Mtihani KenGold baada ya kushuka

Muktasari:
- Kushuka kwa KenGold inafanya timu hiyo kurudia ilichowahi kufanya Mbeya Kwanza (2021-2022), Ihefu na Gwambina (2020-2021), African Lyon (2018–19) na Njombe Mji (2017-2018) ambazo nazo zilipanda na kushuka katika misimu ya hivi karibuni.
LICHA ya KenGold kushuka daraja huku ikiwa na michezo mitatu mkononi, lakini bado timu hiyo inakabiliwa na mtihani mmoja wa kuhakikisha haiachi rekodi mbaya zaidi kwenye Ligi Kuu Bara.
Kushuka kwa KenGold inafanya timu hiyo kurudia ilichowahi kufanya Mbeya Kwanza (2021-2022), Ihefu na Gwambina (2020-2021), African Lyon (2018–19) na Njombe Mji (2017-2018) ambazo nazo zilipanda na kushuka katika misimu ya hivi karibuni.
Rekodi zinaonesha katika misimu kumi kuanzia 2014-2015 hadi uliopita 2023-2024, hakuna timu iliyoshuka daraja ikiwa na pointi 16 kama ilizonazo KenGold kwa sasa, hivyo timu hiyo mechi tatu zilizobaki ina mtihani wa kufanya kuepuka rekodi hiyo mbovu zaidi.
Katika mechi hizo tatu zilizobaki, KenGold inaweza kujitetea itakapocheza nyumbani dhidi ya Pamba Jiji na Simba, kisha kumalizia ugenini kwa Namungo.
Kwenye kujitetea huko, inakutana na timu ambazo zipo kwenye vita kali, Simba inawania ubingwa ikiwa nafasi ya pili na pointi 57, huku Pamba Jiji yenye pointi 27 nafasi ya 13, inapambana isishuke daraja kwani hivi sasa ipo kwenye mstari wa kucheza mechi ya mtoano. Namungo inashika nafasi ya tisa na pointi 31, bado nayo haijajihakikishia kubaki ligi kuu kwani ikipoteza mechi tatu zilizobaki kwa idadi kubwa ya mabao kisha timu sita zilizopo chini zikashinda inaweza kushuka.
Rekodi za timu zilizomaliza mkiani mwa Ligi Kuu Bara na pointi zao kuanzia 2014-2015, ni Polisi Morogoro iliyokuwa na 25 msimu huo, huku 2015-2016 Coastal Union ikimaliza na pointi 22.
JKT Ruvu nayo msimu wa 2016-2017 ilipata pointi 23, huku 2017-2018 Njombe Mji ilimaliza na pointi 22. Msimu wa 2018-2019, African Lyon ilimaliza na pointi 23, kisha 2019-2020 Singida United ikawa na pointi 18.
Mwadui iliyoshuka msimu wa 2020-2021, ilikuwa na pointi 19, wakati 2021-2022 Mbeya Kwanza ikawa na 25, huku 2022-2023 Ruvu Shooting ikimaliza na 20. Mtibwa Sugar katika msimu wa 2023-2024 ilimaliza na pointi 21.
Chini ya Kocha Omary Kapilima, KenGold imeshuka daraja baada ya kufungwa mabao 2-1 dhidi ya Coastal Union katika mchezo uliofanyika Jumatatu wiki hii kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Matokeo hayo yameifanya KenGold kubaki mkiani na pointi 16 ikiwa na michezo mitatu ambayo hata ikishinda yote haitatoka katika nafasi mbili za mkiani ambazo zinaipa tiketi ya kushuka daraja.
Kuhusu mechi tatu zilizobaki, Kapilima alisema: “Ninakwenda kujipanga katika michezo mitatu iliyobaki, tumetoka kufungwa na tumekubali matokeo.”
Winga wa KenGold, Hija Ugando, alisema: “Bado tutaendelea kupambana hadi mwisho, hatujakata tamaa.”