Mtihani mzito unamkabili Husseni Mihambo Yanga
Muktasari:
- Mihambo anapaswa kufahamu kuna njia mbili. Kufanikiwa au kufeli, haya yanamkabili mchezaji yeyote ndani ya timu hasa anayeangaliwa zaidi ni yule mgeni kila mmoja akitaka kuona ana kitu kipi cha ziada anakwenda kukitoa baada ya kusajili. Hivyo uamuzi ni wake kupita moja ya njia hiyo.
USAJILI wa mshambuliaji Husseni Mihambo (18) kwenda Yanga kwa mkataba wa miaka minne umeibua mjadala mkubwa sio kwa sababu tu ya umri wake mdogo, bali kutokana na ukweli kwamba anaingia kwenye moja ya klabu zenye presha kubwa zaidi Afrika Mashariki, ambako kila mchezaji analazimika kupambana na ushindani wa nafasi kila siku.
Kwa mchezaji yeyote anayesajiliwa Yanga, kusaini mkataba ni hatua ya kwanza lakini kazi inanzia unapoingia kambini.
Hilo ndilo linalomsubiri Mihambo, ambaye anajiunga na kikosi chenye washambuliaji ambao tayari wameshajitengenezea nafasi kwenye kikosi hicho.
Mihambo anapaswa kufahamu kuna njia mbili. Kufanikiwa au kufeli, haya yanamkabili mchezaji yeyote ndani ya timu hasa anayeangaliwa zaidi ni yule mgeni kila mmoja akitaka kuona ana kitu kipi cha ziada anakwenda kukitoa baada ya kusajili. Hivyo uamuzi ni wake kupita moja ya njia hiyo.
Inafahamika wazi kwamba, ili ufanikiwe, lazima juhudu kubwa ianzie mazoezini, lakini ukizembea hapo, bila shaka utakuwa umechagua njia ya kufeli.
Bahati nzuri Mihambo amesajiliwa Yanga wakati ambao kocha mkuu, Manqoba Mngqithi na wasaidizi wake ni wageni hivyo ndio kwanza wanaanza kutengeneza timu na kama atafanya juhudi mazoezini huenda akawa ndio mshambuliaji anayepata nafasi ya kuanza na kuonyesha uwezo wake.
Kwa falsafa ya kocha huyo aliyetua akitokea Afrika Kusini, huwa hatazami jina la mchezaji bali kiwango. Anataka washambuliaji wanaoshiriki katika kukaba kuanzia mbele, wanaotengeneza nafasi, wanaocheza kwa kasi na wanaotumia vizuri nafasi chache wanazozipata.
WALIOPO
Ndani ya kikosi hicho tayari kuna Clement Mzize, ambaye ni miongoni mwa washambuliaji wanaoelewa vizuri mfumo wa timu. Yupo Laurindo Depu ambaye alisajiliwa dirisha dogo akitokea Radomiak Radom.
Lakini ndani ya kipindi hicho alicheza mechi 18 za Ligi Kuu akifunga mabao tisa, mechi nne za Ligi ya Mabingwa Afrika akifunga mabao mawili.
Mbali na Depu wapo Emmanuel Mwanengo na Edmund John ambao nao bado wanapambana kutafuta nafasi ya kudumu. Hiyo inaonyesha wazi kuwa Mihambo hataingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza atalazimika kuthibitisha kupata nafasi.
REKODI ZAKE ALIPOTOKA
Kinachoongeza ugumu zaidi ni rekodi aliyotoka nayo Mashujaa FC. Msimu uliopita hakupata muda mwingi wa kucheza kutokana na ushindani wa kikosi na alimaliza akiwa amefunga bao moja. Hiyo ina maana kuwa anatua Yanga bila takwimu za kutisha zinazoweza kumbeba mbele ya mashabiki wanaotaka kuona matokeo ya haraka.
Ni kweli kabla ya kurejea Tanzania aliwahi kupitia mfumo wa vijana wa Jomo Cosmos nchini Afrika Kusini, huku pia akifanya majaribio kwa zaidi ya mwaka mmoja Dubai.
Uzoefu huo unaweza kumsaidia kukabiliana na mazingira mapya, lakini hautampa nafasi ya moja kwa moja kwenye kikosi lakini Yanga ni klabu ambayo kila mechi ni fursa ya kuthibitisha uwezo.
HISTORIA INAKATAA
Katika miaka ya hivi karibuni Yanga imesajili vijana wengi wenye vipaji vikubwa, lakini si wote walioweza kuhimili ushindani wa ndani ya kikosi.
Wapo waliosajiliwa na kutabiriwa makubwa lakini baada ya muda mchache walijikuta wakikaa benchi au kutolewa kwa mkopo ili kupata dakika za kucheza.
Mfano ni kiungo Shekhan Khamis. Alipotua Yanga alionekana kuwa miongoni mwa vipaji bora vya kizazi chake. Mashabiki walitarajia angekuwa sehemu ya kikosi cha kwanza kwa muda mfupi lakini alishindwa kuhimili presha.
Na taarifa zinaeleza kuwa yupo mbioni kutolewa kwa mkopo kwenda Singida Black Stars ili akatafute muda wa kucheza, jambo linaloonyesha namna ilivyo vigumu kwa mchezaji chipukizi kujihakikishia nafasi ndani ya kikosi hicho.
Hapo ndipo mtihani upo. Katika klabu kama Yanga, kuna nyakati unaweza kucheza dakika 15 kwa mechi tatu mfululizo, lakini ukitumia vibaya dakika hizo unaweza kujikuta ukisubiri nafasi nyingine kwa muda mrefu.
Mngqithi pia anapenda wachezaji wenye nidhamu ya hali ya juu na wanaotekeleza maelekezo ya kimfumo. Kama Mihambo ataonyesha utayari wa kujifunza, kuongeza nguvu kwenye mazoezi na kutumia kila nafasi atakayopewa, anaweza kutengeneza nafasi yake taratibu.
Kwa upande mwingine, umri wake bado ni faida kubwa. Mkataba wa miaka minne unaonyesha Yanga haijamsajili kwa ajili ya matummizi ya muda mfupi, bali kwa ajili ya baadae. Klabu inaonekana inaamini anaweza kukua ndani ya mfumo huo na baadaye kuwa mmoja wa washambuliaji muhimu wa timu.
Hata hivyo mashabiki wa Yanga hawana subira. Mashabiki wanataka matokeo ya haraka hawana muda wa kukusubiria kipindi kirefu hivyo ni kazi kwako kupambana na kuwa na nidhamu ya kazi.
Kwa Mihambo safari imeanza, amefanikiwa kusajiliwa na moja ya klabu kubwa Afrika ambayo vijana wengi huitamani nafasi hiyo, lakini sasa anapaswa kuthibitisha kuwa anastahili kuvaa jezi ya Yanga.
Kama ataweza kuvuka mtihani wa ushindani, presha na matarajio makubwa ya mashabiki, ana nafasi ya kuandika historia yake Jangwani.
MSIKIE MWENYEWE
Akizungumzia baada ya kutambulishwa Mihambo alisema: "Yanga ni timu kubwa na kusajiliwa kwangu ni kama deni wananchi wameniamini kwa hiyo napaswa kuipambania klabu hii na wanipokee tupammbanie mataji wote."