Chama Lako limefundishwa na makocha wangapi?

Muktasari:
- Katika mabadiliko hayo wapo makocha waliolazimika kuondoshwa kufuatia matokeo mabaya ya vikosi vyao, lakini wengine wakiwa na sababu zao binafsi. Wakati Tabora United ikiongoza kwa kuwa kinara wa mabadiliko hayo ikifundishwa na makocha wanne, Yanga na Singida Black Stars zinaifuata.
KUNA timu tatu vinara zilizokimbizana kutimua makocha na kuajiri wengine ndani ya msimu huu wa Ligi Kuu Bara, lakini pia zipo tatu zilizokomaa zikionyesha zitamaliza na makocha wanne walewale zilioanza nao.
Katika mabadiliko hayo wapo makocha waliolazimika kuondoshwa kufuatia matokeo mabaya ya vikosi vyao, lakini wengine wakiwa na sababu zao binafsi. Wakati Tabora United ikiongoza kwa kuwa kinara wa mabadiliko hayo ikifundishwa na makocha wanne, Yanga na Singida Black Stars zinaifuata.
TABORA UNITED
Tabora United ilianza msimu na Mkenya Francis Kimanzi, lakini hakufikisha mechi 10 licha ya kuanza vizuri kwani mambo yalibadilika na kulazimika kuachia ngazi, kisha akashushwa Mkongomani Anicet Kiazayidi ambaye hakufanikiwa kudumu akiwa na mwanzo mzuri kama mtangulizi wake, lakini akaondoshwa kimyakimya.
Baada kuondoka kwa Mkongomani huyo akashushwa Mzimbabwe Genesis Mangombe aliyeiongoza katika mechi nne akipoteza zote, lakini naye akaikimbia timu hiyo kabla ya sasa kuletwa Mzambia Simona Kaunda, akiwa ameshapoteza mechi ya kwanza.
YANGA
Yanga inaifuta Tabora United kwa kuachana na makocha msimu huu, kwani mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara tofauti na miaka mingi iliyopita wameingia kwenye historia ngumu ya kulazimika kubadilisha makocha, wakiwa tayari wameshaajiri makocha watatu ndani ya msimu mmoja.
Yanga ilianza msimu na Miguel Gamondi ambaye alipopoteza mechi mbili za ligi dhidi ya Azam na Tabora United kibarua chake kiliingia matatani akalazimika kukubaliana kusitisha mkataba wake akiwa ametoka kuipa mafanikio ya ubingwa mara moja na kuifikisha robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliotangulia. Hata hivyo, hilo halikusaidia kubakizwa.
Kuondoka kwa Gamondi kulifanya aletwe Sead Ramovic ambaye aliiongoza Yanga kwenye mechi 12 za mashindano yote kisha akatangaza kutimka alipopata ofa ya kwenda kuifundisha CR Belouizdad ya Algeria.
Kuondoka kwa Ramovic Yanga kukaifanya imchukue kocha wa Singida Black Stars, Hamdi Miloud ambaye ndiye anayeiongoza kwa sasa.
SINGIDA BLACK STARS
Pembeni ya Yanga Kuna Singida Black Stars ambao wamebadilisha makocha mara tatu wakianza msimu na Mbelgiji Patrick Aussems ambaye aliiongoza timu hiyo kwenye mechi 11 za ligia akianza vizuri, lakini sare mbili za mwisho dhidi ya Coastal Union nyumbani na ugenini dhidi ya Tabora United zikamfanya aondoshwe.
Kuondoka kwa Aussems kukaifanya Singida Black Stars iongozwe kwa muda na mkurugenzi wake wa Ufundi, Ramadhan Nsanzurwimo, kabla ya kushushwa Miloud ambaye kabla hata ya kuanza ligi Yanga ikamchukua kisha timu hiyo kutua kwa Mkenya David Ouma.
KAGERA SUGAR
Kagera Sugar pia wamo kwani wamefundishwa na makocha watatu msimu huu wakianza Mganda Paul Nkata aliyeongoza timu hiyo katika mechi chache za kwanza akianza vibaya na baadaye kutimuliwa.
Kutimuliwa kwa Nkata kukaifanya timu hiyo imlete Mmarekani Mellis Medo aliyetokea Mtibwa Sugar ambaye naye alianza kuonyesha mwanga, lakini mambo yakabadilika baadaye na kujiondoa kisha akashushwa Juma Kaseja ambaye anapambana na timu hiyo isishuke daraja.
KENGOLD
KenGold ipo kwenye kundi la timu tisa zilizofundishwa na makocha wawili ambapo walianza na Fikirini Elias ambaye mapema tu alipoona mambo magumu alirusha taulo na kuamua kujiweka kando mwenyewe kisha jahazi hilo likatua kwa Omar Kapilima, ambaye matokeo ya kupoteza ugenini majuzi dhidi ya Coastal Union 2-1 yaliishusha timu hiyo kwenda Championship ikiwa mikononi mwake.
MASHUJAA
Mashujaa wapo katika kundi hilo la makocha wawili wakianza msimu na Mohamed Abadallah ‘Baresi’ ambaye alikomaa na timu hiyo kabla ya kufukuzwa hivi karibuni na akashushwa Salum Mayanga ambaye anaendelea kupambana na kikosi hicho.
NAMUNGO
Namungo ya Ruangwa mkoani Lindi msimu huu ilianza maisha na kocha Mkongomani Mwinyi Zahera, lakini mwendo wao haukuwa mzuri ukiwa wa kupepesuka ukamuondoa na kumsukumia kwenye idara ya ufundi.
Kuondolewa kwa Zahera kuliifanya timu hiyo imshushe Juma Mgunda ambaye anaendelea kupambana na hali yake na timu hiyo ikiwa bado haina mwendelezo bora wa matokeo mazuri ikishinda na kuanguka.
PAMBA JIJI
Pamba Jiji ilirejea Ligi Kuu msimu huu ikionyesha hesabu nzuri za kutaka kufanya vizuri ikiwa chini ya kocha Goran Kopunovic, lakini mambo hayakuwa kama ilivyotarajiwa ilikutana na matokeo mabaya mpaka ikaamua kumtimua kocha huyo.
Kuondoka kwa Kopunovic kukaifanya imchukue Freddy Minziro ambaye aliibadilisha na kurudisha makali ikianza kuonyesha matumaini ya kusalia katika ligi msimu ujao.
FOUNTAIN GATE
Fountain Gate baada ya kuanza vizuri chini ya Mohammed Muya timu hiyo ikionyesha ubabe, lakini baadaye mambo yalibadilika na kocha huyo kutimuliwa akiwa na benchi zima la ufundi, na kuondoka kwake kukaifanya imshushe Mkenya Robert Matano ambaye anaendelea kupambana.
TAZANIA PRISONS
Tanzania Prisons nako mambo sio mazuri sana, ikifundishwa na makocha wawili wazawa tofauti ambapo ilianza na Mbwana Makata ambaye alifanikiwa kumaliza nusu msimu tu, lakini mzunguko uliofuata akaondoshwa na kupewa Amani Josiah ambaye anaendelea kupigania kubaki Ligi Kuu msimu ujao.
COASTAL UNION
Wagosi ‘Coastal Union’ wamo msimu huu, kumbuka ilicheza Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza na kuondoshwa mapema tu, ila walianza msimu na Ouma, lakini baadaye wakaachana na kocha huyo akaletwa Juma Mwambusi ambaye naye matokeo mabaya yalimng’oa na sasa kikosi hicho kipo chini ya kocha msaidizi Joseph Lazaro.
AZAM
Matajiri Jiji la Dar es Salaam, Azam, msimu huu wanaonyesha mambo hayatakuwa mazuri kama walivyotarajia ambapo walianza msimu na Youssouph Dabo aliyewapa nafasi ya pili msimu uliopita.
Matarajio ya Azam yalikuwa msimu huu Dabo angelifuata taji la ubingwa, lakini haikuwa hivyo akianza vibaya kisha kuamua kutemana na kocha huyo Msenegali na kumleta Mmorocco Rachid Taoussi ambaye naye upepo sio mzuri sana akiendelea kupambana na kikosi chake.
KMC
Watoza ushuru wa Kinondoni - KMC - wameishi msimu huu na makocha wawili, na mbaya zaidi kwao ni Yanga ambao ‘waliwanyang’anya’ aliyekuwa kocha wao Abdihamid Moallin, raia wa Marekani mwenye asili ya Somalia hatua ambayo iliwakera mabosi. Kuondoka kwa Moallin alipewa ajira Kally Ongala ambaye anaendelea kupambana na timu hiyo.
SIMBA
Simba ni miongoni mwa timu tatu ambazo zimeishi msimu huu na kocha mmoja ikiwa chini ya Fadlu Davids, huku mambo yakionekana kuwa safi kwao ikiwa inawania mataji yote matatu inayoyapigania na sasa ikiwa kwenye nusu fainali mbili yaani ile ya Kombe la Shirikisho Afrika (inayocheza mechi ya pili leo) na Kombe la Shirikisho (FA), lakini pia ipo nafasi ya pili kwenye ligi.
JKT TANZANIA
JKT Tanzania imeendelea kupambana ikiwa na kocha Ahmad Ally iliyeanza naye msimu ikimchukua mwisho wa msimu uliopita kutokea Prisons.
DODOMA JIJI
Wakali wa makao makuu ya nchi, Dodoma Jiji wanaendelea kukomaa na kocha Mecky Maxime wakishika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi ambapo kocha huyo walianza naye msimu huu.
WASIKIE HAWA
Akizungumzia uhusiano wa makocha na timu, mchezaji wa zamani wa Simba, Dua Said anasema Simba msimu huu imeanza ikiwa moto kutokana na mabadiliko makubwa iliyofanya hasa eneo la benchi la ufundi.
“Moja kati ya vitu vikubwa vilivyoijenga Simba kwa sasa ni falsafa ya kocha Fadlu Davids ambaye amekuwa na kikosi hicho tangu mwanzo wa msimu. Simba sasa iko vizuri, kwani uwepo wa kocha mmoja unaiongezea nafasi ya wachezaji kuelewa mfumo na mbinu za mwalimu na mwisho lazima watafika mbali,” anasema mkongwe huyo na kuongeza:
“Nikumbushe wakati wa kocha Nabi (Nasreddine), Yanga ilifika mbali kwani ndani ya misimu miwili kikosi kilishajua kila mbinu na benchi la ufundi lilikuwa na utulivu wa kusoma kila timu ya Ligi Kuu ndio maana walifanikiwa. Tunakubaliana kuwa kila mwalimu ana mbinu zake, hivyo wakibadilishwa wachezaji lazima wavurugike hata kama wana uwezo mkubwa kwa sababu kabla hajashika vizuri mbinu hizi analetewa zingine.”
Lakini, kupitia Mwanaspoti, kiungo wa Yanga, Stephane Aziz KI aliwahi kusema kuwa mojawapo kati ya sababu zilizochangia kushuka kwa kiwango chake msimu huu ni pamoja na mabadiliko ya makocha.
“Kila kocha anakuja na mbinu zake, kwa hiyo kabla hujatulia kumuelewa unabadilishiwa mwingine, jambo ambalo limewaathiri mastaa wengi,” alikaririwa Aziz KI katika moja ya mahojiano na Mwanaspoti.
Aziz ambaye msimu uliopita alibeba tuzo ya ufungaji bora akiwa na mabao 21, lakini huu amefunga manane na asisti saba, huku Yanga ikisalia na mechi nne mkononi.