AKILI ZA KIJIWENI: Kagera Sugar kilichobaki ni miujiza tu

Muktasari:
- Hawakuwa timu iliyoweka dhamira ya dhati ya kubaki licha ya kufanya usajili wa wachezaji wengi dirisha dogo la usajili lililoanza Disemba 16 mwaka jana na kumalizika Januari 15, mwaka huu.
ILIKUWA suala la wazi wazee wa makarasha, KenGold wasingebakia Ligi Kuu Bara kwa vile walionyesha dalili nyingi za kurudi Championship.
Hawakuwa timu iliyoweka dhamira ya dhati ya kubaki licha ya kufanya usajili wa wachezaji wengi dirisha dogo la usajili lililoanza Disemba 16 mwaka jana na kumalizika Januari 15, mwaka huu.
Ingekuwa siriazi, ingepambana kuhakikisha wachezaji wake wa kigeni wanapata vibali vya kuwawezesha kutumika Ligi Kuu Bara, pia isingesajili mchezaji ambaye alikuwa majeruhi na ikifahamu fika asingetumika katika michezo mingi.
Baada ya juzi kushuka walipochapwa mabao 2-1 na Coastal Union pale Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, sasa hamu imebakia ni kuona timu gani ambayo itawafuata huko walikoenda Championship.
Kwa hali ilivyo Kagera Sugar ina mlima mrefu sana wa kupanda ili ibaki kwenye ligi na kwa sasa wanategemea zaidi kudra za Mungu maana katika mpira ukishafika hatua matokeo ya mechi zako pekee hayakubebi basi upo katika mashaka.
Sasa ndicho kinachoikuta Kagera Sugar maana hata ikipata ushindi katika mechi zake tatu zilizobakia bado usalama wake utategemea timu nyingine zivurunde na kama hazijafanya vibaya maana yake wanazama.
Ukiangalia mechi ambazo Kagera Sugar imebaki nazo ni dume hasa na sio za kupata ushindi au pointi kirahisi kutokana na aina ya timu ambazo itacheza nazo na mahitaji ambayo zinazo kwa sasa.
Ina Mashujaa ambayo haina uhakika wa kubakia, baada ya hapo inaifuata Namungo FC ambayo nayo haina uhakika wa kunusurika na mechi ya mwisho itapiga na mnyama Simba ambayo inasaka ubingwa lakini pia ina kisasi binafsi na Kagera Sugar.
Nadhani mnakumbuka Kagera Sugar ilivyowahi kuinyima ubingwa Simba kwa sakata la Mohamed Fakhi mnyama akakosa pointi mezani. Sidhani kama Simba wamesahau lile.