Yanga kutesti tena Kombe la Muungano

Muktasari:
- Nusu fainali hiyo ya pili baada ya ile iliyopigwa jana ikizikutanisha JKU na Azam FC, itapigwa kuanzia saa 1:15 usiku, huku kila moja ikipiga hesabu kulinasa taji linaloshikiliwa kwa sasa na Simba.
KIKOSI cha Yanga usiku wa leo kitarudi tena kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba kuvaana na Zimamoto katika mechi ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Muungano, ikilenga zaidi kuboresha rekodi ilizonazo kwa michuano hiyo iliyorejeshwa kuanzia mwaka jana baada ya kusimama tangu 2003.
Nusu fainali hiyo ya pili baada ya ile iliyopigwa jana ikizikutanisha JKU na Azam FC, itapigwa kuanzia saa 1:15 usiku, huku kila moja ikipiga hesabu kulinasa taji linaloshikiliwa kwa sasa na Simba.
Zimamoto inayofundishwa na kocha Mohamed Ali inayoshika nafasi ya sita katika msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar ikiwa na pointi 36 baada ya mechi 22, inaingia kwenye mechi hiyo kibabe kufuatia kuichapa Coastal Union bao 1-0 hatua ya robo fainali, huku Yanga ikiifunga KVZ kwa mabao 2-0.
Kitendo cha Zimamoto kuifunga Coastal, inaamini moto wao huo wa kuzichapa timu za Bara utaendelezwa mbele ya Yanga inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa pointi 70 baada ya mechi 26.
Kwa upande wa Yanga, inalisaka taji hilo ili kuongeza idadi ya kulibeba mara nyingi zaidi baada ya hivi sasa kuwa sawa na Simba kila mmoja akilichukua mara sita, hivyo inasaka rekodi mpya.
Rekodi zinaonyesha tangu kuanzishwa kwa michuano hiyo mwaka 1982, Yanga imechukua miaka ya 1983, 1987, 1991, 1996, 1997, 2000, huku Simba ambayo ni bingwa mtetezi imechukua 1993, 1994, 1995, 2001, 2002, 2024.
Zimamoto inafahamu kwa kushinda dhidi ya Yanga, kwao itawaweka kwenye njia ya kwenda kuandika rekodi ya kushinda ubingwa huo kwani haijawahi kuubeba. Kwa Zanzibar timu zilizoshinda Kombe la Muungano ni Malindi (1989, 1992) na KMKM (1984).
Kocha Mohamed Ali anaamini mchezo unachezwa ndani ya uwanja hivyo hana hofu ya kukutana na Yanga ambayo kupitia kocha Miloud Hamdi, bado msisitizo wao ni kuona wanarudi Dar es Salaam na ubingwa wa michuano hiyo.
Mshindi wa mechi hiyo ya leo ataungana na aliyeshinda jana usiku kati ya JKU na Azam kwa ajili ya fainali itakayopigwa Mei Mosi.
Michuano hiyo iliyorejea mwaka jana baada ya kusimama kwa takribani miaka 22 kuanzia 2003 hadi 2024, Simba ikilinyakua taji la sita na kuifikia Yanga baada ya kuifunga Azam bao 1-0 katika fainali iliyopigwa Aprili 27, 2024 kupitia kiungo raia wa Senegal, Babacar Sarr, dakika ya 77.
Mshindi wa mechi hiyo ya leo ataungana na aliyeshinda jana usiku kati ya JKU na Azam kwa ajili ya fainali itakayopigwa Mei Mosi.