Utata sakata la Noble Fountain Gate

Muktasari:
- Mwanaspoti limefanya juhudi za kumtafuta Noble, lakini hajapatikana na wala simu yake ya mkononi haikupatikana na hata alipotumiwa ujumbe wa maandishi wa kawaida na ule wa WhatsApp hauonekani kusomwa na hata simu yake haionyeshi kuwa hewani.
WAKATI uongozi wa Fountain Gate ukipanga kukutana na kipa wa timu hiyo, John Noble ili ajibu tuhuma za kucheza chini ya kiwango, mwenyewe anadaiwa kutopatikana huku ikidaiwa kwamba kaondoka nchini kimyakimya kurudi kwao Nigeria.
Mwanaspoti limefanya juhudi za kumtafuta Noble, lakini hajapatikana na wala simu yake ya mkononi haikupatikana na hata alipotumiwa ujumbe wa maandishi wa kawaida na ule wa WhatsApp hauonekani kusomwa na hata simu yake haionyeshi kuwa hewani.
Sakata la kipa huyo lilianza baada ya mchezo dhidi ya Yanga uliochezwa Aprili 21, 2025 kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Babati mkoani Manyara, ambapo aliruhusu mabao mawili kipindi cha kwanza katika kipigo cha mabao 4-0 ilichopata timu hiyo.
Kipa huyo alifungwa mabao hayo dakika 38 na 43 yaliyowashangaza mashabiki na baadaye kuibua mjadala, lakini kwa upande wake alifanyiwa mabadiliko mapema akaingia Ibrahim Parapanda ambaye naye aliruhusu mawili.
Taarifa ilizonazo Mwanspoti ni kuwa, kipa huyo anadaiwa hana mawasiliano pia na wachezaji wenzake wala viongozi, huku uongozi ukiwa umepanga kesho akutane na na kamati ya maadili kwa mahojiano ya kina.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari wa Fountain Gate, Issa Liponda alisema uongozi haufahamu lolote kuhusu kipa huyo wala mahali alipo. “Tumeziona hizo taarifa mitandaoni (zinazodai ameondoka nchini), kama ambavyo mnaziona na nyie. Klabu tunazifuatilia kwa kina kujua kama ni kweli ameondoka. Tulimuita tukitaka akakutane na kamati ya maadili, sasa kama ameondoka uongozi utakuja na taarifa baadaye, lakini hilo ni kosa lingine kama kweli atakuwa amelifanya,” alisema Liponda.
“Ni kosa yeye kuondoka, tunamtumia barua ya kuja ofisini Jumatatu asipokuja tutapambana naye.”