Ngorongoro Heroes yaanza msako wa Afcon U20

Muktasari:
- Fainali za AFCON U20 zinaendelea kufanyika Misri ikishirikisha timu za nchi 13 zilizopangwa katika makundi matatu, na zimeanza juzi Aprili 27 na zitafikia tamati Mei 18, ambapo timu nne zitakazotinga nusu fainali zitakata tiketi ya Fainali za Kombe la Dunia U20 zitakazofanyika huko Chile.
TIMU ya taifa ya Tanzania ya vijana wa chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes kesho Jumatano itaanza kampeni za kusaka ubingwa kucheza fainali za Kombe ka Mataifa ya Afrika (AFCON) dhidi ya Afrika Kusini ikiwa Kundi A.
Fainali za AFCON U20 zinaendelea kufanyika Misri ikishirikisha timu za nchi 13 zilizopangwa katika makundi matatu, na zimeanza juzi Aprili 27 na zitafikia tamati Mei 18, ambapo timu nne zitakazotinga nusu fainali zitakata tiketi ya Fainali za Kombe la Dunia U20 zitakazofanyika huko Chile.
Mechi hiyo ya kwanza kwa Ngorongoro itapigwa kwenye Uwanja wa Suez Canal, Ismailia ukiwa wa kwanza kwenye kundi A ambalo pia wapo wenyeji wa mashindano hayo Misri. Timu nyingine za kundi hilo ni Zambia, Ngorongoro Heroes, Sierra Leone na Afrika Kusini.
Baada ya mechi dhidi ya Sauzi, itashuka uwanjani tena Mei 3 kwa kuvaana na Sierra Leone kabla ya Mei 6 kuumana na Zambia na kuja kumalizia ratiba ya makundi na wenyeji na kusikilizia kama itaenda robo fainali au la.
Akizungumza na Mwanaspoti, mshambuliaji wa kikosi hicho, Mourice Sichone alisema wanaamini watafanya vizuri kwenye mashindano hayo licha ya ugumu wa kundi lao.
“Tuna kikosi ambacho kinaweza kuamua matokeo, wachezaji kama Shekhan, Selemani Mwalimu, Zidane Sereri kilichobaki ni juhudi zetu binafsi na kocha ametupa mipango yote,” alisema Sichone na kuongeza:
“Mimi ninacheza Zambia na timu hiyo kwa asilimia kubwa wachezaji wake nawafahamu kwa sababu nimekutana nao sana licha ya ubora wao lakini nawafahamu wana udhaifu pia.”
Hii ni mara ya kwanza kwa Afrika Kusini kushiriki fainali hizo huku Ngorongoro Heroes ikishiriki kwa mara ya pili.
Ngorongoro Heroes ilishiriki mashindano hayo kwa mara ya kwanza katika fainali za 2021 ambapo iliishia katika hatua ya makundi zilipofanyika Mauritania.
Misri ndio timu tishio zaidi katika kundi hilo kwa vile inashika nafasi ya pili kwa kutwaa taji hilo mara nyingi ikifanya hivyo mara nne ambazo ni 1981, 1991, 2003 na 2013.
Misri imeshika nafasi ya pili mara moja na imewahi kumaliza katika nafasi ya tatu mara tatu.
Zambia ni timu nyingine iliyowahi kuonja mafanikio kwenye kundi A ambapo imetwaa ubingwa mara moja ambayo ni mwaka 2017 na imeshika nafasi ya nne mara tatu ambazo ni 1991, 1999 na 2007.
Mabingwa wa kihistoria wa fainali hizo Nigeria ambao wametwaa taji hilo mara saba, wamepangwa katika kundi B.
Wako timu za Tunisia, Kenya na Morocco.
Watetezi, Senegal wamepangwa Kundi C na timu za Jamhuri ya Afrika ya Kati, DR Congo na Ghana.