Madee: Rayvanny hajapotea kutoka WCB
![Madee Pict](/resource/blob/4924510/60600ba6b526892c617a6b5367b3d47b/madee-pict-data.jpg)
Muktasari:
- Madee ameliambia Mwanaspoti, watu wanataka Rayvanny afanye kiki zake ambazo watu wengi wamezizoea kuzisikia ndio wajue hajapotea?
MWIMBAJI wa muziki wa Bongofleva, Madee amewatolea uvivu watu wanaosema Rayvanny amepotea kimuziki toka atoke Lebo ya WCB.
Madee ameliambia Mwanaspoti, watu wanataka Rayvanny afanye kiki zake ambazo watu wengi wamezizoea kuzisikia ndio wajue hajapotea?
"Napingana na watu wanaosema Rayvanny amepotea toka atoke Lebo ya WCB, yaani simuoni kama kapotea, mbona anasikika sana tu, ametoa nyimbo kibao nzuri zimehit, ameenda kufanya kazi ya muziki nje ya nje na haya juzi kati ametoka huko,au watu wanataka afanye zile kiki zake ambavyo vijana wamezoea kuzisikia?" Amehoji Madee.
Aidha Madee aliendelea kusema kuwa hata kutoka kwa Rayvanny Lebo ya WCB asilaumiwe mtu yeyote kati ya Diamond Platnumz ambaye mwenye Lebo hiyo au Rayvanny aliyekuwa anaitumikia kwani,alishajiona amekuwa na kwenda kuanza maisha yake sehemu nyingine.
"Msanii anapotaka kutoka kwenye Lebo hatupaswi kumlaumu mtu yeyote,sababu huyo anaonekana amekuwa anaenda kuanza maisha yake sehemu nyingine, yaani kama sisi tulivyo, tumekuwa tunalelewa na wazazi wetu ikifikia muda fulani inatakiwa twende tukajitafutie wenyewe," amesema Madee na kuongeza;
![MD 01](/resource/image/4924548/landscape_ratio2x1/320/160/2b5fc78adfa952f56f3a95b50c26f06e/PY/md-01.jpg)
"Sasa sisi tuliokuwa pembeni ndio tunaangalia je atafanikiwa hapo ndio tutapata majibu kumbe huyu alikuwa anategemea kulelewa kwahiyo ni kitu kizuri mtu kwenda kujianzishia kitu chako mwenyewe kama alivyofanya Rayvanny na wasanii wengine, na Rayvanny ni Moja kati ya wamuziki wenye ni dhamu ya hali ya juu sana, na hili ni sababu alitengenezewa njia nzuri toka alipokuwa WCB na ameweza kuondoka nayo vizuri, na ili ufanikiwe kwenye kitu chochote lazima uwe na nidhamu kwanza, kwahiyo Rayvanny nidhamu yake haijawahi kupungua haijapotea "amesema Madee
Hata hivyo, Madee amesema hakuwahi kuwa na Lebo kama baadhi ya watu wanavyodhani, bali alikuwa anafanya hisani kwa wasanii kwa kuwakusanya wanatengeneza kitu kimoja kinafanyika.
"Kitu ambacho watu wengi hawakielewi hawajui kama Mimi sikuwa na Lebo ya muziki, nilikuwa nafanya hisani Kwa wasanii ambao niko nao karibu, tunajikusanya pamoja tunatengeneza kitu, kwahiyo sikuwahi kufanya biashara ya Lebo ya muziki na ndio maana unaona tunaweza Kukaa mwaka hakuna kitu kinachofanyika kwetu, Sasa kama ningekuwa nayo mtu huwezi Kukaa mwaka bila kufanya biashara siutapata hasara."
Amesema katika hiyo hisani aliyokuwa anaifanya, kwenye suala la malipo inategemea mtu anayefanyiwa hisani ndio atawaza kumpatia kitu gani kwani ni jukumu lake.
"Kumfanyia mtu hisani sio lazima upate mlipo, japo nashukuru nilishawahi kupata kitu kutoka kwa wasanii nilikuwa nao, lakini Mimi msanii katika historia yake akinitaja tu jina langu kuwa Kuna kitu kizuri nilimfanyia kwenye safari yake ya muziki kwangu mimi ni baraka tosha na upendo wa hali ya juu,hayo mambo mengine ni jukumu lake kuamua kunipa pesa au kutonipa."
Madee amezungumzia pia kiki za kwenye muziki, amesema muziki wasasa upo kwenye kiki na watu wapo kabisa kuwekeza kwenye kiki ili wafanikishe hizo kiki.
![MD 02](/resource/image/4924550/landscape_ratio2x1/320/160/799fc23a3550c1f033fcdf448091a234/NN/md-02.jpg)
"Muziki wa sasa hivi upo kwenye kiki,watu wanawekeza kabisa ili afanikishe hizo mambo, sababu online TV zipo, magazeti, instagram na mitandao mengine zimeweka vitu hivyo kwanza kabla ya muziki wao, na hili sababu watu wanapenda kusikia umefanya nini Jana usiku umekutwa na mwanamke wa watu,umepigwa baada ya hapo ndio wanakuja kusikiliza muziki wao, hivi vitu vipo tayari watu wanaviweza vizuri kudili na hivyo vitu," amesema na kuongeza;
"Sasa sisi tuliotoka kitambo huko kabla ya haya mitandao tunaweza kubakia kwenye mstari wetu, na nadhani ndio heshima inayoendelea kuwepo kulingana na umri na nyakati tulizonazo sisi wanamuziki wa zamani, leo huwezi nisikia eti Madee amefumaniwa na nani na nani sijui, au jana katembea na mwanamke huyu sijui ilimradi wimbo wangu uende hapana, mie nitatoa kazi yangu kama nilivyozoea kutoa zamani ila waimbaji wa sasa hivi ndio wanaitaka iwe hivyo hivyo, tuwaache wafanye tu."