa hilo ila pia shukrani nyingine ziende kwa mashabiki wangu maana bila wao mimi nisingekuwa hapa nilipo sasa.
Mwanaspoti: Hivi kwa ulipofikia sasa hivi kwenye muziki, unafanya shoo kuanzia bei gani?
Billinas: Mimi sasa hivi sifanyi shoo chini ya Sh20 milioni. Pia inategemea na mazungumzo sasa kama tukielewana nafanya ndiyo maana sasa hivi kwenda kwenye shoo ndogondogo nimepunguza kabisa.

Mwanaspoti: Tutegemee lini mtoto wa pili kwa mke wako Nandy?
Billinas: Mungu akipenda muda wowote, maana napenda sana kuwa na watoto wengi.