Fountain Gate yamsimamisha kipa kisa mabao ya Yanga

Muktasari:
- Noble amefungwa mabao mawili kati ya manne waliyofungwa na Yanga akicheza kwa dakika 45 za kipindi cha kwanza kabla ya benchi la ufundi kufanya uamuzi wa kufanya mabadiliko kumwingiza kipa mwingine ambaye naye alifungwa mabao mawili, akiokoa hatari nyingi.
UONGOZI wa Fountain Gate umemsimamisha kipa wake John Noble kwa makosa yanayodaiwa kuwa ni ya kizembe kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Yanga timu hiyo ikikubali kichapo cha mabao 4-0.
Noble amefungwa mabao mawili kati ya manne waliyofungwa na Yanga akicheza kwa dakika 45 za kipindi cha kwanza kabla ya benchi la ufundi kufanya uamuzi wa kufanya mabadiliko kumwingiza kipa mwingine ambaye naye alifungwa mabao mawili, akiokoa hatari nyingi.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya timu hiyo kimeliambia Mwanaspoti kuwa ni kweli wamefanya uamuzi wa kumsimamisha mchezaji huyo kutokana na kufanya makosa mawili yaliyoigharimu timu hiyo.
“Ni kweli tumemsimamisha hatujapendezwa na makosa aliyoyafanya ambayo yamesababisha timu yetu kuondolewa mchezoni kutokana na uzembe wa mtu mmoja ambaye ameighalimu timu nzima.”
Kocha wa Fountain Gate, Robert Matano baada ya mchezo alisema; “Golikipa leo amewapa mabao. Ametuangusha kabisa golikipa wa aina yake kufanya makosa kama yale, sasa kama tunacheza vizuri halafu tunapeana mabao vile itakuwa vigumu sisi kushinda,” alisema na kuongeza;
"Hawezi kufanya makosa kama yale golikipa wa kariba ya juu kama yeye ametutoa mchezoni kabisa, kwa mabao aliyofungwa hakuna timu yoyote hata Yanga pia wangeanza kufungwa mabao kama yale wangetoka mchezoni."
Alipotafutwa Ofisa Habari wa klabu hiyo, Issah Liponda Mbuzi kuthibitisha suala hilo alijibu kuwa hajui chochote na yeye anaona kwenye mitandao.
“Hata mimi naona kwenye mitandao tu, sijafahamishwa chochote na uongozi wangu wa juu, siwezi kuzungumza lolote juu ya suala hilo,” alisema Issa Mbuzi.
Fountain Gate imefungwa na Yanga jumla ya mabao 9-0 katika Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kufungwa 5-0 katika mechi yao ya mzunguko wa kwanza Desemba 29, 2024.