Prime
ARNE SLOT: Historia ya makocha hawa inamweka pabaya

Muktasari:
- Taji hilo ni la pili tangu msimu wa 2019/20 ilipobeba chini ya Klopp baada ya miaka 30 iliyotawaliwa na wapinzani wao Manchester United chini ya Kocha Sir Alex Ferguson.
LIVERPOOL, ENGLAND: UBINGWA una raha yake bana. Kwa sasa mashabiki wa Liverpool wanakenua baada ya kutwaa taji la Ligi Kuu England. Ni taji la 20 na la kwanza kwa Kocha Anrne Slot ukiwa ndiyo msimu wake wa kwanza tangu achukue mikoba ya Jurgen Klopp.
Taji hilo ni la pili tangu msimu wa 2019/20 ilipobeba chini ya Klopp baada ya miaka 30 iliyotawaliwa na wapinzani wao Manchester United chini ya Kocha Sir Alex Ferguson.
Kwa sasa miamba hiyo imelingana mataji huku Liverpool ikiizidi kwa mafanikio kwa kuwa na mataji mengi zaidi katika makabati yao.
Slot raia wa Uholanzi anaingia katika makocha walioweka ya kubeba taji la Ligi Kuu England katika msimu wao wa kwanza na katika orodha hiyo wapo makocha wengine wanne, Jose Mourinho, Carlo Ancelotti, Manuel Pellegrini na Antonio Conte.
Mtihani ulioko mbele yake ni kutetea ubingwa huo kwani rekodi zinaonyesha makocha wote walioshinda taji hilo msimu wao wa kwanza hawakudumu sana na kufutwa kazi. Hawa hapa...

Jose Mourinho (Chelsea – 2004/05)
Alianza kwa mafanikio makubwa msimu wake wa kwanza alipojiunga na Chelsea mwaka 2004 na alitoka kushinda ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na FC Porto.
Alipotua Chelsea alianza kwa kushinda Kombe la Carabao, kisha kuipa taji lao la kwanza la Ligi Kuu England baada ya mara ya mwisho kubeba msimu wa 1954/55 wakati huo likiitwa Daraja la Kwanza.
Msimu wake wa pili aliipa tena The Blues taji la pili la Ligi Kuu England na msimu wa tatu akashinda kombe la Carabao na FA.
Hata hivyo, mambo yalianza kumwendea kombo msimu wake wa nne na alitimuliwa Septemba 20, 2007, baada ya kuanza vibaya msimu.
Hata hivyo, Mourinho alirudishwa tena mwaka 2013 na kuisaidia kushinda taji lingine la Ligi Kuu England msimu wa 2014/15.
Iwapo Slot atashinda mataji mawili ya ligi na vikombe vitatu vya ndani misimu mitatu Anfield, kuna uwezekano akapewa muda zaidi ya ilivyokuwa Mourinho miaka 18 iliyopita.

Carlo Ancelotti Chelsea – (2009/10)
Alishinda taji la Ligi Kuu England katika msimu wake wa kwanza pamoja na taji la FA, ikiwa ni taji la tatu la ligi kwa Chelsea tangu Mourinho aondoke miaka mitano iliyopita.
Katika kipindi hicho hadi anatua katika kikosi hicho, Chelsea ilimaliza msimu bila taji wakati Mourinho alipotimuliwa na alikuja Avram Grant aliyeiongoza hadi fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na msimu uliofuata ilishinda Kombe la FA chini ya kocha wa muda Guus Hiddink, aliyemrithi Luiz Felipe Scolari.
Msimu wake wa pili alifukuzwa baada ya timu hiyo kumaliza nafasi ya pili katika msimamo wa ligi uamuzi ulioshangaza watu wengi kwa kuwa kocha huyu hakufanya vibaya sana kiasi cha kuondolewa.
Baada ya kuondoshwa hapa, Ancelotti alitimkia Paris Saint-Germain kabla ya kwenda Real Madrid, Bayern Munich, Napoli, Everton na kisha kurejea Real Madrid.

Manuel Pellegrini (Man City – 2013/14)
Katika msimu huo aliochukua ubingwa akiwa na Man City, Arsenal iliongoza ligi kwa muda mrefu kuliko timu yoyote lakini ikashindwa kuwa mabingwa.
Chelsea na Liverpool zilionyesha ushindani lakini zote zikaangukia pua na hatimaye Man City wakashinda.
Pellegrini alionekana kama mrithi wa muda mrefu wa Roberto Mancini na alidumu kwa misimu mitatu Etihad kabla ya kuondolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Pep Guardiola.
Msimu wake wa mwisho ulikuwa ni ule wa 2015/16 na Leicester ndiyo ilikuwa bingwa huku wao wakimaliza nafasi ya nne na kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa iliyokuwepo kati yao na Manchester United na alibeba taji la Carabao.
Kijumla, alishinda mataji matatu katika misimu mitatu lakini hiyo haikutosha kuwashawishi viongozi wa Man City kumbakisha.
Baada ya kuondoka Etihad, alitimkia Hebei ya China, kisha akarudi England akijiunga na West Ham na baadae kutimkia Real Betis alipo hadi sasa tangu mwaka 2020.

Antonio Conte (Chelsea – 2016/17)
Alishinda taji la kwanza Chelsea ikimaliza na pointi 93 pamoja na mabao 85.
Hata hivyo, msimu huo, licha ya kupata taji, Chelsea haikuanza vizuri ligi kwani ilitoka sare na Swansea na kufungwa na Liverpool na Arsenal, baada ya hapo Conte alibadilisha mfumo na kutumia mabeki watatu hali iliyosababisha washinde mechi 13 mfululizo.
Katika msimu wa pili, mambo yaliharibika kabisa kwani Chelsea ilishindwa kutetea taji lao kwa kiwango kilichotarajiwa.
Ilimaliza nafasi ya tano lakini ikapata heshima kwa kushinda Kombe la FA kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Manchester United.
Hili halikutosha kuokoa kibarua chake na akandoshwa yeye pamoja na benchi lake la ufundi na walilipwa fidia ya Pauni 26.6 milioni.
Chelsea haijashinda taji la ligi tangu Conte aondoke lakini imewahi kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu 2020/21.
Baada ya kuondoka Chelsea, Conte alitua Tottenham ambako mambo hayakwenda vizuri, baaaye alirudi Italia na kushinda taji la Serie A akiwa na Inter Milan na sasa anakinoa kikosi cha Napoli.