Championship ilivyoacha namba, maumivu na rekodi 2025-2026
Muktasari:
- Geita Gold na Kagera Sugar ndio timu pekee zilizojihakikishia kucheza Ligi Kuu Bara moja kwa moja msimu wa 2026-2027, baada ya miamba hiyo kuonyesha ushindani mkali tangu mwanzoni wa ligi, zikimaliza nafasi ya kwanza na ya pili.
LIGI ya Championship imefikia tamati kwa msimu wa 2025-2026 baada ya kivumbi cha jasho na damu kuvuja kwa wachezaji wa timu 16, zilizokuwa zinapigania nafasi mbalimbali hususani ile ya lengo mama ya kupanda Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao.
Geita Gold na Kagera Sugar ndio timu pekee zilizojihakikishia kucheza Ligi Kuu Bara moja kwa moja msimu wa 2026-2027, baada ya miamba hiyo kuonyesha ushindani mkali tangu mwanzoni wa ligi, zikimaliza nafasi ya kwanza na ya pili.
Katika mechi 30, ilizocheza Geita Gold inayofundishwa na Kocha Zubery Katwila imeshinda 24, sare tano na kupoteza moja ikiongoza na pointi 77, ikirejea Ligi Kuu Bara msimu ujao, baada ya kikosi hicho kushuka daraja msimu wa 2023-2024.
Kagera Sugar inayofundishwa na aliyekuwa nyota wa Simba, Yanga na timu ya Taifa Stars, Juma Kaseja imemaliza nafasi ya pili na pointi 72, baada ya kushinda mechi 22, sare sita na kupoteza miwili kati ya 30, iliyocheza msimu wa 2025-2026.
Kaseja aliyewahi kuitumikia pia Kagera akiwa mchezaji na kocha wa makipa, ameirejesha timu hiyo Ligi Kuu baada ya kushuka msimu wa 2024-2025, iliposhinda mechi tano, sare nane na kupoteza 17, ikishika nafasi ya 15 na pointi zake 23.
Wakati Ligi hiyo yenye ushindani mkubwa ikifikia tamati kwa msimu wa 2025-2026, zipo rekodi mbalimbali zilizoandikwa na baadhi ya timu huku nyingine zikiwa ni za maumivu, kama ambavyo Mwanaspoti linakuelezea kwa kina kila kilichojitokeza.
GEITA YAWEKA REKODI MPYA
Licha ya Geita kutwaa ubingwa wa Championship kwa kumaliza vinara, timu hiyo imeweka rekodi ya kumaliza na pointi nyingi (77), kwani kabla ya hapo hakuna klabu iliyoshiriki mashindano hayo iliyofikisha tangu msimu wa 2021-2022.
Msimu wa 2021-2022, bingwa wa Championship alikuwa ni Ihefu ambayo kwa sasa ni Singida Black Stars iliyomaliza kinara na pointi 66, huku msimu wa 2022-2023, maafande wa JKT Tanzania ilimaliza kibabe kwa kuongoza ikiwa imekusanya pointi 63.
Kwa msimu wa 2023-2024, KenGold ya Mbeya iliyoshuka daraja 2024-2025 ikitoka Ligi Kuu, ilimaliza na pointi 70, ikiungana na Pamba Jiji ya Mwanza iliyokuwa na pointi 67, iliyorejea baada ya kusota takribani miaka 23 tangu iliposhuka 2001.
Mabingwa wa Championship msimu wa 2024-2025, Mtibwa Sugar ya Morogoro inayocheza kwa sasa Ligi Kuu Bara ilimaliza vinara na pointi 71, ikiungana na kikosi cha Mbeya City cha jijini Mbeya kilichomaliza nafasi ya pili kwa kukusanya pointi 68.
Kwa maana hiyo, Geita Gold imeandika rekodi ya kutwaa ubingwa wa Championship kwa kukusanya pointi nyingi (77), ikiwa ni mafanikio makubwa kwa Kocha Zubery Katwila aliyewahi kuipandisha pia daraja Ihefu kucheza Ligi Kuu msimu wa 2019-2020.
POLISI TZ, MBEYA KWANZA VITA INAENDELEA
Wakati timu mbili zilizomaliza nafasi ya kwanza na ya pili zikipanda Ligi Kuu moja kwa moja, vita kwa sasa imebakia kwa Polisi Tanzania iliyomaliza ya tatu na pointi 66 na Mbeya Kwanza iliyoshika nafasi ya nne baada ya kukusanya pointi 61.
Katika mechi mbili za msimu huu wa 2025-2026, kila timu imeshinda nyumbani kwake, ikianza Mbeya Kwanza iliyoshinda mabao 4-2, Januari 11, 2026 kisha raundi ya pili kwenye Uwanja wa Ushirika Moshi, Polisi ikashinda pia bao 1-0, Juni 14, 2026.
Timu hizi zitakutana tena katika ‘Play-Off’ (mtoano) na mechi ya kwanza itapigwa Juni 28, huku marudiano yakipigwa Julai 5 na mshindi wa jumla atakutana na atakayepoteza kutoka Ligi Kuu Bara kwa atakayemaliza kwenye nafasi ya 13 na 14.
KAZI IPO HUKU!
Mechi nyingine za mtoano zitakazovuta hisia za mashabiki ni zile zitakazozikutanisha timu zilizomaliza nafasi ya 11, 12, 13 na 14 kusaka tiketi ya kubakia msimu ujao wa ligi zitakapopambana zenyewe kisha kukutana na za Ligi Daraja la Kwanza.
Bigman FC iliyomaliza ya 11 na pointi 36, itacheza na African Sports iliyoshika nafasi ya 14 na pointi 21, huku Songea United iliyohitimisha msimu ikiwa nafasi ya 12 na pointi 32, itakutana na Stand United iliyomaliza ya 13 na pointi 25.
Mechi za mtoano zitaanza kupigwa Juni 27 na marudiano yakifanyika Julai 1 na timu mbili zitakazoshinda kati ya hizo zitabakia Championship na zitakazopoteza zitacheza ‘Play-Off’, nyingine na klabu za Ligi Daraja la Kwanza ili kujitetea.
HAUSUNG FC, BARBERIAN MWENDO ZIMEUMALIZA
Hausung FC ya mkoani Njombe na Barberian FC ya jijini Dar es Salaam zimeshuka rasmi daraja kutoka Ligi ya Championship hadi Ligi Daraja la Kwanza, baada timu hizo zote kuonyesha kiwango kisichovutia tangu kuanza kwa msimu huu wa 2025-2026.
Katika mechi 30, Barberian FC imeshinda tatu, sare tisa na kupoteza 18, ikiwa nafasi ya 15 na pointi 18, huku Hausung FC iliyopanda daraja msimu wa 2024-2025, ikiburuza mkiani na pointi tisa, baada ya kushinda tatu, sare tatu na kupoteza 24.
RHINO, BANDARI WAGENI WAPYA
Wakati Hausung FC na Barberian FC zikishuka daraja, tayari timu mbili za Rhino Rangers kutoka Tabora na Bandari Tanzania ya Mtwara zitashiriki Ligi ya Championship kwa msimu wa 2026-2027, baada ya kufanya vizuri katika Ligi Daraja la Kwanza.
Bandari ilimaliza vinara kundi A na pointi 32, katika Ligi Daraja la Kwanza msimu wa 2025-2026, baada ya kushinda mechi 10, sare mbili na kupoteza mbili kati ya 14, iliyocheza huku ikifunga mabao 25 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa tisa.
Kwa upande wa Rhino Rangers ilimaliza vinara wa kundi B na pointi 35 kwa msimu wa 2025-2026, baada ya kushinda mechi 11, sare mbili na kupoteza moja tu kati ya 14, iliyocheza huku ikifunga mabao 31 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara tisa.
Timu hizo zilicheza mechi ya fainali kusaka bingwa wa Ligi Daraja la Kwanza kwa msimu wa 2025-2026, ambapo Rhino ilitwaa taji hilo kwa kuifunga Bandari Tanzania FC kwa penalti 4-2, baada ya sare ya mabao 2-2, mechi iliyopigwa Juni 17, 2026.
CHIRWA, MAULID WANG’ARA
Sehemu nyingine iliyokuwa na mvuto ni katika vita ya ufungaji bora, ambapo tumeshuhudia wachezaji wawili ambao ni Obrey Chirwa wa Kagera Sugar na Maulid Shaban wa Geita Gold wakimaliza vinara, baada ya kila mmoja wao kumaliza na mabao 18.
Idadi hiyo ya mabao 18, ni sawa na iliyofungwa msimu wa 2024-2025 na wachezaji watatu pamoja, ambao ni Andrew Simchimba, Raizin Hafidh na Abdulaziz Shahame ‘Haaland’ ikionyesha ushindani wa washambuliaji katika suala nzima la kufunga mabao.
Simchimba alifunga mabao hayo akiwa Geita Gold japo kwa sasa anacheza Mtibwa Sugar kwa mkopo kutoka Singida Black Stars, sawa na Raizin Hafidh huku Shahame akiifungia TMA FC ya Arusha ingawa kwa msimu huu yupo Namungo FC ‘Wauaji wa Kusini’.
HAT-TRICK TANO
Baada ya msimu wa 2025-2026, kumalizika tumeshuhudia zikifungwa ‘Hat-Trick’ tano na nyota mbalimbali, ingawa hazijafikia za msimu wa 2024-2025, ambao wachezaji sita walifunga, hali inayoonyesha wazi ushindani na ugumu uliopo wa Championship.
Mshambuliaji wa Kagera Sugar, Mzambia Obrey Chirwa aliandika rekodi ya mchezaji wa kwanza wa Ligi ya Championship msimu huu kufunga mabao matatu (Hat-Trick), wakati kikosi hicho kilipoifunga Hausung kutoka Njombe mabao 3-1, Desemba 2, 2025.
Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Kaitaba Bukoba, mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga, Azam, Namungo, Ihefu (kwa sasa Singida Black Stars) na KenGold, alifunga mabao hayo, akiendeleza kiwango bora cha kuirejesha Kagera Ligi Kuu.
Mwingine aliyefunga (Hat-Trick) ni Boniface Mwanjonde wa Mbeya Kwanza katika ushindi wa kikosi hicho wa mabao 5-0, dhidi ya B19 FC, Desemba 17, 2025, ambapo mchezaji huyo kwa msimu mzima wa 2025-2026, aliifungia timu hiyo jumla ya mabao 11.
Wengine ni Japhet Makarai wa TMA FC ya Arusha aliyeifungia timu hiyo katika ushindi wa mabao 4-2, dhidi ya Stand United, Aprili 19, 2026, huku wa nne ni Salum Ngadu wa Gunners FC wakati kikosi hicho kikiichapa Mbuni FC 3-2, Aprili 20, 2026.
Nyota wa mwisho kufunga ‘Hat-Trick’, ni Frank Ikobela wa Transit Camp ambapo mchezaji huyo alikifungia kikosi hicho cha maafande kilipoichapa Mbuni FC ya jijini Arusha mabao 4-3, katika mechi kali na ya kuvutia iliyochezwa Juni 14, 2026.
KAULI ZA WADAU
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia alizipongeza timu zote 16 kwa ushiriki mzuri wa Ligi ya Championship kuanzia mwanzoni hadi mwisho, huku akitumia pia fursa hiyo kwa kuzipongeza Geita Gold na Kagera Sugar.
“Nitumie fursa hii kwa kuzipongeza Geita Gold na Kagera Sugar kwa kupanda Ligi Kuu Bara, lengo letu TFF ni kuhakikisha kila msimu unakuwa bora zaidi ya uliopita kiushindani, tunashukuru tunaliona hilo siku baada ya siku,” anasema Karia.
Kocha msaidizi wa TMA ya jijini Arusha, Omary Matwiko ‘Tico Tico’ anasema ulikuwa ni msimu mgumu kwa timu hiyo baada ya kumaliza nafasi ya 10, licha ya kuweka malengo ya kukipambania kikosi hicho kicheze Ligi Kuu kwa msimu wa 2026-2027.
“Nafasi tuliyopo inaonyesha jinsi gani ushindani ulivyokuwa, nimekuwa mchezaji wa TMA FC katika Championship na sasa ni kocha, nikiri wazi umekuwa ni msimu mbaya kwetu lakini tunaenda kusahihisha makosa yaliyojitokeza,” anasema Tico Tico.
Kocha Mkuu wa Geita Gold, Zubery Katwila anasema siri ya mafanikio ya kikosi hicho ni umoja na mshikamano kati ya uongozi, benchi la ufundi na wachezaji, jambo ambalo ni nguzo muhimu ya kutwaa ubingwa huo na kurejea Ligi Kuu.