Mastaa wanavyonufaika na umaarufu wa kazi zao

Muktasari:
- Sio ajabu kuona msanii akipewa dili la fedha nyingi kwa lengo la kutangaza biashara, bidhaa, huduma au kuhamasisha kampezi fulani kupitia mitandao ya kijamii, ushawishi wa chapa ya msanii husika hasa mtandaoni ndio unaleta fursa hiyo.
Umaarufu wa kazi zao unawafanya wasanii kutengeneza chapa zenye ushawishi mkubwa na hivyo kujikusanyia mamilioni ya wafuasi katika mitandao ya kijamii kitu ambacho ni fursa nyingine kwao kuingiza fedha nje ya sanaa yao.
Sio ajabu kuona msanii akipewa dili la fedha nyingi kwa lengo la kutangaza biashara, bidhaa, huduma au kuhamasisha kampezi fulani kupitia mitandao ya kijamii, ushawishi wa chapa ya msanii husika hasa mtandaoni ndio unaleta fursa hiyo.
Kwa mujibu wa Influencer Marketing Hub, Selena Gomez ndiye msanii duniani anayelipwa fedha nyingi kutangaza katika mtandao wa Instagram, Selena mwenye wafuasi zaidi milioni 420 Instagram anakadiriwa kulipwa Dola2.5 milioni kwa tangazo moja.
Selena ambaye anafanya muziki na filamu amekuwa akitangaza bidhaa za urembo na mitindo na kwa jumla ni watatu katika ya watu wenye ushawishi (influncer) duniani wanaolipwa vizuri akiwa ametanguliwa na Cristiano Ronaldo na Lionel Messi.
Hata hivyo, ukweli, sio kila msanii maarufu mwenye idadi kubwa ya wafuasi kwenye mitandao ya kijamii ana nguvu ya ushawishi ya kumwezesha kupata dili hizo kama wengi wanavyodhani.
Pia baadhi ya wasanii wamekuwa wakilalamika chapa kubwa zimekuwa zikitoa dili hizo kwa upandeleo, kitu ambacho kinafafanuliwa na wenzao.
Wasanii wa Bongo Fleva, Rosa Ree na G Nako wamekuwa na maoni yanayoshabiana kuhusu hilo wakati wakiongea na gazeti hili, wote wamekiri ni fursa kwao ya kuingiza kipato nje ya muziki wao.
Rosa Ree ambaye amekuwa akitangaza bidhaa za pombe na nywele, anasema ni biashara nzuri ambayo inategemea zaidi msanii husika ameijenga vipi chapa yake mbele ya jamii na wanaohitaji kumtumia.
"Ni kitu kikubwa kwa sababu sanaa ni ajira, pale kampuni zinakufuata zinataka kufanya kazi na wewe ina maana sanaa yako ina ushawishi katika jamii. Kwa hiyo ni kitu kikubwa ambacho kimewapa mafanikio makubwa wasanii wengi na nina furahi na mimi ni miongoni mwa hao, nimepata dili nyingi," anasema.
"Kwa kifupi hiki kitu ni kikubwa kwa wasanii kwani imeweza kutengeneza mlango mwingine wa kuingiza kipato upande wetu. Shukrani kwa mashabiki wameniweka sehemu ambayo imenifungulia milango mingi," anasema Rosa Ree.
Rosa anasema kampuni yoyote inapomtazama msanii na kuona ana ushawishi na anaweza kuwaongezea kitu, ndipo wanamuita mezani na kumpa dili, hakuna msanii anayepewa dili kwa bahati mbaya, lazima uwe na kitu ambacho unakiweka mezani na yeye.
"Hivyo wasanii wote unaona wanafanya kazi na kampuni mbalimbali, ni kwamba wanaweza kushawishi jamii kuhusu bidhaa na huduma za kampuni husika, pia wanaweza kuwaongezea kiasi kikubwa cha mauzo ndiyo maana wanatoa hizo dili," anasema.
Kwa upande wake G Nako kutoka kundi la Weusi ambaye anatangaza mavazi, huduma za mitandao ya simu, pombe n.k, anasema wasanii kupata dili hizo kwa wingi sasa ni ishara tasnia inazidi kukua.
"Ni kitu kingine ambacho inaonyesha tasnia inatanuka, kampuni nyingi zinawatumia wasanii kama 'influencer' na hiyo inaonyesha wasanii ni watu wanaoaminika na kuweza kuzishika hizo chapa na kwenda nazo sokoni," anasema.
Je, kampuni hizo zinapokuwa zinamfuata G Nako huhitaji nini hasa kutoka kwake na kwa kuzingatia nini?. Rapa huyo anasema cha muhimu na taswira (image) ambayo tayari msanii anakuwa ameitengeneza ambayo inaendana na bidhaa anayoenda kuitangaza.
"Ni namna msanii anavyokuwa ameijenga chapa yake na chapa nyingine zinakuwa zinakuona na kila chapa inakuwa inamhitaji msanii kwa namna ambavyo anakuwa amejiweka mbele ya jamii," amesema na kuongeza.
"Kwa mfano mimi nimewejiweka kama mtu ambaye napenda mavazi, kwa hiyo ni rahisi kumshawishi mtu ambaye anatengeneza chapa zake na mavazi kuniona. Au ni mtu ambaye anapenda kusafiri, ni rahisi kwa mtu ambaye anahusika na vitu vya safari kama hoteli kuniona na kunipa dili," anasema G Nako.
Naye Mtaalamu wa Chapa na Mawasiliano, Docta Ulimwengu ambaye anasimamia chapa za wasanii kama Hamisa Mobetto, Idris Sultan, Jux n.k, amesema linapokuja suala la biashara kinachoangaliwa kwa msanii ni ushawishi kuendana na chapa ya mteja tu.
"Chapa inapotafuta balozi inaangalia mtu mwenye ushawishi kuendana na chapa yake na sio mtu anayefanya vizuri kwenye tasnia yake. Naweza kupenda muziki wako lakini sipendi unavyovaa, kwa hiyo hata ukitangaza bidhaa ya nguo sitoinunua kwa sababu sikuamini kwenye mavazi," anasema Docta Ulimwengu.
Ikumbukwe Diamond Platnumz kutokea WCB Wasafi aliwahi kudai kwa mwezi mmoja anapokea Sh200 milioni kwa kutangaza bidhaa na huduma mbalimbali, dili ambazo anazipata kutokana na ushawishi wake.