Straika Fountain atamani bao moja tu!

Muktasari:
- Mshambuliaji huyo chipukizi, amesema kwa vile wameshindwa kufunga bao katika mechi 27 zilizochezwa na timu yake, kama mchezaji asingependa kutoka kapa ndiyo maana anaomba kwa dakika 270 zilizobaki kufunga msimu aambulie japo bao moja limfariji.
MAISHA hayana usawa, kwani wakati washambuliaji wa timu nyingine za Ligi Kuu Bara hususan waliopo Simba, Yanga, Azam na Singida BS wakipigia hesabu kiatu cha mfungaji bora wa msimu, hali ni tofauti kwa Hashim Omary wa Fountain Gate anayetamani angalau afunge bao moja tu.
Mshambuliaji huyo chipukizi, amesema kwa vile wameshindwa kufunga bao katika mechi 27 zilizochezwa na timu yake, kama mchezaji asingependa kutoka kapa ndiyo maana anaomba kwa dakika 270 zilizobaki kufunga msimu aambulie japo bao moja limfariji.
Hali ni tofauti kwani kwa nyota wa Yanga, Clement Mzize mwenye mabao 13 na Prince Dube (12) sambamba na Jean Charles Ahoua (12) wa Simba wanachuana kileleni katika mbio za ufungaji mabao kutaka kumpokea Stephano Aziz KI.
Hata hivyo, kwa Omary mambo yamekuwa tofauti na akisungumza na Mwanaspoti alisema msimu uliyopita alimaliza na bao moja alilofunga dhidi ya Kagera Sugar, kitu ambacho anatamani kitokee msimu huu na hadi sasa asisti moja.
“Nilipandishwa msimu uliyopita, hivyo sikucheza mechi nyingi kama ilivyo msimu huu, naendelea kupambana kufanya mazoezi nikiamini kuna siku nitakuwa tegemeo kikosi cha kwanza,” alisema Omary na kuongeza;
“Kama nitapata bahati ya kucheza katika mechi zilizosalia ambazo ni dhidi ya JKT Tanzania, Coastal Union na Azam FC natamani nifunge bao moja msimu huu usipite bure kwa nafasi ninayocheza ya ushambuliaji, maana hata mabeki wapo waliyofunga mabao.”
Mabeki waliyofunga mabao mengi katika Ligi Kuu kwa sasa ni Lusajo Mwaikenda wa Azam mwenye mabao matano, akifuatiwa na Ibrahim Hamad ‘Bacca’ wa Yanga (manne), Shomari Kapombe (Simba), Paschal Msindo (Azam) na Hernest Malonga wa (Singida BS) kila mmoja akifunga mabao matatu.
Chipukizi huyo alikuwa kivutio katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Simba iliyochezwa Februari 6, Uwanja wa Tanzanite, Kwaraa, Babati Manyara baada ya kipa John Noble kupewa kadi nyekundu na idadi ya wachezaji wa kubadilishwa kukamilika kwa timu hiyo ya FG na kumlazimisha mshambuliaji huyo kukaa langoni na aliokoa mchomo mkali wa Elie Mpanzu dakika za jioni na mechi kuisha kwa sare ya 1-1.