Prime
WCB Wasafi: Miaka 10, wasanii 9 wakisainiwa

Muktasari:
- Hatua hiyo inakuja wiki chache baada ya Mbosso kuripotiwa kuachana na lebo hiyo ambayo ilimtambulisha mwaka 2018 ikiwa ni zaidi ya mwaka mmoja tangu kusambaratika kwa kundi la Yamoto Band ambalo alikuwepo.
REKODI Lebo inayosifika kwa kutoa wasanii wakali, WCB Wasafi tayari imeweka wazi kumsaini msanii mwingine ambaye atakuwa ni wa tisa katika historia yao tangu kuanza kazi hiyo takribani miaka 10 iliyopita.
Hatua hiyo inakuja wiki chache baada ya Mbosso kuripotiwa kuachana na lebo hiyo ambayo ilimtambulisha mwaka 2018 ikiwa ni zaidi ya mwaka mmoja tangu kusambaratika kwa kundi la Yamoto Band ambalo alikuwepo.
Utakumbuka mwanamuziki wa kwanza kusainiwa WCB Wasafi ni Harmonize aliyetoka na wimbo wake, Aiyola (2015) uliofanya vizuri hadi mwanamuziki huyo kushinda tuzo mbili, AFRIMMA na AEAUSA kama Msanii Bora Chipukizi 2016.
Hata hivyo, biashara ya pande hizo mbili ilifikia tamati mwaka 2019 baada ya Harmonize kuvunja mkataba akiwa tayari ni chapa kubwa katika muziki akishirikiana na wasanii kama Burna Boy na Yemi Alade waliosikika katika EP yake, Afro Bongo (2019).
Mkurugenzi Mtendaji wa WCB Wasafi, Diamond Platnumz ndiye amethibitisha kusainiwa kwa msanii huyo mpya wiki hii ingawa bado haijajulikana ni nani na lini atatambulishwa kwa mashabiki.
“A new icon is coming!,” ameandika Diamond katika Insta Story huku akionyesha sehemu ya mkataba ambao umesainiwa Machi 18 kati ya huyo ambaye hajatajwa dhidi ya kampuni ya Wasafi Limited (WCB).
Hilo linajiri wiki mbili baada ya Diamond kuahidi kusaini wasanii wawili waliofanya vizuri katika Bongo Star Search (BSS) msimu wa 15 na Moses Luka kutokea DR Congo ndiye aliibuka mshindi huku nafasi ya pili ikienda kwa Saluh wa Tanzania.

Ikiwa kweli Diamond atafanya hivyo, itakuwa ni mara ya kwanza kuchukua wasanii waliofanya vizuri katika shindano hilo la kusaka vipaji vya uimbaji ambalo lilianza rasmi mwaka 2006 chini ya Benchmark 360.
Ikumbukwe Harmonize naye alipita BSS lakini hakufanya vizuri akitolewa hatua za mwanzo kabisa, kwa mujibu wa Master J ambaye ni miongoni mwa majaji wa shindano hilo, hawakufanya makosa wala hawajutii kumtoa maana wakati huo uwezo wake ulikuwa mdogo.
Ila Harmonize si msanii pekee aliyeshindwa BSS kisha akaja kusainiwa na lebo kubwa Bongo, kuna K2ga na Cheed waliochukuliwa na Kings Music ya Alikiba ingawa Cheed aliachana na lebo hiyo na kwenda Konde Music ya Harmonize ambapo hakudumu pia.

Diamond, mshindi wa tuzo kubwa za MTV EMAs mara tatu, anatangaza kusaini msanii mpya ikiwa ni zaidi ya mwaka mmoja tangu amtambulishe D Voice aliyekuja na albamu yake, Swahili Kid (2023) yenye nyimbo 10.
Ndani ya muda mfupi D Voice amepata mapokezi mazuri kazi zake zikipata namba kubwa katika majukwaa ya kidijitali, huku Diamond akiongozana naye katika matukio makubwa na muhimu kama tuzo za Trace 2025 kwa lengo la kumtangaza zaidi.
Tangu kujiunga na WCB Wasafi, muziki wa D Voice ameonekana kuendana vizuri na ule wa Zuchu na hadi sasa wameshirikiana katika nyimbo nne ambazo ni Nimezama (2023), BamBam (2023), Nani (2024) na Hujanizidi (2024).

Ni wazi D Voice anaifukuzia rekodi ya Diamond kwa Zuchu ambaye pia ndiye msanii pekee wa kike Bongo aliyeshirikiana mara nyingi na Diamond aliyetoka kimuziki na kibao chake, Kamwambie (2009) kilichobeba jina la albamu yake ya kwanza.
Diamond aliyeshinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) kama Msanii Bora Chipukizi 2010, wasanii wengi aliowasaini katika lebo yake wamekuwa na mafanikio makubwa kimuziki, mathalani Zuchu tayari ameshinda tuzo saba za TMA ndani ya muda mfupi tu.
Naye Rayvanny alishinda tuzo ya BET 2017 Marekani akiwa ni msanii wa kwanza Tanzania kufanya hivyo na wa pili Afrika Mashariki baada ya Eddy Kenzo wa Uganda aliyeshinda 2015.
Wasanii wanaofanya vizuri zaidi YouTube Afrika Mashariki ni wale walioibuliwa na WCB Wasafi, mfano waliotazamwa zaidi ya mara bilioni 1 katika mtandao huo ukanda huu ni watatu pekee ambao ni Diamond, Rayvanny na Harmonize.

Utakumbuka hadi sasa WCB Wasafi imesaini wasanii nane ambao ni Harmonize (2015), Rayvanny (2016), Queen Darleen (2016), Rich Mavoko (2016), Lala Lava (2017), Mbosso (2018), Zuchu (2020) na D Voice (2023) aliyetoka na kibao chake, Kuachana Singapi (2021).
Hata hivyo, tayari Rich Mavoko, Harmonize, Rayvanny na Mbosso ameachana rasmi na lebo hiyo, huku Queen Darleen akiwa kimya kimuziki kwa takribani miaka mitano sasa, hivyo haeleweki kama bado yupo au ametoka ila kwa jicho la kawaida tu kuna kitu hakipo sawa hapo.