Hatma ya vita Harmonize, Ibraah

Muktasari:
- Mzozo baina ya wawili hao ulianza Mei 3, 2025 baada ya Ibraah kuweka wazi kwenye akaunti yake ya Instagram anaomba michango kutoka kwa Watanzania ili kujinasua kwenye Lebo ya Konde Gang, inayomilikiwa na Harmonize.
GUMZO kubwa kwenye burudani nchini kwa sasa ni mzozo wa msanii Harmonize na Ibraah. Wawili hao wamefikishana kwenye mamlaka ya uamuzi ambazo huenda Jumatano hii zikatamka jambo.
Ndiyo siku ambayo watakutana uso kwa uso ofisi za Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Dar es Salaam.
Mzozo baina ya wawili hao ulianza Mei 3, 2025 baada ya Ibraah kuweka wazi kwenye akaunti yake ya Instagram anaomba michango kutoka kwa Watanzania ili kujinasua kwenye Lebo ya Konde Gang, inayomilikiwa na Harmonize.
“Dah! Hili mimi limenishinda narudi kwenu Watanzania mzee Konde anataka nimlipe B1. Mimi tangu nianze muziki sijawahi kuingiza hata robo ya Sh1 bilioni kwa itakayempendeza hata ukiwa na buku nisaidieni.
“Mimi sitaki kubishana na mzee Konde ila hili suala la kulipia Sh1 bilioni linaninyima usingizi hofu yangu pia kipaji changu kupotea na sina kazi nyingine. Kwa yeyote atakaye jaaliwa chochote,” aliandika Ibraah kwenye ukurasa wake wa Instagram.
Utakumbuka Konde Music Worldwide (Konde Gang) ya Harmonize mwaka huu inatimiza miaka sita tangu kuanzishwa kwake Alhamisi ya Oktoba 10, 2019.
Konde Music ilikuja baada ya Harmonize kuachana na WCB Wasafi, lebo yake Diamond Platnumz na ndiyo iliyomtoa kimuziki mwaka 2015, kupitia wimbo wake maarufu, ‘Aiyola’.
Ndani ya Konde Gang, Aprili 11, 2020 ilitangaza kumsaini msanii wa kwanza ambaye ni Ibraah, Mei 8 mwaka huo akaachia ‘Extended Playlist (EP)’ yake, ‘Steps’ ikiwa na nyimbo tano alizowashirikisha Joeboy, Skibii na Harmonize.
Licha ya hayo kutokea miaka hiyo nyuma, sasa wawili hao wamechukua sura mpya kwenye mitandao ya kijamii kutokana na kurushiana kwao maneno.
Mei 11, 2025 Harmonize kupitia ukurasa wake wa Instagram aliandika: “Nimemchunguza sana mdogo wangu Chinga nimegundua ana roho **** na kama sio ibilisi amempanda kichwani. Maana hata siku aliyoposti na kusema namdai 1B ni ile siku ya birthday ya mjukuu wangu Amarah, yaani mimi na kipenzi changu tunatrendi.
“Guys, sijamuomba Chinga bilioni ila mkataba aliosaini na lebo unasema ikitokea watu wanataka kumnunua wenye malengo makubwa zaidi ya Konde Gang. Pengine tunaweza tofautiana kipato, inatakiwa ailipe lebo ya Konde Gang 1B ili wawasaidie vijana wengine na nilimwambia nitabaki kuwa kaka yako na Konde Gang chama lako, mchangieni.”
Hata hivyo baada ya mnyukano huo mkali kwenye mitandao, Uongozi wa Kampuni ya Harmonize Ent.Ltd kupitia Lebo ya Konde Gang Music Worldwide ilitoa taarifa rasmi ya kumsimamisha Ibraah kutoa na kushiriki katika shughuli zozote za muziki hadi suala lake la kujitoa kwenye lebo hiyo litakapopatiwa ufumbuzi.
“Uongozi wa kampuni ya Harmonize Entertainment Ltd kupitia lebo yake ya Konde Gang Music Worldwide unapenda kutoa taarifa kwa umma kama ifuatavyo. Mnamo tarehe 03/05/2025, tulipokea barua ya madai (Demand Notice) kutoka kwa Wakili wa msanii wetu, Ibrahim Abdallah Nampunga IBRAAH.
“Barua hiyo iliainisha madai kadhaa ambayo uongozi umeanza kuyafanyia kazi mara tu baada ya kuipokea, kwa mujibu wa taratibu za kisheria na kimkataba. Licha ya juhudi zetu kujaribu kumuelekeza msanii taratibu za kufuata kulingana na mkataba wake.
“Hivi karibuni, tumebaini kuwepo kwa machapisho, matamshi, na mawasiliano kutoka kwa Ibraah katika vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii, ikiwemo Instagram na Facebook,” ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo iliendelea kwa kueleza machapisho hayo yanaonyesha malalamiko na lugha isiyofaa kwa afya ya lebo pamoja na kumhusisha mkurungezi muwekezaji wa lebo ambaye bado anaendelea kufanya kazi chini ya lebo hiyo.
“Tungependa kufafanua kuwa machapisho na matamshi hayo siyo tu yanachafua taswira ya lebo na wasanii wake, bali pia yanakiuka utamaduni wetu kama Watanzania na kukiuka masharti ya mkataba aliosaini na lebo hii. Aidha, yanaenda kinyume na sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Kampuni yetu inahifadhi haki zake zote za kisheria katika suala hili. Wakati huu ambapo mchakato wa kushughulikia masuala haya unaendelea, umma unapaswa kufahamu kwamba Ibrah bado ni msanii halali wa Lebo ya Konde Gang Music Worldwide na ina haki ya kuendelea au kusitisha mkataba wake kwa kufuata na kuzingatia taratibu rasmi zilizowekwa katika mkataba aliosaini,” ilieza taarifa hiyo na kuongezea kuwa.
“Konde Gang inampiga marufuku Ibraah dhidi ya kuchapisha, kutamka, au kufanya mawasiliano yoyote kuhusu suala hili kwenye vyombo vya habari au mitandao ya kijamii (kama vile Instagram, WhatsApp, Facebook, n.k.). Hii ni pamoja na mawasiliano ya aina yoyote ambayo yanaweza kuharibu taswira ya lebo au kumdhalilisha mkurugenzi muwekezaji wa lebo ambaye ni msanii,”
Aidha taarifa hiyo ilisisitiza kuwa inatoa onyo kali iwapo masharti hayo yatakiukwa, lebo haitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi yake katika Mahakama za Tanzania.
Mnyukano huo uliokuwa ukipokea maoni mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii ulifika Basata na kupelekea Mei 12,2025 wawili hao kuitwa. Hata hivyo katika wito huo alifika Ibraah pekee bila ya Harmonize kuonekana ofisini hapo. Baada ya mazungumzo na msanii huyo Mkuu wa Kitengo cha Sheria Basata, Christopher Kamugisha alisema wamesikiliza malalamiko ya pande zote mbili kuhusu wito wa wasanii Harmonize na Ibraah. Ambapo maamuzi waliyokubaliana ni kufika wote kwenye ofisi za Basata Jumatano hii asubuhi saa 5 kwa ajili ya kusikilizwa.
“Tumefanikiwa kuongea na pande zote mbili, upande wa Harmonize na Ibraah, ila tumepanga kuongea siku ya Jumatano ili wasanii wote tuliowaita waweze kufika wakiwa na wanasheria wao.
Ikumbukwe Konde Music ilisimamia wasanii saba ambao ni Harmonize, Ibraah, Country Boy, Anjella, Cheed, Killy na Young Skales kutoka Nigeria lakini hadi sasa wote wamejiengua kundini aliyebaki ni Ibraah ambaye ana sakata hilo.
Tangu kuanzishwa kwa lebo hiyo, hakuna msanii wa Konde Music ambaye ameshinda tuzo kimataifa ingawa Harmonize amekuwa akitajwa kuwania tuzo kama Afrimma (Marekani) na Afrima (Nigeria). Katika tuzo za Muziki Tanzania (TMA) 2021 zilizotolewa Aprili 2024, Harmonize pekee ndiyo aliibuka kidedea.