Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba v Stellenbosch hizi hapa dakika za mtego

Muktasari:

  • Timu hizo zinakutana katika mechi ya marudiano ya nusu fainali ya michuano hiyo itakayochezwa Uwanja wa Moses Mabhida uliopo Durban, Afrika Kusini kuanzia saa 10 jioni.

NI wazi dakika 45 za kwanza zitatoa picha ya timu ipi inaweza kusonga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika pale Stellenbosch itakapokuwa mwenyeji wa Simba, Jumapili hii.

Timu hizo zinakutana katika mechi ya marudiano ya nusu fainali ya michuano hiyo itakayochezwa Uwanja wa Moses Mabhida uliopo Durban, Afrika Kusini kuanzia saa 10 jioni.

Kocha wa Simba, Fadlu Davids anasisitiza katika mchezo huo wataingia kwa ajili ya kufunga bao ili kulinda ushindi wa nyumbani huku mpinzani wake,  Steve Barker akijibu mapigo kwa kusema ameandaa kikosi ambacho lazima kitikise nyavu.

Fadlu amesema katika mkakati wa kulinda ushindi wa nyumbani, ataingia kwenye mchezo huo kwa kushambulia zaidi huku akiamini dakika 10 za kwanza zitaamua - akitaka lipatikane bao kwa ajili ya kuwachanganya wenyeji wao.

Simba inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na mtaji wa ushindi wa bao 1-0 ilioupata katika mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar kupitia Jean Charles Ahoua aliyetikisa nyavu dakika ya 45+2 kwa pigo la faulo.

Katika mchezo huu, Simba inapaswa kulinda ushindi huo kwa kutowaruhusu wapinzani wao kupata bao kwani wakiwaacha wakifunga moja, itawalazimu kwenda hatua ya penalti kuamua mshindi.

“Tunakwenda kwenye mchezo wa marudiano tukiwa na lengo moja tu kutafuta bao la mapema na kumaliza kazi. Hatutacheza kwa kujilinda. Hatutacheza kwa woga. Hatutaki sare. Tunataka ushindi.

“Tumefanya uchambuzi wa kina na kubaini kinachohitaji kufanyika katika mechi ya marudiano. Sare nchini Afrika Kusini itatupeleka fainali, lakini hatuchezi kwa ajili ya kutafuta sare. Tunacheza ili kushinda, na hiyo ndiyo njia ya Simba.

“Tunajua haitakuwa rahisi kucheza ugenini. Hatujajiandaa kwa nusu fainali pekee bali tumejiandaa kushinda ubingwa wa michuano hii. Ninaamini tunaweza kufunga bao tukiwa Durban. Lengo letu la kutoruhusu bao nyumbani lilifanikiwa, lakini Simba ni klabu kubwa na klabu hazifurahii kupata ushindi mwembamba wakati nafasi za kufunga zaidi zipo,” alisema Fadlu.

Kocha wa Stellenbosch, Steve Barker alisema kiwango walichoonyesha mechi ya kwanza licha ya kupoteza kinawapa matumaini ya kupindua matokeo, hivyo wataingia kwa kushambulia zaidi kupata bao la mapema. “Tulikuwa timu imara zaidi ugenini na tulijaribu kupata bao, ikashindikana, nina imani sana kwamba mechi ya pili tutafunga na kuingia fainali.

“Ingawa hakuna uhakika kwamba tutafika fainali, lakini kulingana na kile nilichokiona mechi ya kwanza, Simba inafungika vizuri tu,” alisema.

Kutokana na kila kocha kuhitaji bao la mapema, ni wazi tutashuhudia dakika 45 za kwanza zikiwa na kasi ya kusaka mabao ya kuamua mechi.

Wakati makocha hao wakitambiana, takwimu zinaonesha mfungaji wa bao katika mchezo wa kwanza, Jean Charles Ahoua, ana maajabu yake kwenye michuano hiyo msimu huu kupitia mabao yake matatu aliyofunga hadi sasa.

Nyota huyo ambaye yupo sawa kwa mabao na Kibu Denis ambao ndiyo vinara wa Simba, kila anapofunga basi timu yake inaondoka na ushindi wa 1-0.

Ahoua alianza kufunga nyumbani katika mchezo wa kwanza hatua ya makundi dhidi ya Bravos do Maquis, Simba ikashinda 1-0, kisha akafunga lingine dhidi ya CS Sfaxien ugenini na Simba kujihakikishia nafasi ya kucheza robo fainali. Katika mchezo huo, Simba ilishinda 1-0.

Bao la tatu Ahoua amelifunga katika mchezo wa nusu fainali ya kwanza nyumbani dhidi ya Stellenbosch, Simba ikishinda 1-0. Katika mabao yote hayo, Ahoua ameyafunga kipindi cha kwanza.

Mbali na kimataifa, pia Ahoua ndiye kinara wa mabao Simba katika Ligi Kuu Bara msimu huu akifunga 12.

Katika mabao hayo 12 aliyofunga Ahoua, ni mechi moja pekee dhidi ya Kagera Sugar ndiyo kikosi chake hakijaondoka na clean sheet huku zingine zote alizofunga, dakika tisini zilimalizika bila Simba kuruhusu bao.

Mechi za ligi alizofunga Ahoua ni dhidi ya Fountain Gate (4-0, alifunga moja), Dodoma Jiji (0-1, alifunga bao pekee), Namungo (3-0 alifunga moja), KMC (4-0, alifunga mawili), Kagera Sugar (2-5, alifunga moja), JKT Tanzania (1-0 alifunga bao pekee), Tanzania Prisons (3-0, alifunga moja), Namungo (0-3, alifunga mawili), Dodoma (6-0, alifunga mawili).


HALI ZA TIMU

Kipa namba moja na nahodha wa Stellenbosch, Sage Stephens anatarajiwa kuwepo katika mchezo huu baada ya kukosekana ule wa kwanza kufuatia kutokuwa fiti, huku nafasi yake ikichukuliwa na Oscarine Masuluke.

Lehlohonolo Mojela na Ashley Cupido wote ni majeruhi, wanatarajiwa kuendelea kukosekana.

Kikosi cha Stellenbosch kinatarajiwa kuwa hivi; Sage Stephens, Enyinnaya Godswill, Fawaaz Basadien, Thabo Moloisane, Ismael Olivier Touré, Genino Palace, Sihle Nduli, Thato Khiba, Devin Titus, Lesiba Nku na Andre de Jong.

Kwa upande wa Simba, Chamou Karaboue ambaye aliumia mechi iliyopita, afya yake imeimarika hivyo anatarajiwa kuwepo, huku kukiwa hakuna taarifa ya kukosekana nyota yeyote kutoka wale waliocheza mechi ya kwanza.

Kikosi cha Simba kinatarajiwa kuwa hivi; Moussa Camara,  Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Abdulrazack Hamza, Chamou Karaboue, Fabrice Ngoma, Yusuph Kagoma, Kibu Denis, Jean Charles Ahoua, Elie Mpanzu na Steven Mukwala.