10 yanawatofautisha Alikiba, Diamond katika Kariakoo Dabi

Muktasari:
Wasanii hawa wa Bongofleva kila mmoja ana upande wake katika dabi hiyo, Alikiba akiwa Simba huku Diamond akiwa Yanga, na hii inaonyesha jinsi utofauti wao ulivyo katika muziki wao hadi katika dabi ya Kariakoo kama ifuatavyo.
Kwa miaka takribani 10, Alikiba na Diamond Platnumz wamekuwa wakishindanishwa na mashabiki kutokana wanafanya vizuri lakini kuna tofauti kati yao kama ilivyo kwa Yanga SC na Simba SC zinazokutana kesho katika dabi ya Kariakoo.
Wasanii hawa wa Bongofleva kila mmoja ana upande wake katika dabi hiyo, Alikiba akiwa Simba huku Diamond akiwa Yanga, na hii inaonyesha jinsi utofauti wao ulivyo katika muziki wao hadi katika dabi ya Kariakoo kama ifuatavyo.
1. Tuzo kama zote
Katika Tuzo za Muziki Tanzania (TMA), Diamond ameshinda mara 22 akiwa ndiye msanii aliyebeba mara nyingi zaidi tuzo hizo zilizoanza mwaka 1999, anafuatiwa na Alikiba ambaye ameshinda tuzo 18 na mara ya mwisho alifanya hivyo kupitia wimbo wake, Mahaba (2023).
Jinsi Diamond na Alikiba wametawala TMA, ndivyo hivyo kwa wababe hao wa Kariakoo katika ubingwa wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara, Simba ikibeba mara 22 huku Yanga ikichukua mara 30 na ndio mabingwa wa kihistoria na bingwa mtetezi.
2. Huko Basata hawacheki
Hadi sasa Alikiba hajawahi kufungiwa wimbo wake na Baraza la Sanaa Taifa (Basata) kutokana na kukiuka maadili, wakati Diamond kafungiwa nyimbo mbili, Hallelujah (2017) na Waka (2017), pia video ya wimbo wake, Mtasubiri (2022) imefungiwa.
Tukirejea katika dabi, tayari Yanga imepoteza mechi mbili msimu huu, ikipoteza mbele ya Azam FC na Tabora United, wakati Simba imepoteza mchezo mmoja pekee tena dhidi ya Yanga katika mzunguko wa kwanza wa Ligi kwa kukubali kichapo cha goli 1-0.
3. Albamu, EP ngoma droo
Diamond ametoa albamu tatu, Kamwambie (2010), Lala Salama (2012), A Boy From Tandale (2018), na EP moja, First of All (2022), hivyo hivyo Alikiba albamu tatu, Cinderella (2007), Ali K 4Real (2009), Only One King (2021) na EP moja, Starter (2024).
Hata hivyo, wanaenda kuitazama dabi wakati Yanga akiwa bingwa kwa misimu mitatu mfululizo na kushinda michezo yote ya Ligi dhidi ya Simba msimu uliopita kwa jumla ya magoli 7-2, na sasa wanasaka taji la nne mfululizo kama walivyofanya Simba hapo awali.
4. Ubabe kwa Afrika
Diamond ni mwanamuziki wa pili aliyetazamwa zaidi YouTube barani Afrika nyuma ya Burna Boy kutokea Nigeria ila Alikiba hayupo hata 10 bora ya waliotazamwa sana katika mtandao huo ulioanzishwa Februari 14, 2005 huko Marekani.
Tukija kwa vigogo wa Kariakoo, kwa mujibu wa chati ya CAF, Simba inashikilia nafasi ya sita kwa ubora Afrika wakati Yanga ikiwa ya 10 kwa bora ingawa msimu huu ilikuwa na nafasi ya kupanda juu zaidi ila isivyo bahati wakashindwa kufuzu robo fainali ya CAFCL.
5. Rekodi za kutisha
Katika tuzo TMA, Diamond amewahi kubeba saba kwa usiku mmoja, hiyo ilikuwa msimu wa 2014, Alikiba akajirabu kuivunja rekodi hiyo 2015 ila akaishia kubeba tano, na hata alipojaribu tena 2021 akaishia kubabeba tano, hivyo rekodi ya Mondi ipo pale pale.
Na katika dabi, mzunguko wa kwanza msimu uliopita wa 2023/24, Yanga ilishinda 5-1, licha ya kipigo hicho kuwa kikubwa lakini walishindwa kuifuta rekodi ya kuchapwa goli 5-0 na Simba msimu wa 2011/12, ikiwa pia ni baada ya kulazwa 6-0 mwaka 1977.
6. Ubabe Afrika Mashariki
Diamond ndiye msanii pekee Tanzania na Afrika Mashariki aliyesikilizwa (streams) mara nyingi zaidi katika jukwaa la Boomplay Music akiwa na streams zaidi ya milioni 498, huku Alikiba akishika nafasi ya saba kwa Tanzania akiwa na streams milioni 207.
Hiyo ni sawa na Simba ambayo ndio timu pekee Tanzania iliyoshiriki michuano yote mikubwa ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), tayari Simba imeshiriki CAFCL, CAFCC na African Football League (AFL), michuano ambayo Yanga bado haijashiriki.
7. Lebo zao zinatofautiana
Lebo ya Diamond, WCB Wasafi ina rekodi ya kusaini wasanii nane hadi sasa huku wa kike wakiwa wawili ambao ni Queen Darlee na Zuchu, wakati ile ya Alikiba, Kings Music ikisaini wasanii sita kwa ujumla na hakuna hata mmoja wa kike.
Tunakwenda kuitazama dabi wakati washambuliaji wa Yanga, Mzize na Dube wakiwa wameshafunga magoli 10 kila mmoja katika ligi sawa na kiungo wa Simba, Ahoua ila magoli yake mengi yanatokana na penalti tofauti na Mzize na Dube ambao hawana penalti.
8. Mzuka hadi DR Congo
Diamond amerekodi na wasanii wakubwa wa DR Congo kama Koffi Olomide (Waah!), Fally Ipuma (Inama) na Innoss’B (Yope Remix), kolabo ambazo zimempa namba kubwa, wakati Alikiba amerekodi na Maud Elka (Songi Songi Remix).
Katika dabi timu zote zina wachezaji wazuri kutokea DR Congo, Yanga wakiwa na Maxi Nzengeli na Chadrack Boka, upande wa Simba yupo Fabrice Ngoma na Elie Mpanzu ambaye alisajiliwa katika dirisha dogo msimu huu na tayari uwezo wake umeonekana.
9. Namba kubwa Afrika
Hadi sasa Diamond ndiye mwanamuziki pekee Afrika mwenye wafuasi wengi YouTube akiwa nao zaidi ya milioni 9.8, wakati Alikiba akiwa hayupo hata 10 bora Afrika na kwa Tanzania akiwa nje ya tano bora akiwa na wafuasi wake milioni 2.0.
Na ndivyo hivyo tunaenda kuitazama dabi wakati Simba ikiwa timu pekee Tanzania kati ya nne iliyosalia katika michuano ya CAF msimu hii ikiwa robo fainali ya shirikisho (CAFCC), huku Coast Union, Azam FC na Yanga SC zikiwa tayari zimetupwa nje.
10. Hamisa Mobetto naye ndani!
Mwanamitindo Hamisa Mobetto na Miss XXL After School Bash 2010, hadi sasa ametokea katika video za nyimbo mbili za Diamond, Mawazo (2012) na Salome (2016), huku kwa Alikiba akitokea katika video moja, Dodo (2020) iliyofanyika Zanzibar.
Ni Hamisa ambaye hii inakuwa dabi yake ya kwanza tangu ameolewa na mchezaji wa Yanga, Stephane Aziz Ki ambaye alijiunga na timu huyo hapo Julai 2022 akitokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast huku msimu uliopita akiwa Mchezaji Bora (MVP) Ligi Kuu Bara.