Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga yaweka rekodi nyingine

YANGA Pict

Muktasari:

  • Yanga imepangwa kuvaana na KVZ kesho Jumamosi katika mchezo wa robo fainali ya michuano hiyo iliyorejeshwa msimu uliopita ambapo watani wao, Simba walibeba taji kwa kuifunga Azam, japo safari hii imeshindwa kwenda kulitetea kutokana na kubanwa na ratiba ya mechi za kimataifa.

KIKOSI cha Yanga kinatarajiwa kuondoka jijini Dar es Salaam leo Ijumaa kwenda visiwani Zanzibar kwa ajili ya ushiriki wa michuano ya Kombe la Muungano 2025 iliyoanza jana, huku ikiwa imeandika rekodi nyingine ya kibabe katika mechi 24 ilizocheza tangu ilipopoteza katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Yanga imepangwa kuvaana na KVZ kesho Jumamosi katika mchezo wa robo fainali ya michuano hiyo iliyorejeshwa msimu uliopita ambapo watani wao, Simba walibeba taji kwa kuifunga Azam, japo safari hii imeshindwa kwenda kulitetea kutokana na kubanwa na ratiba ya mechi za kimataifa.

Lakini, ikiwa njiani kwenda Pemba kunakofanyikia michuano huyo, Yanga imeandika rekodi nyingine tamu baada ya kucheza mechi 23 mfululizo bila kupoteza, zikiwamo 15 za Ligi Kuu Bara, nne ya Kombe la Shirikisho (FA) na nyingine nne za Ligi ya Mabingwa Afrika ilikotolewa katika hatua ya makundi.

Wababe hao wa soka nchini, waling’olewa wakiwa katika Kundi A baada ya kushika nafasi ya tatu, wakitibuliwa na MC Alger ya Algeria iliyowalazimisha suluhu nyumbani kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na kuwafanya imalize wakiwa na pointi nane, moja pungufu na waliyovuna wapinzani wao hao.

Hata hivyo, rekodi zinaonyesha tangu ilipofungwa na MC Alger katika mchezo wa mkondo wa kwanza, Yanga haijapoteza mchezo wowote baada ya hapo kitu ambacho hata watani wao Simba hawajafikia, licha ya kuendelea katika michuano ya kimataifa wakicheza nusu fainali kwa sasa. Simba ilitibuliwa rekodi kwa kufungwa mabao 2-0 na Al Masry katika mechi ya mkondo wa kwanza ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kabla ya kuing’oa kwa mikwaju ya penalti 4-1 baada ya kuilaza 2-0 ziliporudiana Dar.

Ipo hivi. Rekodi zinaonyesha tangu ilipochapwa 2-0 ugenini jijini Algiers, Algeria Desemba 7, mwaka jana katika mechi ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga imekuwa haishikiki kwani hadi sasa haijapoteza mchezo wowote wa kimashindano. Kabla ya mechi hiyo, Yanga ilianza msimu kwa kucheza mechi nane mfululizo za Ligi Kuu na nne za raundi za awali za Ligi ya Mabingwa kwa kushinda zote na kutinga makundi ambapo ilianza kwa kufungwa mechi mbili mfululizo dhidi ya Al Hilal na Mc Alger, huku katika Ligi ilitibuliwa na Azam iliyowafunga bao 1-0 kisha kulala 3-1 mbele ya Tabora United.

Ndipo baada hizo nne ilizopoteza mfululizo, Yanga ikajipanga na kucheza michezo 23 ya mashindano yote bila ya kupoteza na kati ya hiyo imeshinda 20 na kutoka sare tatu, ambapo safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho imefunga mabao 75 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 10.

Katika michezo hiyo 15 ni ya Ligi Kuu, ambapo imeshinda 14 na kutoka sare moja dhidi ya JKT Tanzania Februari 10, 2025, huku safu ya ushambuliaji ikifunga mabao 52 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara sita.

Mingine minne ni ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi, ikianza na sare ya bao 1-1 dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo kisha marudiano ikashinda 3-1, jijini Dar es Salaam, ikaifunga Al Hilal bao 1-0 na suluhu mbele ya MC Alger.

Katika michezo hiyo, safu ya ushambuliaji ya Yanga imefunga mabao matano huku ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili pekee.

Michezo minne ni ya Kombe la Shirikisho (FA), ikianzia hatua ya 64 Bora kwa kuichapa Copco ya Mwanza mabao 5-0, kisha 32 Bora ikaichapa Coastal Union 3-1 na kutinga 16 Bora ilipoifunga Songea United 2-0 na kufuzu robo fainali.

Katika robo fainali, Yanga ikakutana na ‘Chama la Wana’ Stand United ikaichapa mabao 8-1 na kutinga nusu fainali itakayoicheza Mei 16 dhidi ya JKT TZ na kuifanya ifunge mabao 18 ya michuano hiyo, huku ikifungwa mawili na kufanya kiujumla imefunge 75 na kufungwa 10 kati ya michezo hiyo 23.

Ushindi wa mabao 4-0, ilioupata Yanga katika Ligi Kuu Aprili 21, 2025 dhidi ya Fountain Gate, ni wa nane mfululizo japo ni wa 15 kwa timu hiyo bila ya kupoteza tangu mara ya mwisho ilipochapwa 3-1, dhidi ya Tabora United, Novemba 7, 2024.

Rekodi ya msimu huu ya kucheza michezo 15 ya Ligi Kuu bila ya kupoteza, inaikaribia ile ya Simba ya mechi 16 ambayo ilicheza tangu ilipochapwa na Yanga bao 1-0, Oktoba 19, 2024 haijapoteza tena hadi leo.

Katika michezo hizo 16 za Simba, imeshinda 14 kama za Yanga na kutoka sare mbili dhidi ya Fountain Gate na Azam FC, lakini kwa kimataifa iliyumba na kuzidiwa ujanja ya watani wao.

Simba ilipoteza dhidi ya CS Constantine ya Algeria katika mechi za makundi ya Kombe la Shirikisho, kisha ikaja kupoteza tena kwa Al Masry katika robo fainali na kutibuliwa rekodi ya kula sahani moja na Yanga.

Kocha wa Yanga, Miloud Hamdi aliyeanza kibarua kwa kulazimishwa suluhu na JKT na baada ya hapo kutopoteza mechi yoyote kati ya 15 alizoiongoza timu hiyo, alisema: “Unapokuwa na wachezaji bora inasaidia kufikia malengo ila ni ngumu kumridhisha kila mmoja wao.”