Wameweka tofauti pembeni, waonywa

Muktasari:
- Ni hivi. Hivi karibuni mastaa watatu wa Bongo Movie, Irene Uwoya, Jacline Wolper, Aunt Ezekiel na Kajala Masanja wameonekana kwa nyakati tofauti wakiwa pamoja.
ONYO. Ndiyo. Mashabiki wamechoka na vurugu za mastaa wao na sasa wameamua kuwafungukia ‘live’ hawataki kuona au kusikia mambo yao yanajirudia kwani inawaboa.
Ni hivi. Hivi karibuni mastaa watatu wa Bongo Movie, Irene Uwoya, Jacline Wolper, Aunt Ezekiel na Kajala Masanja wameonekana kwa nyakati tofauti wakiwa pamoja.
Hii ni baada ya miaka ya nyuma kuingia katika mabifu baina yao na kusababisha majibishano na kutukanana mitandaoni na kuwafanya mashabiki kuingilia kati na wengine kugawanyika kabla ya kuamua kumaliza tofauti zao hivi karibuni.
Inaelezwa wasanii hao hawakuwa wakiiva kwa sababu mbalimbali ikiwamo mapenzi, kazi za sanaa na biashara na ni kama kila mmoja ameona yaliyokuwa yanaendelea hayana maana na badala yake wawe kitu kimoja.
Sasa basi, umoja huo ndiyo ukawaibua mashabiki na kuwataka wasirudie tena mambo ya nyuma ya kugombana na pia kuvunjika kwa mahusiano yao na ndoa.
Pia wamewataka kuangalia kitu cha kufanya chenye faida kwao na siyo hasara na kusababisha mahusiano yao na wapenzi wao kuvunjika.
wa kwanza alisema; “Hapa sasa sawa, kama hawa wasanii wameamua kuwa pamoja tena basi tunataka wawe hivi hivi na siyo kuja kugombana tena maana tunawajua hawa huwa hawakawii kugombana na kurushiana maneno mitandaoni. Ukweli hii ni hatua nzuri sana, hongera kwao ila tu urafiki wao usije kusababisha pia kuvunjika kwa mahusiano yao na wapenzi wao, familia muhimu na urafiki muhimu.”
Shabiki mwingine alifunguka; “Nimefurahishwa kuwaona pamoja Uwoya, Wolper, Aunt Ezekiel na Kajala, ila nawapa onyo wasije kuwa mbali tena, kama wameamua kuungana basi sawa na tunataka kuungana kwao basi kuwepo na faida, yaani wafanye mambo ya maana tujue kama wameamua kufanya kitu kwao na mashabiki zao.”

Wenyewe wafunguka
Wakizungumza na Mwanaspoti kwa nyakati tofauti, wasanii hao wameeleza sababu ya wao kuwa na tofauti huko nyuma.
Wolper anasema; “Kwanza niwatoe hofu mashabiki zangu na watu wangu wa karibu, watu sasa hivi tumekuwa watu wazima wenye kujitambua. Binafsi siwezi kuvunja ndoa yangu sababu ya kuwa karibu na Uwoya, Kajala na Aunt Ezekiel, kwani kwangu familia kwanza, vitu vingine baadae.
“Na sidhani kama itatokea kukorofisha kwani mwanzo kilichokuwa kinaniponza mimi ni kusema ukweli, yaani unanikosea nakupa ukweli wako ukikasirika lakini nakuwa nishakwambia. Hiki kitu wengi walikuwa hawanijui niko hivyo, ila nashukuru kwa sasa wote hawa wameshanijua na wanaweza kuishi na mimi bila tatizo lolote na hata kama likitokea huwa tunalimaliza kwa haraka sana,” anasema Wolper.
Kajala anasema kilichokuwa kinamponza ni mitandao ya kijamii kuleta ugombanishi kwa watu wake hao wa karibu.
“Yaah wanachosema watu tusije kugombana wanaweza kuwa sahihi kabisa, ila wajue kilichokuwa kinafanya kuwa hivyo huko nyuma ni mitandao ya kijamii. Kuna watu wanaitumia vibaya kunigombanisha na watu wangu wa karibu
“Yaani mtu anaweza kuongelea kitu changu akamhusisha rafiki yangu kwa namna mbaya sana, ila sema sasa hivi nimejua kuishi na watu wa mitandaoni, hivyo sitaweza kuyumbishwa na maneno yao,” anasema Kajala.

Kwa upande wa Aunt Ezekiel anasema;
“Hili ni kawaida watu hubadilika, upendo hubadilika ndivyo ilivyo kwenye maisha yetu ya kila siku. Watu wanakuwa marafiki au wapenzi na baadaye wanageuka kuwa maadui. Lakini bila kutegemea baada ya muda tena wanapatana na inawezekana wakatofautiana tena. Lakini kwa sasa hakuna kitu kinaweza kutokea hivyo sababu siyo muda wote yupo karibu na sisi ukaribu wetu upo kwenye kazi, kipo kitu kinakuja na wala siyo tupo kufanya starehe, suala la kuvunjika mahusiano hakitatokea kwani nipo na mwanamume muelewa sana Kusah na tunaamini ana sana.”
Uwoya anasema tatizo kubwa linalochagia ugomvi wao ni mitandao ya kijamii, kumezuka makundi ambayo yamekuwa yakitumia utabiri wao wanaoufahamu wenyewe kuzidi kuchochea ugomvi uliokuwepo kati ya yeye na wasanii hao baadhi.
“Kwanza niseme kitu kimoja, ukaribu wetu sisi hapa kwa sasa upo zaidi kwenye kazi, kuna kitu tunakiandaa kukifanya, halafu pia tumeshakuwa watu wazima mambo ya bifu bifu ni mambo ya kitoto sana na sidhani kama tutarudi huko tulipokuwa zamani, hapa maisha yalishapita, kipindi kile chanzo kikubwa kilikuwa makundi ya watu ndiyo yamekuwa chachu kubwa ya bifu za watu kugombana na kuzidisha mapambano kati ya wasanii kwa wasanii, sema mimi nilikuwa napenda sana kukuangalia tu timu zinazotuzunguka zinazidi kututia chumvi ili tugombane, sasa hakuna wa kuweza kufanya hivyo watu tushavuka huko,” anasema Uwoya.

Tujikumbushe
Kipindi cha nyuma Wolper alishawahi kugombana na Aunt Ezekiel kisa mchezo wa upatu aliokuwa anachezesha Aunt na ilidaiwa Wolper alikuwa anadaiwa pesa nyingi na kulipa alikuwa mgumu.
Hii ilisababisha sauti zao kuvuja za kutoleana maneno wakiwa kundi lao la upatu kupitia mtandao wa WhatsApp.
Wolper pia alishawahi kuingia bifu na Kajala kisa penzi la Harmonize na baada ya kuachana na Harmonize ndiyo akaingia Kajala na kuna vijembe vya maneno vilikuwa vinatembea mtandaoni kwa wawili hao.
Pia Aunt aliwahi kugombana na Uwoya kisa biashara ya vinywaji. Aunt alianza kufungua sehemu ya kuuza vinywaji ‘pub’ na kuwavuta wasanii wengi kumpa sapoti katika pub yake, baada ya muda Uwoya akafungua naye pub hapa ndipo ikaleta bifu za kuchukulia na wateja na kuwayumbisha wasanii wenzao waende wapi kula kinywaji.
Hizo ni baadhi tu za bifu zilizowahi kutrend za wasanii hao ambao kwa sasa ni mashosti ambao kwa sasa wanaonekana pamoja sehemu mbalimbali za starehe na kwenye sherehe na mikutano.