Shilole awaponda wanaotoa siri za waume zao

Muktasari:
- Akizungumza na Mwanaspoti, Shilole alisema tabia hiyo imekuwa ikimkera sana na yeye kwenye maisha yake hawezi kuthubutu kufanya hivyo.
MSANII wa Bongo Fleva na mfanyabiashara, Zuwena Mohamed 'Shilole' amewaponda wanawake wanaopenda kutoa siri za waume zao au wanaume wanaoachana nao na kusema huo ni ulimbukeni uliopitiliza.
Akizungumza na Mwanaspoti, Shilole alisema tabia hiyo imekuwa ikimkera sana na yeye kwenye maisha yake hawezi kuthubutu kufanya hivyo.
“Mimi mwanamume hata nikiachana naye siwezi kwenda kumtangaza madhaifu yake kwa watu wengine, kufanya hivyo nitakuwa namdhalilisha na kujidhalilisha mimi mwenyewe.
“Hivi mwanamume ambaye umetoka naye unaanzaje kumtangaza madhaifu yake, halafu wewe ukaikwepa aibu?” alisema Shilole na kuongeza, ameolewa na kuachika zaidi ya mara tatu, lakini hakuwahi kuwazungumzia vibaya wanaume hao.
"Nadhani binadamu tumeumbwa tofauti na kila mmoja anakuwa na tabia yake. Mimi unanifahamu vizuri napenda ndoa sana, ila nimeolewa na kuachana na wanaume zaidi ya wawili lakini hukuwahi kusikia nimewazungumzia vibaya hadharani, hivi ndivyo inavyotakiwa kwa wanawake, hata wanaume nao pia, tusiachane kwa kudhalilishana."
Shilole ameshawahi kufunga ndoa tatu na wanaume tofauti na baadae wakaja kuachana na ya awali aliolewa na dereva wa malori wakati akiwa na umri wa miaka 17, ambaye alikuja naye Dar es Salaam akitokea kwao Igunga ambako alikuwa tayari amepata mtoto wa kwanza. Akazaa mtoto mmoja kwenye ndoa hiyo, akiwa ni wa pili kwake. Baadaye mwaka 2009 akaachana na mwanamume huyo kwa talaka akimtuhumu kumpiga hadi kumdhuru mguu wake wa kulia.
Ndoa ya pili alifunga na Ashraf Uchebe ambaye waliachana baada ya awali kuvuja kwa picha zikimuonyesha akiwa amejeruhiwa usoni kisha akaolewa na aliyekuwa mpigapicha wake, Rommy 3D ambaye naye waliachana.