Bayer Leverkusen yakubali kwa Alonso

Muktasari:
- Alonso aliiongoza timu hiyo ya Ujerumani kutwaa ubingwa wa Bundesliga msimu uliopita, na msimu huu wanatarajiwa kumaliza nafasi ya pili nyuma ya Bayern Munich.
LEVERKUSEN, UJERUMANI: MKURUGENZI wa Bayer Leverkusen, Fernando Carro amethibitisha hatma ya kocha wao Xabi Alonso itaamuliwa katika wiki chache zijazo baada ya mazungumzo zaidi na wangependa kuendelea kuwa naye lakini hawatomzuia ikiwa ataamua kuondoka kwa sasa.
Alonso aliiongoza timu hiyo ya Ujerumani kutwaa ubingwa wa Bundesliga msimu uliopita, na msimu huu wanatarajiwa kumaliza nafasi ya pili nyuma ya Bayern Munich.
Kocha huyu anahusishwa kujiunga na Real Madrid ambayo mustakabali wa kocha wake Carlo Ancelotti, bado haujulikani huku ripoti zikieleza anaweza akaondoka katika timu hiyo kabla ya kumalizika kwa mwezi huu.
Moja ya sababu zinazoonekana kuchangia sana Madrid kuachana na Ancelotti ni kiwango cha timu hiyo katika michuano mbalimbali, ikiwa imeondoshwa katika Ligi ya Mabingwa na katika La Liga bado inaenda kwa kusua sua licha ya kuwa nafasi ya pili.
Alonso,43, aliyewahi kuwa kiungo wa Liverpool, inadaiwa alishafanya makubaliano ya ‘kiheshima’ na Leverkusen na ataruhusiwa kufikiria kujiunga na moja ya timu alizowahi kuzichezea na aliwahi kuwa na mafanikio akiwa na Real Madrid, Bayern Munich na Liverpool.
“Hapana, lakini tuna makubaliano ambayo yanaeleza ikiwa timu aliyowahi kuichezea itakuja, tutakaa chini tuzungumze na hatutamwekea vikwazo. Hivyo inaweza kuwa Bayern, Liverpool, Real Madrid na Real Sociedad... labda hata Real Sociedad itakuja, ”alisema Mkurugenzi wa Leverkusen, Carro.