HADITHI: Zindiko (sehemu 12)

Muktasari:

  • Huu ni mwendelezo wa hadithi tamu na ya kusisimua ya Zindiko kutoka kwa mtunzi mahiri wa riwaya, SULTAN TAMBA. Twende naye.

MKONO wa Ras Kim ukaweka picha ya jengo mezani. Kazumba akaichukua na kuitazama.

Lilikuwa ni jengo kubwa zuri!

“Ni jengo zuri sana, liko mji gani hili, ila inaonekana kama kijijini – tena jipya. Vipi, linauzwa?”

“Ni jengo lililojengwa miaka 20 iliyopita! Hapo unaliona katika upya wake, lakini kwa sasa haliwezi kuwa hivyo. Nafikiri unanielewa. Kwa msisitizo tu ni kwamba picha ni ya miaka 20 iliyopita wakati lilipomalizika kujengwa.”

Kazumba akazumbaa katika mshangao.

“Ina maana huna picha mpya? Au?”

“Sijawahi kwenda kwa miaka yote hiyo. Kwa hiyo sijaliona tena. Baada ya kulijenga nikaliacha. Kwa hiyo sasa nataka kwenda, najua nitalikuta liko tofauti, labda rangi kubadilika, uchakavu au hata mazingira yake mengine.”

Kazumba akarudi kwenye hali yake ya kushangaa.

“Sijakuelewa bosi. Ina maana wewe huko zamani ulikuwa mkandarasi tu, ulitumwa kujenga ukalipwa ukaondoka. Na sasa wenyewe wanataka kuligeuza kuwa kiwanda cha mikate kama ulivyonambia wakakufuata tena... labda kwa sasa sio mkandarasi unataka utupe sisi hili dili, au?

Ras Kim akatangulia kukataa kwa kichwa.

“Hapana. Sijawahi kuwa mkandarasi wala mjenzi. Jengo hilo nililijenga mimi mwenyewe kwa fedha zangu. Niliwalipa mafundi wakafanya hiyo kazi kwa muda mfupi sana. Lakini sio mali yangu. Na wala sitaki liwe mali yangu. Ila inanilazimu.”

Kazumba akaendelea kushangaa.

“Na hivi ninavyokwambia, baada ya wiki chache hizi kupita, itakuwa sina jinsi zaidi ya kulimiliki. Na hilo litakuwa ni jambo la huzuni sana.”

Kazumba akamtazama katika hali ya kutoelewa.

“Kwa hiyo ulilijenga kwa fedha zako, ukawalipa mafundi, wakajenga na kumaliza! Lakini sio mali yako!”

Ras Kim akakubali kwa kichwa huku akiweka tabasamu la kwa mbali.

“Japo sijaelewa vizuri, lakini basi kama mpango wako ndio huo wa kukatabati na kulifanya kuwa kiwanda chako inabidi upate picha mpya, au twende tukalione kwa sababu kama kuna watu wanaishi na kulitumia taswira hii unayoiona kwenye picha inaweza kuwa imebadilika sana tu.”

Kim anatabasamu, kisha anatangulia kukataa kwa kichwa tena kama kawaida yake.

“Tangu lijengwe halijawahi kuishi mtu.”

Kazumba akamtazama tena katika hali ya kutoelewa.

“Kwa hiyo hii ni kazi ambayo nitakupa. Nitaenda kesho kwenye jengo hili, nitapiga picha mpya ili kukuridhisha. Yaani ulione kwa sasa likoje na mazingira yake. Naamini hakutakuwa na mabadiliko makubwa.

Kazumba akakubali kwa kichwa kuonyesha kuelewa. Alichoelewa hapo ni hilo suala la kwenda kesho kupiga picha mpya lakini si maelezo mengine yaliyotangulia!

Kwamba jengo hilo kwa miaka yote ishirini hakuna mtu anaishi wala mpangaji! Lipo lenyewe tu!

Maswali yakajijenga kichwani mwake, kama hajaenda miaka yote hiyo, ana uhakika gani kama lipo. Na kama lipo, ana uhakika gani kwamba hakuna watu waliolivamia na kulitumia? Kama hajawahi kwenda kwa miaka 15 anajuaje kwamba jengo halijavunjika na kubomoka na pengine hata kiwanja chake kishajengewa nyumba nyingine?

Ras Kim alikunywa kinywaji chake na kuweka chupa chini.

Kazumba akamtazama akitegemea kusikiliza maelezo zaidi.

Ni kweli, yalikuwepo.

“Kule Zimbabwe nina kiwanda kikubwa cha mikate. Kinahudumia miji mikubwa na vijijini. Sasa huo muda ukifika wa kulazimika kuwa mmiliki nitahitaji kuongeza majengo machache ili nifanye kuwa kiwanda kikubwa kama kile kihudumie ukanda wote huu.”

“Sawa. Ntakupeleka ofisini ukakutane na wataalamu wa kila aina. Kama unataka kufanya kitu kikubwa na tofauti - basi umefika mahali pake. Utapata majengo bora na ya kudumu. Hata ikibidi kulikarabati, sisi tutakufanyia kazi nzuri sana.”

“Kwa hiyo umeniambia kabla kuandaa michoro itategemea na majengo yatakayohitajika. Si ndio ulivyoniambia. Au kutembelea eneo husika?” Ras Kim alizungumza.

“Mimi ni mtu wa masoko tu, ukionana na wataalamu wetu, watakuambia cha kuzingatia. Lakini... Hebu nikurudishe nyuma kidogo... Unasema jengo halijatumika na mtu yoyote kwa miaka 20, na wewe hujafika hapo mahali kwa miaka 15, ina maana ni jengo lililotelekezwa. Una uhakika gani kwamba lipo salama, au bado lipo au halina watu wanaoishi?”

Ras Kim akatabasamu na kuchelewa kujibu! Ni mtu anayeongea bila papara na kwa uangalifu. “Kuna siri nyingine za maisha ni lazima zitunzwe. Si wewe tu, hata kijiji kizima ambacho jengo hilo lipo hawajui  kitu. Lakini nina uhakika lipo na hakuna mtu anayeishi ndani yake. Kwa kukuongezea tu, sijalitelekeza, kwa sababu jengo lina maana kubwa sana kwenye maisha yangu.”

Kazumba akawa anamtazama tu.

Ras Kim akaonekana kuguswa na hisia fulani. Alitulia kidogo, akawa anaangalia pembeni, kisha akapata cha kuzungumza kilichoendana na hisia alizoonekana nazo.

“Nikifikiria kuhusu hili jengo na kutimia kwa miaka 20 naumia sana. Moyo wangu unakuwa mzito kulichukua na kulitumia. Kwa sababu lengo kuu la kujenga jengo hili halikutimia. Natamani isingetimia. Labda hapa tunapozungumza ingekuwa miaka 10 au 15! Kwamba lile tumaini ningekuwa nalo! Lakini linayeyuka! Linayeyuka kama moshi angani.”

Kazumba akamtazama kwa makini.

“Hebu naomba unisaidie kupunguza maswali kichwani kwangu. Naomba nikuulize. Iliwezekanaje kuwepo miaka yote hiyo bila wavamizi kumega eneo, au kukutwa na yale niliyokuuliza mwanzo?”

Ras Kim akatabasamu!

“Zindiko.”

Kazumba akaduwaa.

* * * * * * * * *

Zaka aliacha kuangalia jengo lenye ofisi za chama cha madalali! Alishakata tamaa nao! Aliwachukia!

Wamemlazimisha kusubiri!

Kwamba wana kesi za madalali ambao wanazishughulikia.

Madalali waliokosa uaminifu kwa wateja zao!

Kwenye wengi pana mengi. Madalali walikuwa wengi, kwa hiyo katika hao, wapo wachache ambao wana tabia tofauti, tabia zinazowaletea kesi hata kushitakiwa au kushitaki mahakamani.

Kwamba hao ndio wanaosaidiwa!

Yeye anaambiwa asubiri!

Kwani kesi na ugonjwa wa mtoto anayekaribia kupoteza maisha, kipi kikubwa!

Hili ni swali lililomsumbua sana.

Ni swali lililomfanya ajidharau mwenyewe na kujiona kama mjinga kwa kukubali kuendelea kuwepo kwenye chama kama kile.

Lakini pia kilikuwa ni chama cha kilazima. Kuwepo kwenye chama hicho ulikuwa ni mwito wa serikali, kwamba vikundi na watu wanaofanya kazi zinazofanana ni lazima kuunda vyama kwa ajili ya uwakilishi na usaidizi mbalimbali.

Wakati mwingine chama hicho hufanya mambo makubwa na kusaidia madalali wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali – ila yeye ameambiwa asubiri!

Hata hivyo, alirudi nyuma na kukumbuka kwamba ni siku chache tu tangu apeleke maombi hayo! Kwa maana kwamba huko nyuma kuna wenzake waliowahi na kupeleka shida zao mbalimbali! Zikiwemo hizo kesi!

Kwamba amechelewa!

Hapana!

Suala lake ni dharura!

Ina maana kama kikitokea kifo leo hawatamchangia akazike?

Alipopata swali hili, akataka kurudi nyuma!

Akataka kurudi kwenye chama cha madalali na kuwauliza! Lakini simu ikaita!

Akaitoa na kuiangalia. Jina la Mama Doto likaonekana!

Moyo ukampasuka!

Mtoto hakuamka vizuri, halafu akiwa kwenye shughuli zake, simu ya mkewe inaita! Kidogo aliogopa! Aliiangalia simu hii akijishauri apokee kwa staili gani!

Lakini kuna stori ndogo aliikumbuka katikati ya kujishauri huko.

Stori aliyosimuliwa na yuleyule mheshimiwa mbunge!

Mbunge yule alisema kwamba miaka fulani nyuma, alikuwa akimuuguza mama yake mzazi. Alifanya jitihada kubwa ikiwa ni pamoja na kumsafirisha kwenda nje ya nchi mara kadhaa kwa tiba.

Inaendelea...