Mbogo: Mkongwe Yanga anayesimama na Pacome, Chama
Muktasari:
- Baada ya kucheza soka la kulipwa nchini kama beki wa kati ‘kitasa’ akiwa na Toto African ya Mwanza, Yanga na hata Kagera Sugar, sasa Mbogo amehamishia nguvu zake katika kulea kizazi kipya cha wanasoka. Ndiyo maana miaka minne iliyopita alianzisha kituo chake cha kukuza vipaji, akiamini kuna watoto wengi wenye vipaji mtaani wanahitaji tu mtu wa kuwaamini.
UKIMUONA leo akisimama pembeni ya Uwanja wa Mirongo, karibu na barabara ya Machemba na katikati ya jiji la Mwanza akiwafundisha vijana namna ya kupiga pasi, kukaba na kusoma mchezo, unaweza kuchukulia poa lakini nyuma ya tabasamu la Ladislaus Mbogo kuna simulizi ndefu ya jasho, majeraha, kukatishwa tamaa na ndoto ambayo hakuwahi kuiacha ife.
Baada ya kucheza soka la kulipwa nchini kama beki wa kati ‘kitasa’ akiwa na Toto African ya Mwanza, Yanga na hata Kagera Sugar, sasa Mbogo amehamishia nguvu zake katika kulea kizazi kipya cha wanasoka. Ndiyo maana miaka minne iliyopita alianzisha kituo chake cha kukuza vipaji, akiamini kuna watoto wengi wenye vipaji mtaani wanahitaji tu mtu wa kuwaamini.
“Nimekuwa nikifikiria jambo hili tangu zamani, nilikuwa napenda sana mpira tangu utoto wangu, nilikuwa najua siku moja nitaacha kucheza, hivyo nilitaka niwe na sehemu yangu ya kuwatoa watoto hapa walipo na kuwafikisha walikofika wengine au hata wanizidi mimi.”
Anasema safari ya kituo hicho haikuwa rahisi hata kidogo. Alianza na watoto wanne tu waliokuwa wakifanya mazoezi kwa mazingira ya kawaida lakini hakukata tamaa. Kadiri siku zilivyokwenda, idadi ikaongezeka hadi kufikia zaidi ya vijana 30.
Leo, anasema, ameanza kuona matunda ya kazi yake. “Kituo sasa kinaelekea mwaka wa nne. Nilianza na watoto wanne, nikapambana mpaka wakafika zaidi ya 30. Cha kufurahisha ni kwamba baadhi yao tayari wameanza kucheza ngazi za juu.”
Mbogo anawataja baadhi ya vijana waliopitia mikononi mwake akiwemo Masanja Batano aliyewahi kucheza Kagera Sugar, Endi Msabila anayekipiga Pamba Jiji, Bakari ambaye yupo Mbeya City chini ya miaka 20 pamoja na kipa Makelele aliyewahi kuwa TRA.
“Nashukuru Mungu kwa kweli. Kwa muda huu mfupi tayari unaanza kuona matunda. Hilo ndilo jambo linalonipa nguvu ya kuendelea.”
Hata hivyo, anasema bado kuna changamoto kubwa katika mfumo wa kuibua vipaji nchini. Kwa maoni yake, si kila mwenye kipaji anapata nafasi anayostahili.
“Kuna vijana wana uwezo mkubwa lakini hawafiki kule wanakostahili. Wakati mwingine si kwa sababu hawajui kucheza, bali kuna watu wanataka upeane kitu kwanza ndipo wakusaidie. Ukikosa uwezo wa kufanya hivyo, mtoto anaweza kubaki mtaani huku kipaji chake kikipotea,” anasema.
SAFARI YA MLIMANI FC
Mbogo anakumbuka kuwa safari yake ilianzia mitaa ya Kirumba, Mwanza ambako pamoja na wenzake waliunda timu ya mtaani iliyoitwa Mlimani FC.
“Sikuwa na safari rahisi. Nimezaliwa Kirumba, Mwanza. Tulianza kama vijana wa mtaani, tukatengeneza timu yetu na baadaye tukaifikisha Daraja la Pili. Nilikuwa nahudumu pia kama nahodha.”
Anaeleza kuwa Mlimani FC ilikuwa sehemu muhimu ya kukuza vipaji huku baadhi ya nyota waliokuja kung’ara baadaye wakipitia hapo akiwemo Jerry Tegete, Obadia Monguza na Joseph.
Lakini changamoto za kifedha ziliifanya timu ishindwe kuendelea na mashindano.
“Tulishindwa hata kuchukua fomu za kuendelea na ligi. Ilikuwa kipindi kigumu sana.”
Baada ya hapo alipata nafasi ya kuichezea Skadi Magu ambako walikwenda kushiriki mashindano ya Daraja la Pili yaliyofanyika Arusha.
Ndiyo mashindano yaliyobadilisha maisha yake. “Tulicheza vizuri sana. Nilikuwepo mimi, Kiji Ruseke, Salvatory Mtebe na wengine. Watu wa FC Arusha wakatuona na mwaka 2004 tukasaini.”
Alicheza msimu mmoja wa Ligi Kuu akiwa FC Arusha kabla changamoto za maisha hazijamfanya aondoke.
MAISHA YALIKUWA MAGUMU
Baada ya kuondoka FC Arusha, Mbogo anasema alirudi Dar es Salaam lakini mambo hayakwenda kama alivyotarajia.
“Nilikaa karibu mwaka mzima bila kucheza mpira, nilikuwa Dar es Salaam, baadaye nikachezea Villa Squad pale Magomeni,” anasema.
Lakini wakati huo huo, kifo cha baba yake kilimlazimisha kufanya uamuzi mgumu. “Mama alikuwa ame-baki peke yake Mwanza, nikasema siwezi kuendelea kubaki Dar, nikarudi nyumbani,” anasema.
Aliporejea Mwanza akajiunga na Mwanza United iliyokuwa chini ya kocha mzee Tegete kabla ya ku-hamia Kagera Sugar ambako alicheza msimu mmoja na baadaye akarudi kuichezea Toto African.
Anasema Toto ndiyo klabu ambayo itaendelea kubaki moyoni mwake kwa kusema; “Hii ni timu am-bayo siwezi kuisahau. Nilipata nafasi kubwa sana pale.”
Anakumbuka alikuwapo kambini pamoja na Kevin Hondani, Mrisho Ngassa na nyota wengine waliokuja kufanya vizuri baadaye.
NDOTO YA YANGA NA UPASUAJI
Baada ya kung’ara akiwa Toto, Yanga ilimfuata na kumsajili. Hata hivyo, ndoto yake ya kung’ara Jangwani haikutimia kama alivyotarajia.
“Ushindani ulikuwa mkubwa sana nakumbuka wakati huo Yanga ilikuwa Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Mbuyu Twite. Nilikuwa nacheza beki lakini safu ya ulinzi ilikuwa imara. Katika timu kubwa wakati mwingine ili upate nafasi ni lazima aliyepo afanye makosa.”
Anasema pamoja na kujituma mazoezini, muda mwingi alicheza mechi za kirafiki pekee huku nafasi za mashindano zikiwa chache.
Kana kwamba hiyo haitoshi, afya yake nayo ikawa kikwazo, anasema; “Nilikuwa na uvimbe ambao nilizaliwa nao. Viongozi wa Yanga walinisaidia kufanyiwa upasuaji lakini baada ya operesheni nikakaa nje kwa muda mrefu.”
Kukaa nje kwa msimu mzima kulimuumiza zaidi kuliko majeraha yenyewe, anasema; “Mchezaji una-taka kucheza, unapokaa nje muda mrefu unaanza kuona ndoto zako zinabadilika.”
ALIVYOONDOKA YANGA
Baada ya kukaa kwa muda mrefu nje ya uwanja kutokana na upasuaji na kushindwa kupata nafasi ya kudumu kikosini, Mbogo anasema alijua wazi kuwa kuendelea kubaki Yanga kungemaliza kabisa mai-sha yake ya soka.
“Nilikaa nikajiuliza, nikiendelea kubaki hapa kiwango changu kitakuwa kinaenda wapi? mchezaji ukikaa benchi muda mrefu unazidi kupotea,” anasema.
Badala ya kusubiri maamuzi ya wengine, alichukua hatua mwenyewe, anasema; “Niliandika barua kwa viongozi wa Yanga nikawaomba waniache niende nikacheze sehemu nyingine. Nilihitaji kucheza kuliko kubaki na jina la kuwa mchezaji wa Yanga bila kupata nafasi.”
ALIVYOPIGWA MILIONI 10
Hatua hiyo ilimfanya kutua Rhino Rangers ya Tabora, alitumaini angeanza ukurasa mpya wa maisha yake ya soka lakini mambo hayakwenda kama alivyotarajia, timu ilipambana msimu mzima lakini mwishoni ikashuka daraja. “Kisoka haukuwa msimu mzuri. Tulishuka daraja, lakini kilichoniumiza zaidi si kushuka kwa timu, bali nilichofanyiwa baada ya msimu.”
Mbogo anadai kuna fedha zake ambazo alikuwa akidai hakuwahi kulipwa, anasema: “Kuna maslahi yangu yalichukuliwa. Nikihesabu yote yalikuwa yanafika karibu Sh10 milioni. Nilisubiri nilipwe lakini hai-kutokea.”
Anasema tukio hilo lilimuumiza kiasi cha kufikia hatua ya kuuchoka mpira, anasema”Nilikasirika sana. Niliona kama juhudi zangu zote hazikuwa na thamani. Kwa kipindi fulani niliuchukia kabisa mpira.”
AKAIREJESHA TOTO LIGI KUU
Wakati huo Toto African ilikuwa imeshuka Daraja la Kwanza. Viongozi wa klabu hiyo walimfuata na ku-muomba arudi kuisaidia.
Anasema hakusita. “Nilirudi kwa sababu nilikuwa naipenda Toto. Tulipambana sana mpaka tukaipandi-sha tena Ligi Kuu.”
Lakini baada ya kazi kukamilika anasema kilichotokea kilimuumiza.
“Nilitegemea watu waliokuwa wameipandisha timu watathaminiwa, lakini haikuwa hivyo. Msimu wa kusajiliwa upya nikajikuta nimeachwa,” anasema.
Kwa Mbogo, huo ulikuwa mwanzo wa kutafuta changamoto mpya nje ya Tanzania.
BURUNDI ILIVYOMPA MAISHA
Safari yake ikampeleka Burundi ambako alipata nafasi ya kufanya majaribio Olimpiki Star.
“Nilienda kufanya majaribio, nilicheza mechi moja, halafu ya pili baada ya mechi viongozi wakaniambia wamefurahishwa na uwezo wangu. Tukakaa mezani tukakubaliana,” anasema.
Anasema wakati huo Burundi ilikuwa bado inapitia changamoto za kisiasa na kiusalama lakini hilo halik-umzuia kutafuta maisha.
“Timu ilikuwa Muyinga (sasa umeunganishwa kuwa Mkoa wa Buhumuza) kaskazini mashariki mwa nchi ya Burundi. Kulikuwa na changamoto nyingi za usalama, lakini niliona huo ndio ulikuwa wakati wangu wa kuendelea na kazi,” anasema beki huyo.
Kwa kiwango alichokionyesha, viongozi wa klabu walifika mbali zaidi ya kumtaka acheze timu yao ya taifa la Burundi.
“Waliniambia nibadilishe uraia niwe raia wa Burundi ili nipate nafasi ya kuichezea timu yao ya taifa,” anasema.
Hata hivyo, uamuzi huo haukufikiwa. “Mama yangu alikataa kabisa. Aliniambia kila siku anasikia habari za machafuko Burundi, akaona isiwe. Niliheshimu uamuzi wake. Nikawaambia viongozi naendelea ku-cheza kama mchezaji wa kigeni.”
Baadaye alirejea Mwanza kwa mapumziko na kukuta Toto African ikiwa kwenye hali mbaya, anasema; “Nikakuta timu iko kwenye wakati mgumu. Nikasaini tena kuisaidia. Tukapambana ikabaki Ligi Kuu, lakini mwisho wa msimu nikajikuta tena sijasajiliwa.”
Anasema hilo lilikuwa pigo lingine ambalo hakulitegemea.
PACOME, CHAMA
Pamoja na kuunga mkono ushindani unaoletwa na wachezaji wa kigeni katika Ligi Kuu Bara, Mbogo anaonya kuwa si kila anayesajiliwa kutoka nje ana ubora unaozidi wazawa. Kwa mtazamo wake, klabu zinapaswa kuwa makini katika usajili ili kuhakikisha kila nafasi inayochukuliwa na mchezaji wa kigeni inaleta thamani ya ziada kwa timu.
Anasema kuna baadhi ya nyota ambao wameonyesha wazi tofauti yao na ndiyo maana wamekuwa wakisifiwa na mashabiki pamoja na wadau wa soka.
Mbogo anawataja kiungo wa Simba, Clatous Chama na mshambuliaji wa Yanga, Pacome Zouzoua kuwa ni miongoni mwa wachezaji waliokuja kuongeza ubora wa ligi kutokana na uwezo wao wa kiufundi na mchango wao ndani ya timu.
“Ukimwangalia Chama au Pacome unaona kabisa kuna kitu cha tofauti. Hawa wamekuja kuongeza ushindani na ubora wa ligi. Hawa ni aina ya wachezaji ambao unakubali kweli nafasi zao zinastahili,” anasema.
Hata hivyo, anasisitiza kuwa si kila mchezaji wa kigeni anayefika nchini anapaswa kupewa nafasi kwa sababu tu ametoka nje. Kwa maoni yake, wapo ambao kiwango chao ni cha kawaida na wakati mwingine kinazidiwa na vijana wa Kitanzania wanaokosa nafasi ya kuonyesha uwezo wao.
“Kuna wengine unawaona uwezo wao ni wa kawaida kabisa, lakini wamepewa nafasi wakati Mtanzania mwenye uwezo anakaa benchi au anakosa timu kabisa. Hapo ndipo tunapaswa kujiuliza kama kweli tunapata thamani ya nafasi za wachezaji wa kigeni.”
Mbogo anaamini changamoto hiyo haiishii kwa viongozi wa klabu pekee, bali hata kwa wachezaji wa Tanzania wenyewe. Anasema vijana wengi wamekuwa wakikosa moyo wa kujituma na kupambana ili kufikia viwango vya juu vya ushindani.
“Wakati mwingine tunashindwa kujitambua. Vijana wengi wa sasa wamekuwa wavivu. Mafanikio yanahitaji kujitoa, lakini wengi wanataka mafanikio ya haraka bila kupitia mchakato wa kufanya kazi kwa bidii,” anasema.
Kwa mujibu wa beki huyo wa zamani, ushindani unaoletwa na wachezaji wa kigeni unapaswa kuwa chachu ya kuwafanya wazawa kuongeza bidii badala ya kukata tamaa. Anaamini mchezaji wa Tanzania akijituma ipasavyo ana uwezo wa kushindana na yeyote anayekuja kutoka nje.
“Mpira hauna uraia. Anayecheza vizuri ndiye anayestahili nafasi. Lakini ili tufike hapo, vijana wetu lazi-ma wajitume zaidi na wajiamini. Tukifanya hivyo, tutakuwa na Watanzania wengi watakaong’ara hata nje ya nchi kama ilivyo kwa Chama na Pacome walivyokuwa mfano wa ubora katika ligi yetu.”
ITAENDELEA KESHO