KONDE BOY NI HARMONIZE AU LUIS?

Muktasari:
WIKI hii msanii wa Bongofleva, Harmonize alikutana na mchezaji wa Simba SC, Luis Miquissone ambaye tangu atue nchini alipewa jina la ‘Konde Boy’ kwa kuwa anatokea Msumbiji nchi ambayo inapakana na Mkoa wa Mtwara ambao wenyeji wake wengi ni kabila la Wamakonde anapotokea Harmonize.
WIKI hii msanii wa Bongofleva, Harmonize alikutana na mchezaji wa Simba SC, Luis Miquissone ambaye tangu atue nchini alipewa jina la ‘Konde Boy’ kwa kuwa anatokea Msumbiji nchi ambayo inapakana na Mkoa wa Mtwara ambao wenyeji wake wengi ni kabila la Wamakonde anapotokea Harmonize.
Mastaa hao walikutana mara baada ya Simba SC kuwachapa AS Vita ya DR Congo bao 4-1 katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo Miquissone alifunga goli la kwanza na kufikisha jumla ya magoli matatu katika michuano hiyo.

Je, kukutana kwao kuna maana gani hasa? Ukweli ni kwamba kukutana kwao kumeibua maswali kutokana na mambo yaliyokuwa yakiendelea hasa upande wa Harmonize. Haya ni maswali hayo na majibu yake.
1. Kwanini Harmonize hakupewa jezi ya Simba?
Miquissone alimpatia Harmonize jezi namba 11 anayoivaa kwenye timu ya taifa ya Msumbiji na kuibua swali ni kwanini hakumpatia jezi ya Simba na ukizingatia walikutana muda mfupi baada ya timu hiyo kufuzu kucheza robo fainali ya Klabu Bingwa Afrika.
Jibu ni kwamba Harmonize asingeweza kuipokea jezi ya Simba kwa kuwa yeye ni sababu wa kutupwa ya Yanga SC, hivyo hilo lingeweza kumuharibia upande wa kibiashara kati yake na timu yake hiyo.
Ikumbukwe mwaka jana Harmonize alikuwa ni miongoni mwa wasanii waliotumbuiza kwenye tamasha la Yanga, Siku ya Mwananchi na kuibua gumzo kwa kitendo chake cha kushuka kikomandoo kwa kutumia kamba kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam. Pia alitunga wimbo maalum wenye mahadhi ya singeli kwa ajili ya timu hiyo.
Hivyo basi, iwapo angepokea jezi ya Simba kuna uwezekano mkubwa wa kutokuja kupewa nafasi kama hiyo na Yanga siku za usoni kutokana na utamaduni klabu hizo kongwe nchini. Pia ingekuwa ni ngumu kwa Miquissone kupokea jezi ya Yanga kutoka kwa Harmonize hasa nje ya uwanja.
2. Kwanini Miquissone apewe jina la Jeshi na sio Konde Boy?
Harmonize aliamua kumpa Miquissone jina la Jeshi kwa namna ambavyo amekuwa akionyesha kiwango kizuri uwanjani na kuisaidia timu yake kuondoka na pointi muhimu dhidi ya mshindani wake, iwe Klabu Bingwa Afrika au VPL.
Hilo likaibua swali kwanini Harmonize ampe jina la Jeshi na sio Konde Boy ambalo ndio limezoeleka na mashabiki wengi wa soka nchini? Hapa kuna majibu mawili;
Mosi; Harmonize anatumia jina la Konde Boy kama chapa yake kibiashara, na hata mwanzo aliwaonya mashabiki wa Simba kutumia jina hilo kwa Miquissone kwani amefanya kazi kubwa kulifanya kuwa maarufu na kutambulika na wengi, hivyo haliwezi kutumika na yeyote bila idhini yake.
Hata lebo yake ‘Konde Music Worlwide’ inaanza na jina hilo, hivyo kuna uwezekano tayari amelisajili kwa mamlaka husika kulitumia katika biashara yake ya muziki, hivyo si rahisi kumpatia mtu mwingine.
Pili; Jina la Jeshi alilompa Miquissone, Harmonize hajaliweka upande wa kibiashara sana zaidi ya kulitaja kwenye nyimbo zake, pia ukizingatia yeye sio msanii wa kwanza Bongo kulitumia. Ikumbukwe kundi la Navy Kenzo linaloundwa na Nahreel na Aika ndio wasanii wa kwanza kuanza kutumia jina hilo na asili yake ni neno, Navy.
Imeandikwa na Peter Akaro