Kumbe Rodrygo alikataa kucheza El Clasico

Muktasari:
- Fowadi huyo mwenye umri wa miaka 24 siku zake zinahesabika kwenye kikosi hicho cha Wahispaniola na huenda akapigwa bei dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi.
MADRID, HISPANIA: STAA wa Real Madrid, Rodrgyo imeripotiwa kugomea kucheza mechi ya El Clasico baada ya kutibuana na wachezaji wenzake kikosini.
Fowadi huyo mwenye umri wa miaka 24 siku zake zinahesabika kwenye kikosi hicho cha Wahispaniola na huenda akapigwa bei dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Rodrygo aliishia tu kukaa benchi kwenye mechi hiyo ambayo iliishuhudia Real Madrid ikikumbana na kichapo cha mabao 4-3 kutoka kwa mahasimu wao wa El Clasico, Barcelona, Jumapili.
Kipigo hicho kilikuwa na madhara makubwa kwa Real Madrid na sasa imeachwa pointi saba nyuma na Barcelona na bado mechi tatu tu kwa msimu wa La Liga kufika tamati.
Kocha Carlo Ancelotti angependa kuanza na kikosi chake cha kwanza bora kabisa, lakini Rodrygo hataki kuchezea tena timu hiyo.
Jambo hilo limeibuliwa na gazeti la Marca linalodai winga huyo anahisi hatendewi inavyopaswa kwenye timu. Kinachoelezwa baada ya ujio wa Jude Bellingham na Kylian Mbappe kwenye kikosi hicho jambo hilo lilimvuruga sana winga huyo wa Kibrazili.
Rodrygo alitaka kuwa mchezaji muhimu kwenye timu sambamba na Vinicius Junior na amechukia baada ya jambo hilo kushindikana. Hata hivyo, haionekani Bellingham au Mbappe wamefanya kosa lolote.
Lakini, uhusiano wa Rodrygo na wachezaji wenzake umedhorota kwa kiwango kikubwa.
Kocha Xabi Alonso ambaye atatua Bernabeu kuchukua mikoba ya Ancelotti yupo tayari kumfungulia mlango wa kutokea Rodrygo. Na Ancelotti ameteuliwa kuwa kocha mpya wa Brazil na atakwenda kufanya kazi na Rodrygo.
MAVITU YA RODRYGO LA LIGI MSIMU HUU
-Amecheza: Mechi 30
-Ametengeneza: Nafasi 49
-Amefunga: Mabao 6
-Ametoa: Asisti 5
-Amelenga goli: Mashuti 20
-Amepiga: Pasi 990