Mo Dewji alivyochochea mageuzi ya soka Tanzania

Muktasari:
- Katika orodha mpya ya mabilionea iliyotolewa na Forbes, Machi 30, 2025, Dewji ambaye ni mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi na mwekezaji wa Simba, ametajwa kuwa na utajiri unaofikia Dola 2.2 milioni (Sh5.8 trilioni) tofauti na ule wa Dola 1.8 bilioni (Sh4.52 trilioni) wa mwaka 2024.
Wakati jarida la Forbes likimuorodhesha Mohammed Dewji (MO) kuwa bilionea wa 12 barani Afrika katika chati mpya ya 2025, klabu ya Simba ni taasisi ya michezo iliyonufaika na utajiri huo.
Katika orodha mpya ya mabilionea iliyotolewa na Forbes, Machi 30, 2025, Dewji ambaye ni mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi na mwekezaji wa Simba, ametajwa kuwa na utajiri unaofikia Dola 2.2 milioni (Sh5.8 trilioni) tofauti na ule wa Dola 1.8 bilioni (Sh4.52 trilioni) wa mwaka 2024.

Kiwango hicho cha fedha kinamfanya aendelee kushika nafasi ya 12 barani Afrika huku kinara akiwa ni Mnigeria Aliko Dangote.
Mafanikio makubwa ambayo Simba imeyapata katika miaka ya hivi karibuni ni ishara tosha ya jinsi utajiri wa Dewji alivyochangia kuleta mageuzi ndani ya klabu hiyo ambayo mfanyabiashara huyo amejitanabaisha kuwa shabiki na mwanachama wake kindakindaki.
Baada ya kukaa nje ya Simba kwa muda, Dewji alirejea ndani ya klabu hiyo mwaka 2017 ambapo muda mfupi baada ya kuingia kwake, Simba ilianza kuwa tishio katika soko la usajili kwa wachezaji wa ndani na nje.

Baadhi ya nyota ambao walisajiliwa katika ujenzi wa Simba mpya ni Erasto Nyoni, Aishi Manula, Shomari Kapombe, Meddie Kagere, Emmanuel Okwi, Shiza Kichuya, Mzamiru Yassin, John Bocco, Clatous Chama na Haruna Niyonzima.
Nyota hao wakiungana na baadhi ambao walikutwa klabuni na wapya walioongezeka baadaye waliifanya Simba kuwa kupata mafanikio makubwa uwanjani.

Tangu 2017 hadi sasa, Simba imetwaa mataji manne ya Ligi Kuu Tanzania Bara, mataji matatu ya Kombe la Shirikisho la CRDB, mataji manne ya Ngao ya Jamii, Kombe moja la Muungano na Kombe moja la Mapinduzi.
Simba imeonekana kutamba kimataifa ambapo imeingia katika hatua ya robo fainali ya mashindano ya klabu Afrika mara sita tofauti huku mara nne ni katika Ligi ya Mabingwa Afrika na mara mbili ni katika Kombe la Shirikisho Afrika.
Ni Mo Dewji ambaye fikra zake za kubadili uendeshaji wa klabu ya Simba kutoka mfumo wa kizamani kwenda kuwa wa kisasa wa kuendeshwa kikampuni na uwekezaji, umechochea mabadiliko kwenye klabu nyingine za soka Tanzania kama watani wao Yanga ambao nao waliingia katika mfumo huo.
Chini ya bilionea huyo, Simba ambayo hapo nyuma haikuwa hata na pointi katika chati ya ubora wa klabu za soka Afrika, sasa ni klabu ya sita Afrika katika orodha ya klabu bora kwa mujibu wa chati ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Ikumbukwe mwanzoni mwa miaka ya 2000, Dewji alileta mabadiliko ya malipo kwa wachezaji kutoka mfumo wa kulipwa kwa posho hadi mishahara rasmi wakati huo alipoanza kuingia ndani ya Simba.
Dewji ambaye pia ni shabiki wa Arsenal, mbali na kuwekeza Simba, amekuwa na ndoto za kumiliki timu Ulaya ambapo kwa mujibu wake lengo ni kuukuza mpira wa Afrika.
"Mimi ni shabiki wa Arsenal, lakini nataka kununua klabu ya Ulaya kwa sababu ninataka kujenga uhusiano kati ya klabu za soka za Afrika Mashariki na klabu za Uingereza," alinukuliwa Dewji katika mahojiano yake siku za nyuma.
Mbali na soka, Dewji pia amekuwa na ndoto za kusimamia mchezo wa masumbwi akifafanua kuwa nia ni kuwafungulia fursa za kiuchumi vijana.
Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Mussa Hassan ‘Mgosi’ amesema kuwa hakuna namna mafanikio ya Simba yatatajwa bila Dewji kuhusika.

"Ukiangalia maisha ya enzi hizo na sasa, ni wazi kwamba Dewji amechangia kwa kiasi kikubwa kuifanya Simba kuwa klabu kubwa zaidi Afrika na ni mtu, ambaye anahitajika kuendelea kuwepo," alisema Mgosi.
Mchambuzi wa soka, Lilian Mukulu amesema kuwa Dewji ameuchangamsha mpira wa Tanzania.
"Kuna mengi ambayo Dewji ameyafanya katika soka la Tanzania, lakini makubwa ni kupandisha thamani ya wachezaji hasa wa Kitanzania lakini pia kuijenga Simba kuwa kati ya timu kubwa Afrika," alisema Mukulu.