Prime
Simba yapewa refa wa 1-0 Sauzi

Muktasari:
- Kuteuliwa kwa Omar kunakuja katika kipindi ambacho mashabiki wa Simba bado wana kumbukumbu na mwamuzi huyo kusimamia chama lao kwenye kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Horoya ya Guinea, Novemba 2, 2023, mechi ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF), limemkabidhi mwamuzi wa kimataifa kutoka Misri, Amin Omar jukumu la kuchezesha mechi ya marudiano ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Stellenbosch dhidi ya Simba itakayopigwa Aprili 27, 2025 kwenye Uwanja wa Moses Mabhida jijini Durban, Afrika Kusini.
Kuteuliwa kwa Omar kunakuja katika kipindi ambacho mashabiki wa Simba bado wana kumbukumbu na mwamuzi huyo kusimamia chama lao kwenye kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Horoya ya Guinea, Novemba 2, 2023, mechi ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Yorokoguia nchini Guinea, Simba walicheza vizuri lakini walizidiwa mbinu, huku refa huyo akiibua mjadala baada ya kuwapa Horoya penalti ambayo hata hivyo haikuzaa bao, kwani Pape Abdou N’diaye alikosa mkwaju huo.
Tofauti na Jean Jacques Ndala wa DR Congo aliyechezesha mechi ya kwanza huko Zanzibar kwa utulivu Simba ikishinda 1-0, Omar anajulikana kwa kuwa mkali wa kadi. Takwimu zinaonyesha kuwa hadi kufikia sasa amesimamia mechi 17 katika mashindano mbalimbali na kutoa jumla ya kadi 66 ikiwa ni wastani wa kadi 3.8 kwa kila mchezo.
Cha kushangaza ni kwamba, licha ya ukali huo wa kutoa kadi za njano bado hajatoa nyekundu msimu huu, jambo analoweza kuelezewa kuwa mwamuzi anayejaribu kuweka nidhamu kwa nguvu ya tahadhari badala ya adhabu kali.
Uteuzi huo wa Omar unapaswa kuifanya Simba kuwa makini zaidi hasa kutokana na mtindo wake wa kusimamia mechi kwa ukali.
Kwa kuteuliwa Omar, Simba inapaswa kujiandaa kwa mchezo mgumu utakaohitaji nidhamu ya hali ya juu ili kuepuka faulo zisizo za lazima na kuhakikisha hawajiingizi kwenye mtego wa kupoteza mwelekeo kutokana na uamuzi wa mwamuzi huyo.
Simba inaisaka fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kufanya hivyo 1993 katika Kombe la CAF - michuano iliyokuja kuunganishwa na Kombe la Washindi na mwaka 2004 kuzaliwa kwa Kombe la Shirikisho Afrika.