Dili iliyokufa - 7
ILIPOISHIA
Baada ya maelezo yangu polisi hao walimkamata Dastan na yule msichana wakawapakia kwenye gari la polisi. Vile vitu vyote walivyoniibia vikachukuliwa. Mimi nilibaki na mfuko wangu wa pesa. Nikaambiwa niingie kwenye gari..
Kwanza tilikwenda kule hoteli. Karani wa hoteli hiyo alipoulizwa kama alikuwa anamtambua Dastan alisema. “Kwanza huyu msichana ndiye aliyekuwa na huyu mlalamikaji jana usiku. Na huyu jamaa kama sikosei alikuwa ndani ya gari. Alikaa siti ya nyuma “
“Mimi uliniona?” Dastan alijitia kuuliza kwa mshituko.
SASA ENDELEA...
“Ndiyo, nilikuona. Ulikuwa umevaa fulana nyekundu.”
“Hapana, si mimi.”
“Ni wewe.”
“Tulitaka ututhibitishie tu,” polisi mmoja akamwambia yule karani na kuongeza, “Tutakuhitaji kituo cha polisi cha Msimbazi uje uandikishe maelezo yako.”
“Ninahitajiwa nije saa ngapi?”
“Wakati wowote kabla ya saa sita.”
“Sawa, nitafika.”
“Ukifika uliza Koplo Msumi.”
“Sawa, afande.”
Tuliporudi kituo cha polisi, Dastan alijuta. Alipigwa vibao hadi uso ukawa mwekundu.
Mbali na kesi hiyo, alikuwa na kesi nyingine tatu zinazohusu wizi na utapeli. Msichana aliyekuwa naye alipohojiwa alieleza kila kitu.
Alieleza kwamba baada ya mimi kumtongoza, Dastan alimshawishi waniwekee madawa ya kulevya kwenye bia ili nipoteze fahamu, na wakapanga kunihamisha hotelini ili waniibie.
“Baada ya kuhama naye, mlikwenda naye wapi?” polisi aliyekuwa akimhoji alimuuliza.
“Kwa vile alikuwa hajielewi tena, Dastan alisema tukamuache kwenye mfereji.”
“Ni kweli tulimkuta kwenye mfereji asubuhi akiwa na kete ya madawa ya kulevya. Nani alimuwekea?”
“Ni Dastan.”
“Alimuwekea kwa ajili gani?”
“Ili aonekane amelewa unga, afunguliwe mashitaka.”
Hapo na mimi nikafarijika kuona polisi wametambua ukweli kuwa kete waliyonikuta nayo haikuwa yangu.
“Na hizi pesa mlizokutwa nazo ni za nani?” polisi aliendelea kumhoji msichana huyo.
“Ndio hizo zilizoibwa.”
“Dastan amesema ni pesa zake ambazo alizipata baada ya kuuza shamba lake Kibaha hapo jana.”
“Ni muongo. Pesa nyingine amezichukua yule msichana wake tuliyekuwa naye jana.”
“Huyo pia tunamuhitaji pamoja na pesa alizochukua. Yuko wapi?”
“Anaishi Buguruni. Naweza kuwapeleka anakoishi.”
“Tupeleke.”
Polisi wawili wanaume na mmoja mwanamke walitoka na yule msichana. Na mimi niliambiwa nifuatane nao. Tukapanda Land Rover 110 ya polisi, tukaondoka.
Ingawa nilikuwa nahisi kizunguzungu kutokana na pombe niliyokunywa jana yake, nilifarijika kuona wabaya wangu walikuwa wanatiwa mbaroni.
Tulifika katika mtaa mmoja uliopo Buguruni, Malapa. Gari likasimama mbele ya nyumba moja iliyokuwa na duka.
Polisi walishuka na yule msichana, wakaingia naye ndani. Baada ya muda mfupi tu walitoka wakiwa na msichana waliyemfuata. Alikuwa ni yule yule aliyeshirikiana na kina Dastan kuniibia.
Alikuwa amejipara akiwa na mkoba wake. Alionekana kama alikuwa anatoka saluni. Sijui alikuwa anataka kwenda wapi.
Aliingizwa kwenye gari huku uso wake ukiwa umefadhaika, na aliponiona mimi alitahayari na kuinamia chini.
Gari likaondoka.
Tulirudi kituoni Msimbazi. Yule msichana aliyekwenda kukamatwa naye akaanza kuhojiwa. Alikuwa akijaribu kubisha kila kitu, lakini alipotiwa makofi alikiri kushirikiana na Dastan.
“Ziko wapi zile pesa alizokupa?” polisi mmoja alimuuliza.
Msichana huyo alifungua mkoba wake na kuzitoa.
“Hizi hapa. Sijapunguza hata senti tano.”
Polisi walizihesabu pesa hizo na kukuta zilikuwa shilingi milioni tatu.
“Alikupa pesa hizi za nini?”
“Alinipa kama mgao wangu,” msichana akajibu bila aibu.
“Mgao wako wa pesa mlizomuibia mwenzenu?”
Msichana akanyamaza kimya.
“Nyinyi nyote kesho tutawapeleka mahakamani,” polisi wakawambia.
Baada ya hapo, polisi walizuia zile pesa isipokuwa walinipa shilingi laki moja ili niweze kujikimu. Waliniambia nitahitajika kuwepo mahakamani kesho asubuhi.
“Kwa hiyo unaweza kwenda, lakini tujulishe tujue utakuwa hoteli gani.”
“Nitakuwa katika hoteli ile ile.”
“Jihadhari na jiji hili!”
“Nitakuwa makini.”
Siku ile nilikwenda kulala kwenye hoteli ile ile. Asubuhi ya siku iliyofuata nikaenda kituo cha polisi, kisha tukaenda mahakamani.
Dastan na wasichana wake wawili walishitakiwa kwa shitaka la ujambazi na uporaji wa shilingi milioni kumi pamoja na vitu vyangu vyenye thamani ya shilingi laki saba.
Pesa na vitu walivyoiba vilitolewa mahakamani kama vielelezo, kisha nikarudishiwa mwenyewe. Kesi ikaahirishwa kwa mwezi mzima.
Polisi wakaniambia ninaweza kurudi Muheza isipokuwa nihakikishe kuwa ninafika Dar es Salaam katika tarehe iliyopangwa kesi.
Baada ya kuelezwa hivyo, nilikwenda zangu kituo cha mabasi cha Mnazi Mmoja. Nikapanda basi linalokwenda Tanga. Basi hilo lilikuwa linaondoka saa tisa alasiri.
Kutoka saa tisa tuliwasili wilaya ya Muheza saa nne usiku. Nilishuka kijijini kwetu Kibanda, nikatembea kwa miguu nikiwa na mizigo yangu hadi nyumbani kwangu.
Kesi ya Dastan ilichukua miezi sita hadi kumalizika. Kila tarehe ya kesi ilipofika nilikuwa nikienda Dar.
Siku ya hukumu, Dastan na wale wasichana walipatikana na hatia. Walihukumiwa kifungo cha miaka saba kila mmoja. Katika hukumu yake, hakimu alitoa maelezo ya kunisifu.
Alisema, “Ni kweli kitendo alichofanya mlalamikaji na kusababisha pesa zake pamoja na vitu vyake kuibiwa ni cha kizembe, lakini jitihada alizochukua kuwatafuta wabaya wake ni za msingi kwani zimesaidia ulinzi...”
Kutoka hapo ndipo nilipojihusisha na biashara. Nilihamia Tanga mjini ambako nilioa mke. Kwa vile sikuwa na uzoefu na biashara, mtaji wangu ulikata. Baada ya miezi michache tu nikawa sina kitu. Mimi na mke wangu tukaishi katika umasikini kwa muda mrefu.
Miaka ilikuwa imepita. Wakati ule ndipo kulikuwa na vuguvugu la vijana wa Kitanzania kukimbilia Afrika Kusini kutafuta maisha. Nikaamua na mimi nijiingize kwenye mkumbo.
Usiku wa siku moja ambao sitausahau, niliagana na mke wangu.
“Nataka nikuage, mke wangu. Kesho asubuhi ninaondoka,” Wakwetu alimwambia mke wake.
“Unakwenda wapi, mume wangu?” mke wake Zainab Shamba alimuuliza kwa mshituko.
“Naenda Sauzi (Afrika Kusini).”
“Unaenda kufanya nini?” mke wake alimuuliza.
“Kutafuta maisha, mke wangu. Si unaona hali tuliyonayo?”
Zainab alisita kwa sekunde kadhaa kabla ya kumwambia:
“Ni sawa, mume wangu, kwa sababu ni kweli hali yangu imekuwa ngumu tangu biashara zilipoharibika. Lakini kuna kitu kimoja ninataka ukijue.”
“Kitu gani?”
Zainab aliushika mkono wa Wakwetu akaupeleka chini ya tumbo lake.
“Minya minya hapa,” alimwambia akimuonesha mahali hapo.
Wakwetu alipaminya.
“Pana nini?” akamuuliza.
“Hujaona kitu?”
“Sijaona kitu.”
“Hujagusa kitu kigumu?”
“Nimekigusa, ni nini?”
Zainab akatabasamu.
“Tumbo limefunga.”
“Limefunga nini?”
“Na wewe kila kitu hujui? Sikuona siku zangu mwezi huu.”
“Una maana una mimba?”
Zainab akamkubalia kwa kichwa.
“Kumbe ni mimba!”
“Ndiyo.”
Wakwetu akashusha pumzi ndefu.
“Kwani itanizuia nisiende Sauzi?”
“Haiwezi kukuzuia. Nimekuonesha tu ili ujue.”
“Ndio natakiwa nikazane. Karibuni nitaitwa baba na wewe utaitwa mama. Watoto watataka kusoma.”
“Sikiliza, mume wangu, mimba yangu bado ni changa na pia sina hakika kama itaendelea kutokana na hali hii.”
“Hali gani?”
“Kwani hii njaa tunayoshinda nayo huioni wewe?”
“Unadhani mimba inaweza kutoka kwa sababu ya njaa?”
“Ndiyo.”
“Nikiwa Sauzi nitakuwa nakutumia pesa za matumizi, mke wangu.”
Zainab akatabasamu.
“Nitafurahi sana.”
“Nataka, mke wangu, upate afya nzuri uweze kumlea mtoto wetu aliye tumboni mwako.”
“Usijisahau, mume wangu. Ukumbuke kuwa umeacha mke wako akiwa na mtoto wako tumboni.”
“Nitakukumbuka, mke wangu. Mimi naenda Sauzi kwa ajili yenu.”
“Sawa, mume wangu.”
“Ondoa wasiwasi. Niombee nifike salama na nipate kazi.”