Prime
Mafanikio Simba CAFCC yaivuruga Bodi ya Ligi, TFF

Muktasari:
- Simba ilitoka suluhu na Stellenbosch katika mechi hiyo ya juzi, lakini ushindi wa bao 1-0 nyumbani ikiwa visiwani Zanzibar, umewavusha kwenda fainali na sasa itavaana na RS Berkane y Morocco, lakini ikiwa na mechi nane mkononi, zikiwamo tano za viporo vya Ligi Kuu zilizopangwa kupigwa ndani ya Mei pamoja na kiporo dhidi ya Yanga katika Dabi ya Kariakoo iliyoahirishwa Machi 8 mwaka huu.
SIMBA imerejea nchini jana kutoka Afrika Kusini ilikoenda kurudiana na Stellenbosch na kufuzu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, lakini kitendo cha Wekundu hao kutinga hatua hiyo kimeleta majanga baada ya mabosi wa Bodi ya Ligi kujifungia ili kuipangua tena ratiba.
Simba ilitoka suluhu na Stellenbosch katika mechi hiyo ya juzi, lakini ushindi wa bao 1-0 nyumbani ikiwa Zanzibar, umeivusha kwenda fainali na sasa itavaana na RS Berkane ya Morocco, lakini ikiwa na mechi nane mkononi zikiwamo tano za viporo vya Ligi Kuu zilizopangwa kupigwa ndani ya Mei pamoja na dhidi ya Yanga katika Dabi ya Kariakoo iliyoahirishwa Machi 8, mwaka huu.
Ratiba ya awali ilikuwa inaonyesha Simba itacheza kuanzia Mei 2-11 dhidi ya Mashujaa, JKT Tanzania, Pamba Jiji na KMC kisha kurudi tena uwanjani sambamba na timu nyingine 15 za Ligi hiyo ili kumalizia raundi tatu za mwisho za kufungia msimu uliopangwa kuisha Mei 25.
Kuwepo kwa mechi mbili za fainali dhidi ya RS Berkane kati ya Mei 17 na 25 umetibua mechi hizo za viporo za Simba sambamba na ile ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Singida Black Stars ya Mei 18, jambo hilo limewalazimisha watu wa Bodi ya Ligi kutaka kupangua ratiba.
Simba itaanza kampeni za kusaka taji hilo kubwa Afrika kwa kucheza fainali ya kwanza ugenini Mei 17 ikiwa Morocco, kisha kurudi jijini Dar es Salaam kwa mechi ya marudiano itakayopigwa Mei 25, ambayo ilikuwa ndio tarehe ya mwisho mwa msimu.
Kwa mujibu wa ratiba ya Ligi Kuu, inaonyesha Simba inaanza Mei 2 kwa kucheza na Mashujaa nyumbani kabla ya kuwafuata maafande wa JKT Tanzania Mei 5, kisha Pamba Jiji Mei 8, huku ikiifuata pia KMC Mei 11 kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mjini Tabora.
Baada ya hapo, Simba ingekuwa na mechi na Singida Black Stars Mei 14, kisha kusafiri Mbeya kuifuata KenGold iliyoshuka daraja Mei 21 na kuikaribisha Kagera Sugar Mei 25, kabla ya kupambana na Yanga ambayo tarehe mpya bado haijapangwa pia.
Mbali na ratiba ya Ligi Kuu Bara, ila mechi nyingine ambayo itaathirika kutokana na fainali hiyo ni ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA), dhidi ya Singida Black Stars iliyopangwa kuchezwa Mei 18, mjini Babati mkoani Manyara.
Kitendo cha ratiba hiyo kubana, kikaifanya Bodi ya Ligi Kuu (TPLB), kupitia kwa Ofisa Habari, Karim Boimanda kuweka wazi watu wa idara watakaa chini kwa ajili ya kupanga vizuri ratiba, ili kutoa pia nafasi kwa wawakilishi hao pekee wa nchi.
“Idara yetu ya Ligi Kuu itakaa na kupanga ratiba upya, lengo ni kutoa nafasi kwa Simba kwa ajili ya maandalizi ya mechi hizo mbili muhimu za fainali ya ugenini na nyumbani, pia kuzingatia inaisha kwa wakati utakaopangwa,” alisema Boimanda.
Mapema Shirikisho la Soka Afrika (CAF) liliainisha kuwapo kwa fainali za Kombe la CHAN 2025 Agosti mwaka huu, kalenda ya ngazi ya klabu zifikie tamati Juni Mosi mara baada ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini kwa hali ilivyo ni wazi msimu wa mashindano Bara huenda usimalizike Mei 31.
Hata hivyo, Boimanda alipoulizwa itakuwaje kwa mlengo huo wa agizo la CAF, alisema wanadhani ratiba za ligi nyingi zitabadilishwa kwani ni ngumu kumalizika kabla ya Juni Mosi hususani Bara, ila kila kitu kitakuwa wazi baada ya Idara ya Ligi Kuu itakapotoka na ratiba mpya.