Prime
HISIA ZANGU: Mnyama alivyofanikisha itifaki katika ardhi ya Nelson Mandela

Muktasari:
- Jana Simba walikuwa jijini Durban kukamilisha itifaki katika jioni ambayo walicheza na Stellenbosch na kutinga fainali za kombe hilo. Hakukuwa na bao lolote lililohesabiwa kwa dakika 90 za pambano hilo, hivyo bao la Jean Charles Ahoua lililofungwa Unguja wiki moja iliyopita likasimama kama lilivyo.
KUTOKA Rustenburg hadi Durban Simba wamekamilisha itifaki. Ardhi ya Nelson Mandela imeubariki mpira wa Tanzania kwa mara nyingine tena. Yanga walisafiri hadi Rustenburg kucheza na Marumo Gallants na wakatinga fainali za Shirikisho Afrika miaka miwili iliyopita.
Jana Simba walikuwa jijini Durban kukamilisha itifaki katika jioni ambayo walicheza na Stellenbosch na kutinga fainali za kombe hilo. Hakukuwa na bao lolote lililohesabiwa kwa dakika 90 za pambano hilo, hivyo bao la Jean Charles Ahoua lililofungwa Unguja wiki moja iliyopita likasimama kama lilivyo.
Haikuwa mechi rahisi kwa Mnyama. Stellenbosch walikuwa wamebadilika tofauti na walivyocheza Unguja. Hawa wa jana walikuwa na kasi nzuri kwenda lango la Simba na kwa muda mwingi wa dakika 90 walikuwa bora zaidi.
Awali nilidhani Simba wangepambana kupata bao na kulitoa pambano kabisa katika mikono ya wenyeji wao, lakini maisha hayakuwa rahisi kama pambano la awali. Shukrani pia kwa matumizi ya teknolojia ya VAR.

Mara zote tatu VAR ilikuwa sahihi. Ilianzia kwa Kibu Denis wetu alipoleta janja janja ya kujigongesha kwa mguu wake kwa beki mmoja wa Stellenbosch, kisha akachupa kama anaingia katika bwawa la kuogelea. VAR ikawaokoa wenyeji.
Baada ya hapo ikawa zamu ya Simba. Ilipulizwa filimbi moja kuashiria penalti baada ya mchezaji mmoja wa Simba kuunawa mpira katika boksi. Ni kweli alikuwa ameunawa, lakini mpira uliugonga mkono ambao ulikuwa usawa mmoja na mwili. Ina maana kama mpira usingemgonga katika mkono bado ungeugonga mwili.
Kama mkono ungekuwa kando ya mwili na kuzuia mpira basi mwamuzi angekuwa sahihi. Mashabiki wengi wa Kitanzania waliokuwa Durban na wale waliokuwa wanatazama kutokea nyumbani wakashusha pumzi. Vinginevyo Stellenbosch wangekuwa wamerudisha bao la Ahoua.

Ukaja wakati mwingine mgumu, huku dakika zikiwa zimeyoyoma. Wenyeji wakatupia bao ambalo lilionekana kuwa zuri na sahihi. Bahati nzuri kwa Simba mzungu wa Stellenbosch aliyekuwa anasumbua kule mbele alikuwa ameotea kidogo wakati akipiga pasi ya kisigino kwa mfungaji. Tukashusha pumzi tena kupitia VAR.
Kuanzia hapo hakukuwa na nafasi tena kwa wenyeji kwa sababu mtaalamu wa kupoteza Moussa Camara alikuwa katika ubora wake langoni. Mwamuzi kutoka kwa Mafarao alipopiga filimbi historia ya Rustenburg ilikuwa imejirudia.
Sasa Simba itacheza fainali na RS Berkane ya Morocco katika mechi mbili za Casablanca na nadhani Uwanja wa Taifa. Hatuna uhakika kama pambano hilo litacheza Dar es salaam au Unguja, ingawa itakuwa vizuri zaidi likichezwa Dar es Salaam katika uwanja ambao utakuwa na mashabiki wengi zaidi kuliko Uwanja wa Amani.

Berkane? Ndiyo, ni ndoto inayotisha kidogo kwa namna nilivyowaona wakicheza na CS Constantine, timu ambayo ilikuwa katika kundi la Simba hatua ya awali. Mechi ya kwanza pale Morocco walishinda 4-0 safi kabla ya kuruhusu kufungwa 1-0 jana ile ile ambayo Simba walikuwa wakishinda Durban.
Kwa haki kabisa Berkane wapo juu ya Simba kimchezo, lakini fainali ni fainali tu. Simba wana muda wa kujiandaa na fainali hii. Kocha Fadlu Davids ana muda wa kuisoma Berkane na kujua aina ya mchezo wanaotumia. Hata hivyo, haitakuwa kazi rahisi kwa sababu Berkane watataka kumaliza mechi nyumbani kwao. Watataka kufanya kilekile walichokifanya kwa CS Constantine.
Kwa Simba fainali ni faraja tosha. Walikuwa wanaumia kuona picha za nahodha wa Yanga, Bakari Nondo Mwamnyeto akiwaongoza kina Fiston Mayele kwenda kuvaa medali za fainali pale Algeria. Simba na Yanga huwa wanashindana kila kitu.

Hata kitendo cha Yanga kufika fainali na kufungwa kilikuwa kinawaumiza. Kwamba hawakutaka hata hivyo fainali wafike. Na hata Yanga walishangaza kidogo licha ya kufungwa katika fainali, lakini walikuwa wanajivunia kufika fainali pengine kuliko kujali matokeo yenyewe.
Sasa Simba wameshusha pumzi. Nimeongea na Wanasimba wachache ambao hawajali sana kuhusu kitachotokea katika fainali. Kitu cha msingi kwao ilikuwa kufikia rekodi ya Yanga na kuwaziba mdomo. Kelele za fainali ya Yanga zilikuwa zinasumbua. Ni uhakika Simba watavaa medali ifikapo Mei mwishoni. Wawe mabingwa au washike nafasi ya pili, lakini wana uhakika wa kuvaa medali za CAF kama ambavyo mtani aliweza kufanya.

Kuna vitu viwili hapa. Kitu kizuri kwa Simba ni wamefanikiwa kufika fainali, huku wakiwa wanaamini bado wanatengeneza timu. Bado hawajafika katika ubora ule wa kina Jose Luis Miquisonne, Clatous Chama, Larry Bwalya, Hassan Dilunga, Meddie Kagere, John Bocco, Chris Mugalu na wengineo. Lakini wamefika fainali.
Kitu kizuri kwa taifa ni kwamba ndani ya misimu mitatu tumefika fainali mbili za Shirikisho. Majirani zetu na hata watu wa kule Afrika Kaskazini watakuwa wanaona tishio linalowakabili kwa soka la Tanzania. Tunakuja juu. Na wangejua kwamba moja kati ya sababu ya kuja juu ni ukweli humu ndani tunasukumana sana kupata mafanikio. Hakuna anayekubali kuchekwa.

Muda si mrefu fainali kama hizi tunaweza kucheza wenyewe kwa wenyewe katika uwanja wa Mkapa. Wakiendelea kuzubaa hata nusu fainali za Ligi ya Mabingwa tunaweza kujikuta tunacheza wenyewe kwa wenyewe.
Kitu cha msingi ni kwa matajiri wa klabu hizi kuendelea kutia pesa pale panapohitajika. Wasirudi nyuma. Huu ndio msingi pekee ambao umetunyanyua. Wachezaji wanaokuja sasa hivi wana ubora mwingine kuliko wale waliokuwa wanakuja zamani. Hata hivyo, wapo wachache ambao sio bora.