Rose Muhando amuombea Harmonize aoe

Muktasari:
- Dua hiyo imekuja baada ya Harmonize kucheza challenge ya wimbo wa Rose Muhando uitwao ‘Amina’ na kwa kitendo hicho Rose amesema kimempa heshima kubwa kwake na kujua ni shabiki wa kazi zake.
MKONGWE wa muziki wa Injili nchini, Rose Muhando amesema amekuwa akimuombea dua njema mkali wa Bongo Fleva, Harmonize a.k.a Konde Boy, ili aweze kuzidi kufanikiwa katika kazi zake za sanaa na kubwa zaidi aoe mwaka huu.
Dua hiyo imekuja baada ya Harmonize kucheza challenge ya wimbo wa Rose Muhando uitwao ‘Amina’ na kwa kitendo hicho Rose amesema kimempa heshima kubwa kwake na kujua ni shabiki wa kazi zake.
Rose alisema atazidi kumuombea dua njema, Harmonize ili aweze kupata mwanamke mwema mwaka huu wa kumuoa.
“Kiukweli nitoe pongezi kwa Harmonize kwa kuweza kucheza chalenji ya wimbo wangu wa Amina, kitendo hiki ni kikubwa sana kwangu kwani ni wasanii wachache wakubwa wenye kuweza kusapoti kazi za watu wengi kama hivyo, na napenda pia kuona kijana huyu (Harmonize) mwaka huu apate mke mwema wa familia na kuoa kabisa. Hii dua naiomba kuanzia sasa,” alisema Rose.
Chalenji ya kucheza wimbo wa Amina uliotoka 2009, imeibuliwa upya kwa kasi sana katika mtandao wa TikTok hivi karibuni kwa baadhi ya watu kucheza na kuanguka.