Mratibu wa zamani Miss Tanzania, Lundenga afariki dunia

Muktasari:
- Taarifa ya kifo chake imethibitishwa na Katibu wa Kamati ya Miss Tanzania, Bosco Majaliwa.
Mratibu wa zamani wa Miss Tanzania, Hashim Lundenga amefariki dunia leo Apili 19,2025 katika Hospitali ya Itengule iliyopo Tegeta jijini Dar es Salaam.
Taarifa ya kifo chake imethibitishwa na Katibu wa Kamati ya Miss Tanzania, Bosco Majaliwa.
“Ndio Hashimu Lundenga amefariki kama masaa mawili yaliyopita katika Hospitali ya Itengule iliyopo Tegeta hapa. Hashimu ameumwa muda mrefu sana, nafikiri taarifa ya kuumwa kwakwe watu wengi wanayo, alipata ‘stroke’ muda mrefu sana, alilazwa kwenye Hospitali Muhimbili alitolewa, alilazwa Mlongazila akatolewa akawa anaendelea kupata kliniki lakini hali ikazidi kuwa mbaya zaidi.
Kwahiyo jana alizidiwa wakamleta hapa kwenye Hospitali ya Itengule lakini bahati mbaya amefariki dunia, msiba upo nyumbani kwake Bunju,” amesema Majaliwa
Aidha aliongezea kuhusiana na mazishi ya mratibu huyo akieleza “Kwa sababu ndio tupo hapa kufanya taratibu za kupeleka mwili mochwari kwahiyo watakaa pale nyumbani watajadiliana kama atazikwa hapa au utaratibu utakuwa vipi,”
Lundenga ambaye ameugua kwa muda mrefu alisimamia mashindano ya urembo Tanzania na kufanya yajulikane na kupata umaarufu, utakumbuka aliachia kijiti cha kusimamia Miss Tanzania 2018 tangu alipoanza kusimamia shindano hilo mwaka 1994, huku akimkabidhi kijiti Basila Mwanukuzi.
Mbali na hilo lakini pia Lundenga aliwahi kuhudumu kwenye Kamati ndani ya Klabu ya Yanga.