Prime
Kukimbiana Simba, Yanga na utamu wake

Muktasari:
- Kwa mujibu wa maelezo yao, Simba kama mgeni wa mchezo huo walipaswa kufanya mazoezi ya mwisho kwa kuzingatia muda wa mchezo kwenye uwanja utakaofanyika mechi, lakini wakazuiwa na meneja wa uwanja akisema hakuwa na maelekezo ya matumizi ya uwanja kutoka kwa kamisaa wa mchezo.
KLABU ya Simba imetoa taarifa rasmi kwamba haitashiriki kwenye mchezo wa watani wa jadi uliopangwa kufanyika leo, Machi 8, 2025. Hii ni kwa sababu walishindwa kufanya mazoezi ya mwisho kuelekea mchezo huo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara.
Kwa mujibu wa maelezo yao, Simba kama mgeni wa mchezo huo walipaswa kufanya mazoezi ya mwisho kwa kuzingatia muda wa mchezo kwenye uwanja utakaofanyika mechi, lakini wakazuiwa na meneja wa uwanja akisema hakuwa na maelekezo ya matumizi ya uwanja kutoka kwa kamisaa wa mchezo.
Na hata kamisaa alipofika, wakatokea watu wengine waliotajwa kama mabaunsa wa Yanga wakavamia msafara wao na kuwafanyia vurugu. Kadhia hiyo, kwa mujibu wa taarifa rasmi ya Simba ilidumu kwa saa mbili na katika kuepusha shari wakaamua kuondoka eneo la tukio.
Kama hayo kweli yalitokea, basi Simba wana haki ya kutoshiriki mchezo huo kwa sababu kisayansi wachezaji hawapaswi kucheza mechi bila mazoezi angalau saa 24 kabla. Simba watakuwa hawajafanya mazoezi kwa zaidi ya saa 50 kabla ya mchezo.
Lakini, hata hivyo, hii siyo mara ya kwanza kwa watani hawa wa jadi kukimbiana. Katika historia ya ligi ya Tanzania tangu kuanzishwa kwake 1965, huo utakuwa mchezo wa sita wa ligi kushindwa kufanyika kutokana timu moja kutofika uwanjani kwa sababu moja au nyingine.
Lakini kwa ujumla ni mchezo wa saba ukichanganya na mashindano mengine.

1. Simba iliikimbia Yanga 1969.
Ilikuwa Machi 3, 1969, wakati huo ikiitwa Sunderland, Simba ilikataa kucheza na Yanga kwa sababu walikataliwa rufaa yao dhidi ya African Sports ya Tanga. Sports na Sunderland walitoka sare ya bao 1-1 katika mchezo wa ligi, lakini Sunderlabd walilalamika kwamba Sports walimchezesha kipa ambaye hakusajiliwa.
Hata hivyo, Sports wakasema waliruhusiwa na FAT (Chama cha Soka Tanzania wakati huo) kwa barua kufuatia maombi yao kwa sababu walikuwa na makipa wawili tu, mmoja alikuwa anaumwa macho na mwingine alikuwa safarini.
Kwa hiyo mechi ilipofika wakawa hawana kipa - wakaomba kwa FAT wamtumie kipa mwingine, FAT ikakubali. Lakini baada ya mechi kuisha kwa sare, Sunderland wakakata rufaa - ikakataliwa, ndipo nao wakagomea mechi na Yanga. Yanga wakapewa alama za mezani na Sunderland kupigwa faini ya Sh500 ambayo hata hivyo walirudishiwa.

2. Yanga waliikimbia Simba 1992.
Ilikuwa Septemba 26, 1992 kwenye mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Daraja la Kwanza Bara. Yanga walikataa kuingia uwanjani kucheza na Simba kwa sababu tayari walikuwa wameshachukua ubingwa. Wakasema hiyo mechi haikuwa na maana kwao kwa sababu ubingwa tayari wanao.
Simba wakapewa alama za mezani na Yanga kupigwa faini ya Sh250,000 ambazo zililipwa na mfadhili wao mpya, Murtaza Dewji aliyejiunga nao akitokea Pan Africa.

3. Simba waliikimbia Yanga 1996
Ilikuwa Februari 26 ambapo Simba waligoma kucheza na Yanga kwa sababu walikuwa wanataka kujiandaa na mechi ya kimataifa, Kombe la Washindi Afrika dhidi ya Chapungu Rangers ya Zambia. Simba waliandika barua FAT kuomba ibadilishe tarehe ya mechi hiyo, lakini FAT ikakataa. Simba wakagoma kucheza Yanga wakapewa alama za mezani.
Hata hivyo, Chapungu wenyewe hawakuja kucheza hiyo mechi, Simba wakapewa ushindi wa mezani na kuvuka hadi hatua iliyofuata.

4. Yanga waliikimbia Simba 2002
Yanga ilimsajili Said Maulid kutoka Simba 2002. Julai mwaka huo, Wizara ya Mambo ya Ndani ikatangaza kwamba mchezaji huyo siyo raia wa Tanzania. Tangazo hilo lilitoka wakati pambano la Yanga na Simba likikaribia.
Yanga wakagomea huo mchezo hadi Said Maulid aruhusiwe kucheza. Serikali ikasema mchezaji huyo ni Mkongomani na akitaka kuendelea kucheza Tanzania basi awe na hati ya kusafiria ya DR Congo. Said Maulid akafungua kesi mahakamani na akashinda, akarudishiwa uraia wake. FAT iliahirisha hiyo mechi hadi Said Maulid alipopata uraia mahakamani.

5. Yanga waliikimbia Simba Kombe la Kagame 2008
Yanga na Simba zilitakiwa kukutana kuwania mshindi wa tatu wa Kombe la Kagame baada ya wote kutolewa nusu fainali. Lakini Yanga hawakuingia uwanjani bila sababu zilizoeleweka. Baadaye mwenyekiti wao, Imani Madega, akasema walikubaliana na Simba, TFF na Cecafa kwamba wapewe Sh50 milioni kabla ya mchezo huo. Lakini, hadi siku siku ya mchezo pesa hizo hawakupewa, ndiyo wakagoma.
Akaongeza kwamba walikubaliana na Simba kugoma pamoja, lakini Simba waliwasaliti na kwenda uwanjani. Cecafa wakaifungia Yanga kushiriki mashindano hayo kwa miaka mitatu. Hata hivyo baada ya miaka miwili wakasamehewa.
TFF pia ikaifungia Yanga kushiriki mashindano yoyote ya kimataifa kwa miaka mitatu. Yakatoka mashinikizo kutoka serikalini kwenda TFF huku wabunge wakiwa na mjadala mkali bungeni kuhusu hilo sakata. Ikaundwa kamati ya kiandamizi kuhakikisha kinatafutwa kipengele cha kuichomoa Yanga kwenye adhabu na kweli ikachomolewa.

6. Yanga waliikimbia Simba 2021
Mei 8, 2021 Yanga walisusia mechi dhidi ya watani wao kutokana na kubadilishwa kwa muda wa mchezo. Matatizo ya mawasiliano kati ya mamlaka za kiserikali, za soka na wahusika wakuu yaani klabu yakavuruga mambo na kuleta mtafaruku mkubwa.
Ni kwamba siku hiyo ilipangwa mgeni rasmi awe Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ndiyo alikuwa ametoka kuingia madarakani miezi michache iliyopita. Lakini siku hiyo hiyo Rais alikuwa akihudhuria hafla ya uzinduzi wa kitabu cha Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi (sasa marehemu).
Kwa hiyo mechi hiyo ambayo ilipangwa kufanyika saa 11 jioni ikasogezwa mbele hadi saa moja usiku ili mheshimiwa aweze kuwahi. Yanga wakagoma na kususia mechi.

7. Simba wameikimbia Yanga 2025
Leo Machi 8, 2025 Yanga walipaswa kuwa wenyeji wa Simba, lakini kama mlivyosikia, Simba wametangaza kutoka nduki.
HITIMISHO
Mechi baina ya watani hao zina siasa nyingi, kiasi kwamba jambo dogo tu basi linaweza kuharibu kila kitu. Haya mambo ya mmoja kumkimbia mwenzake yameshatokea mara kadhaa huko nyuma kiasi cha mechi kutofanyika kabisa, sababu ni vitu vidogo vidogo tu ambavyo vinaweza kuepukwa.
Tatizo kubwa ni kwamba hakuna anayependa kukutana na mwenzake kwa sababu wanaogopana. Kwa hiyo sababu yoyote ikitokea, mmoja anaitumia na kuharibu kila kitu. NI DALILI YA UOGA!
Makala hii tuliichapisha mara ya kwanza Mei 2021 baada ya kushindwa kufanyika mechi kama hii, Mei 8. Tumeirudia kwa sababu ya umuhimu wake wakati huu.