Simbu arejea nchini, ataja siri ya kung'ara Boston Marathon

Muktasari:
- Mbio hizo zilifanyika April 21, 2025 jijini Boston ambapo Simbu alimaliza wa pili akitumia muda wa 2:05:04 na kuwa Mtanzania wa pili kushika nafasii hiyo kwa mbio hizo baada ya Gabriel Geay kufanya hivyo mwaka 2013.
Mwanariadha wa Kimataifa wa Tanzania, Alphonce Simbu, leo Aprili 24, 2025 amerejea nchini akitokea Marekani alikokwenda kushiriki mbio za Boston Marathon huku akisema siri ya kufanya vizuri imetokana na jitihada kubwa ambazo amekuwa akifanya kwa kushirikiana na wenzake kwenye mazoezi lakini pia kufuata maelekezo ya mwalimu.
Mbio hizo zilifanyika April 21, 2025 jijini Boston ambapo Simbu alimaliza wa pili akitumia muda wa 2:05:04 na kuwa Mtanzania wa pili kushika nafasii hiyo kwa mbio hizo baada ya Gabriel Geay kufanya hivyo mwaka 2013.
Akizungumza baada ya kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Simbu amesema mbio hazikuwa rahisi kutokana na ushindani uliokuwepo baina ya wanariadha kutoka mataifa mengine ambao walishiriki.
"Nimpongeze Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake ambazo amekuwa akifanya kuhakikisha michezo nchini inapiga hatua, pia nimefurahi sana kwa sababu baada ya ushindi huu alinipongeza.

"Pia Mkuu wa Majeshi kwa jitihada kubwa ambazo anafanya kwetu wanariadha ambapo tumekuwa tukipata muda mzuri wa kufanya mazoezi na kuiwakilishi nchi vyema Kimataifa," amesema Simbu.
Naye kocha wa timu ya riadha ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), mteule daraja la pili , Antony Mwingereza, amesema siri ya Simbu kufanya vizuri Boston Marathon ni kujituma kwa bidii kwenye mazoezi kwa kushirikiana na wenzake lakini pia kumtanguliza Mungu kwenye kila jambo analofanya.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Utimamu wa Mwili, Michezo, Sanaa na Utamaduni Makao Makuu ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) ambaye pia ni Mkuu wa Shule ya Mafunzo ya Utimamu wa Mwili na Michezo iliyopo wilayani Monduli mkoani Arusha, Kanali John Nyanchoa, amempongeza Simbu kwa jitihada zake za kuitangaza nchi Kimataifa kupitia michezo.

Amesema Simbu ni mtu ambaye anajituma, mwaminifu na mwadilifu jambo ambalo limemfanya aendelee kung'ara katika mashindano mbalimbali anayoshiriki.
Kanali Adam Kimaro ambaye ni mwakilishi wa Brigedia Komandi 303 KJ, amesema kama Jeshi na Taifa ni jambo la kufurahia kuona mwanariadha wao anafanya vizuri Kimataifa.
"Nipende kuwapa moyo wanariadha wengine wafanye mazoezi kwa kujituma na kuwa na nidhamu katika michezo ili kuiletea taifa sifa kubwa kama alivyofanya Simbu," amesema Kimaro.
Meja Didas Msholwa ambaye ni Kaimu Kamanda Regimeti 977 anapofanya kazi Alphonce Simbu, amesema ushindi huo ni kwa nchi ya Tanzania na kuongeza kuwa utii wake na kukubali kupokea maelekezo kutoka kwa viongozi ndio siri ya mafanikio yake.

"Pongezi kwa Mkuu wetu wa Majeshi, Jenerali Jacob John Mkunda kwa sababu yeye ndiye anatoa nafasi kuhusu vijana hawa na hawapangiwi majukumu yoyote zaidi ya kufanya mazoezi," amesema Msholwa.
Meneja wa timu ya riadha ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Kapteni Christopher Masanga amewataka wanariadha wengine kuiga kile ambacho amekifanya Simbu ili nao waweze kuitangaza nchi.