Prime
Rekodi zinaisogeza Simba fainali CAFCC

Muktasari:
- Simba itashuka kwenye Uwanja wa Moses Mabhida, uliopo jijini Durban kuanzia saa 10:00 jioni (kwa saa za Afrika Mashariki) kurudiana na Stellenbosch huku ikiwa na hazina ya ushindi wa bao 1-0 iliyopata nyumbani wikiendi iliyopita zilizovaana Uwanja wa New Amaan, Zanzibar.
SIMBA inahesabu saa tu kwa sasa kabla ya kushuka uwanjani kukabiliani na Stellenbosch ya Afrika Kusini katika mechi ya marudiano ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, huku rekodi zikiibeba mapema dhidi ya wenyeji katika mechi hizo za kimataifa na hata katika mechi 10 zilizopita nyumbani.
Simba itashuka kwenye Uwanja wa Moses Mabhida, uliopo jijini Durban kuanzia saa 10:00 jioni (kwa saa za Afrika Mashariki) kurudiana na Stellenbosch huku ikiwa na hazina ya ushindi wa bao 1-0 iliyopata nyumbani wikiendi iliyopita zilizovaana Uwanja wa New Amaan, Zanzibar.
Lakini kabla ya mchezo huo, kuna ukweli mmoja unaoipa Simba nguvu mpya, nayo ni udhaifu wa wenyeji hao, Stellenbosch kuruhusu mabao 12 katika mechi za kimataifa, huku pia rekodi za uwanja wa nyumbani kwa mechi 10 zilizopita za mashindano yote ikiwaangusha kulinganisha na ubabe wa Simba ugenini kwa msimu huu katika michuano hiyo ya CAF.

Tuanze na mechi 10 zilizopita za michuano yote, Stellenbosch inayoshiriki michuano ya CAF kwa mara ya kwanza msimu huu, imeshinda mitatu tu, ikitoka sare tano na kupoteza mbili, lakini ikifunga mabao tisa na kufungwa manane.
Lakini kwa mechi 13 za kimataifa ilizocheza hadi sasa, Stellenbosch imeshinda saba, ikiwamo nne za nyumbani na kutoka sare mbili, ikiwamo moja ya nyumbani na imepoteza mara nne ikiwa moja ya nyumbani, huku ikifunga jumla ya mabao 18 na yenyewe kufungwa 12. Nyumbani imefunga mabao 12 na kufungwa matatu tu, lakini ugenini ikifunga sita na kufungwa manane.
Takwimu zinaonyesha namna timu hiyo inavyofungika na Simba ikikomaa inaweza kunufaika.

Mabao matano kati ya hayo 10 yalitokana na pasi mpenyezo kutoka katikati au pembeni mwa uwanja jambo linaloashiria kuwa safu yao ya ulinzi ambayo imekuwa ikiundwa na Fawaaz Basadien, Ismael Olivier Toure, Thabo Moloisane na Enyinnaya Godswill ina changamoto katika kukaba maeneo ya hatari na kushughulikia mipira ya kasi inayokuja kwa ustadi.
Katika mchezo wa pili katika hatua ya makundi dhidi ya RS Berkane waliopoteza kwa 5-0, mabao yote matano yalitokana na makosa haya, jambo linalotoa nafasi kwa Simba kutumia ubunifu wa wachezaji wao kama Charles Jean Ahoua, Elie Mpanzu na Kibu Denis.
Tatizo hilo la ulinzi halikomei hapo. Mabao mengine matatu walifungwa kupitia faulo mawili dhidi ya RS Berkane katika mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi wakati wakipoteza kwa mabao 3-1 na moja kutoka kwa Simba kwenye Uwanja wa Amaan ambalo walifungwa na Ahoua.

Uwepo wa wachezaji wenye ubora mkubwa wa kupiga mipira iliyokufa ndani ya kikosi cha Simba, hasa Ahoua, ni silaha inayopaswa kutumika tena. Stellenbosch si wazuri kwenye kupanga ukuta wala katika kusoma mwelekeo wa mipira hiyo.
Hakuna timu inayotaka kuruhusu penalti, lakini Stellenbosch walifanya kosa hilo dhidi ya AS Vita katika hatua ya makundi na kujikuta wakilazimishwa sare ya 1-1. Mchezo huo unaonyesha kuwa mabeki wao huwa na wakati mgumu wanapobanwa, na hulazimika kufanya madhambi ndani ya eneo la hatari jambo ambalo Simba wanaweza kulilazimisha kupitia ujanja wa washambuliaji wake.
Katika kipigo kingine cha 3-1 walichopata na RS Berkane, bao la tatu lilikuwa ni shuti kutoka nje ya eneo la hatari. Safu ya ulinzi ya Stellenbosch ilionekana kuruhusu nafasi kwa wapinzani kupiga mashuti ya mbali na hilo ni pengo ambalo wachezaji wa Simba wanaopenda kujaribu mashuti kama Mpanzu au Ahoua wanaweza kulitumia kufunga.

Simba, tofauti na wapinzani wao, imeonyesha uimara mkubwa barani Afrika kwa msimu huu kwani katika mechi tano za ugenini, imeshinda mbili, kutoka sare mbili na kupoteza mbili vilevile, huku ni mechi mbili pekee ilizoshindwa kufunga bao lolote.
Simba ilianza michuano hiyo katika raundi ya pili kwa kutoka suluhu mjini Tripoli, Libya dhidi ya Al Ahli Tripoli, kisha ikapoteza 2-1 mbele ya CS Constantine ya Algeria na kushinda 1-0 mbele ya CS Sfaxien ya Tunisia na kutoka sare ya 1-1 na Bravos ya Angola kabla ya kupasuka 2-0 kwa Al Masry ya Misri ikiwa ni hatua ya robo fainali. Katika mechi hizo sita za ugenini Simba imefunga mabao matatu na kufungwa matano, lakini kwa mechi 10 za mwisho ikiwa ugenini kwa michuano yote, Simba imeshinda sita na kupate sare mbili kama ilizopoteza, lakini ikifunga mabao 19 na kufungwa manane tu.

UTAMU ZAIDI
Kwa timu hizo zinazokutana kesho kuamua nani aende fainali ili kukutana na mshindi wa mchezo wa nusu fainali nyingine itakayopigwa kuanzia saa 1:00 usiku hiyo kesho kati ya wenyeji CS Constantine ya Algeria na Berkane ya Morocco, takwimu mbalimbali bado zinawabeba mastaa wa Simba zaidi kuliko wa Stellenbosch, jambo linaloweza kuwapa faida kubwa ikiwa watacheza kwa nidhamu ya hali ya juu.
Tukianzia na kwenye vita ya ufungaji, Kibu Denis anashika nafasi ya tatu kwa nyota waliofunga mabao mengi katika Kombe la Shirikisho msimu huu, baada ya kufunga matatu, akizidiwa na Oussama Lamlioui wa RS Berkane ya Morocco mwenye manne.
Mabao ya Oussama ni sawa na ya nyota wa Enyimba, Ifeanyi Ihemekwele ambaye tayari timu hiyo imeshatolewa kwenye michuano hiyo nyuma ya kinara, Ismail Belkacemi wa USM Alger ya Algeria aliyefunga matano ingawa kikosi hicho kimeshatolewa pia.

Katika kutengeneza mabao, nyota wa Simba pia wamefanya vizuri ambapo kiungo mshambuliaji wa kikosi hicho, Jean Charles Ahoua amechangia mawili, japo kiujumla hadi sasa amehusika na mabao matano, baada ya kufunga matatu na kuasisti mawili.
Kwa maana hiyo, kwa nyota waliochangia mabao mengi, Ahoua anashika nafasi ya tatu, akichangia matano sambamba na Oussama Lamlioui na Issoufou Dayo wote wakiichezea RS Berkane, nyuma ya nyota, Brahim Dib wa CS Constantine aliyechangia sita.
Kinara aliyehusika na mabao mengi ya kufunga na kuasiti ni Ismail Belkacemi wa USM Alger aliyechangia saba, baada ya kiungo huyo mshambuliaji kufunga matano akiwa ndiye anaongoza na kuchangia pia upatikanaji wa mengine mawili hadi sasa.

Kwa wachezaji walioonyeha viwango vizuri hadi sasa kwa mujibu wa mtandao wa FotMob, Jean Charles Ahoua anashika nafasi ya tatu akiwa na 7.76, nyuma ya Oussama Lamlioui wa RS Berkane mwenye 7.77 na Ismail Belkacemi wa USM Alger mwenye 8.30.
Kwenye nyota waliotengeneza nafasi nyingi hadi sasa, Jean Charles Ahoua anaongoza akiwa ametengeneza 27, nyuma ya Brahim Dib wa CS Constantine aliyetengeneza 22, huku kiungo mshambuliaji, Yassine Labhiri wa RS Berkane akitengeneza nafasi 21.
Kwa upande wa makipa wanaongoza kwa kutoruhusu mabao 'clean sheets', Moussa Camara wa Simba anashika pia nafasi ya pili akiwa na tano sawa na kipa wa Stellenbosch, Sage Shane Stephens aliyeukosa mchezo wa mkondo wa kwanza visiwani Zanzibar.

Kipa anayeongoza ni Munir Mohamedi wa RS Berkane mwenye 'Clean Sheets' saba hadi sasa na kukiweka kikosi hicho katika nafasi nzuri ya kutinga fainali, baada ya mchezo wao wa kwanza kushinda mabao 4-0, dhidi ya CS Constantine ya Algeria.
Katika makipa wanaongoza kwa kuokoa michomo mingi golini mwao, Camara anashika nafasi ya saba akiwa na 73.9%, nyuma ya Sage Shane Stephens wa Stellenbosch mwenye 77.3%, huku Nayan Sena Rodrigues wa CD Lunda Sul ya Angola akiwa na 77.8%.
Makipa wengine wanaofuatia ni Mohamed Awad wa Zamalek ya Misri mwenye 78.9%, huku Oussama Benbot wa USM Alger ya Algeria akishika nafasi ya pili akiwa na 80.0%, wakati kinara ni Munir Mohamedi anayeichezea RS Berkane ya Morocco mwenye 83.3%.

Kwa upande wa nyota waliopiga pasi sahihi, Fabrice Ngoma wa Simba anaongoza akiwa amepiga 453, nyuma ya Messala Merbah wa CS Constantine ya Algeria aliyepiga 422, akifuatiwa na Ahmed Abou El Fotouh wa Zamalek SC ya Misri mwenye pasi 419.
Katika nyota 10 bora waliopiga pasi sahihi katika michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, Simba ina wachezaji wawili ambapo mbali na Ngoma mwingine ni beki, Abdulrazack Hamza anayeshika nafasi ya tano akiwa na usahihi wa pasi 411.
Kwa takwimu hizo wachezaji wa Simba wametokea katika kila idara wakiwa wanaongoza au kushika hata nafasi tatu za juu, tofauti na wapinzani wao, Stellenbosch ambao wameonekana kubebwa zaidi na kipa wa kikosi hicho, Sage Shane Stephens.

CHAMOU ATULIZA PRESHA
Katika hatua nyingine ile hofu iliyokuwa imetanda juu ya afya ya beki wa kati ya Simba, Chamou Karabou aliyeumia kwenye mchezo wa kwanza wa nusu fainali na kushindwa kumaliza dakika 90 inaelezwa mambo yapo freshi na kulipunguzia presha benchi la ufundi la timu hiyo.
Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar na kumalizika kwa wenyeji Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0, Chamou aliumia na nafasi yake kuzibwa na kiungo mkabaji, Yusuf Kagoma.
Hata baada ya mchezo huo, beki huyo raia wa Ivory Coast alionekana akishika pua huku akigulia maumivu makali wakati akiingia kwenye basi la timu, jambo lililowatia wasiwasi mashabiki wengi wa Msimbazi waliohisi huenda jamaa angelikosa pambano la kesho Jumapili.
Hata hivyo, habari njema ni kwamba beki huyo ametua Afrika Kusini akiwa sehemu ya kikosi cha wachezaji waliokwenda kumalizia kazi. Uwepo wake ni faraja kwa kocha Fadlu Davids ambaye amekuwa akimtegemea kwa kiasi kikubwa katika ukuta wa kati tangu kuumia kwa Che Malone Fondoh ambaye naye ameanza kupiga tizi taratibu na wenzake kuashiria anaendelea vyema kwa sasa.
Daktari wa Simba, Edwin Kagabo, alithibitisha kuwa majeraha aliyopata Chamou hayakuwa makubwa kama ilivyodhaniwa awali na kwamba aliweza kuruhusiwa kushiriki mazoezi kabla ya kusafiri na timu.
“Karabou (Chamou) alipatwa na shida kidogo kufuatia kugongana na mshambuliaji wa Stellenbosch, lakini hali yake imeimarika na yuko fiti kwa mechi ya marudiano,” alisema Kagabo.
Kwa upande wa Chamou alieleza kuwa tayari amepona kwa kiasi kikubwa na anataka kuwajibika kama ilivyo kawaida yake. “Ninajisikia vizuri zaidi sasa. Nafanya mazoezi na timu, na kama kocha atanipa nafasi, niko tayari kupigana kwa ajili ya Simba kufika fainali,” alisema.
MAKOCHA
Fadlu Davids wa Simba alisema; "Hatuangalii matokeo ya mchezo uliopita, kwa sasa akili zetu tumezielekeza katika mechi ijayo, tunatambua wazi ni ngumu kwa sababu tumewaona jinsi walivyocheza kwetu hasa kipindi cha pili, hivyo tutacheza kwa tahadhari na nidhamu kubwa."
Kuhusu Chamou, alikiri kwamba uwepo wa beki huyo wa kati ni jambo linaloongeza chaguo muhimu kwenye safu ya ulinzi. “Chamou ni mchezaji wa kiwango cha juu na anatoa utulivu mkubwa kwenye beki ya kati. Kuwa naye tena kikosini ni faida kubwa kwetu,” alisema Fadlu.
Chamou amekuwa akicheza sambamba na Abdulrazack Mohamed Hamza katika eneo la beki ya kati, wakisaidiana kudhibiti mashambulizi ya wapinzani. Kombinesheni hiyo imesaidia Simba kuwa na ukuta imara katika mechi za hivi karibuni za Kombe la Shirikisho.
Tangu Che Malone aumie, wengi walitarajia pengo lake lingeathiri uimara wa safu ya ulinzi, lakini Chamou ameibuka kuwa shujaa mpya wa ukuta wa Msimbazi, akicheza kwa utulivu, nguvu na akili nyingi za kusoma mchezo.
Katika mchezo dhidi ya Stellenbosch uliopita, Chamou alifanya kazi kubwa kuhakikisha washambuliaji wa wapinzani hawapati nafasi nyingi za kufunga, kabla ya kulazimika kutolewa kutokana na kuumia.
Kwa upande wa kocha wa zamani wa Simba SC, Dylan Kerr, ambaye aliwahi kuiongoza timu hiyo mwaka 2015, ametoa maoni yake kuhusu mchezo huo wa marudiano.
"Simba wana nafasi nzuri ya kufuzu fainali. Stellenbosch ni timu nzuri lakini wana mapungufu katika safu ya ulinzi ambayo Simba inaweza kuyatumia. Ni muhimu kwa Simba kucheza kwa nidhamu na kutumia nafasi zao vizuri."
Kerr, ambaye pia amewahi kuifundisha Gor Mahia na timu nyingine kadhaa barani Afrika, aliongeza kuwa uzoefu wa Simba katika mashindano ya kimataifa unaweza kuwa faida kubwa katika mchezo huo wa marudiano ambapo Simba inawinda rekodi ya kurudia rekodi iliyoweka kwa kufika fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993 na kupoteza mbele ya Stella Abidjan ya Ivory Coast kwa mabao 2-0.
Michuano hiyo ndiyo iliyokuja kuunganishwa na ile ya Kombe la Washindi Afrika mwaka 2004 na kuzaliwa kwa Kombe la Shirikisho Afrika la sasa ambalo ni Yanga pekee iliyofika fainali kwa timu za Tanzania ikifanya hivyo 2022-2023 na kupoteza mbele ya USM Alger ya Algeria kwa kanuni ya bao la ugenini baada ya matokeo ya jumla kuwa sare ya 2-2, ikipoteza nyumbani 2-1 na kushinda ugenini 1-0.