CHOBANKA: Kocha wa Masaka anayeeleza kwanini anafundisha wanawake

Muktasari:
- Ukitaja mafanikio ya mshambuliaji wa Brighton ya England, Aisha Masaka ni kwamba amepita kwenye mikono ya kocha huyo anayeamini kukuza vipaji ni mafanikio makubwa kwake.
KAMA kuna kocha aliyevumbua vipaji vya soka kwa mabinti wadogo, basi ni huyu Ezekiel Chobanka ambaye anaifundisha Ceasiaa Queens ya mkoani Iringa.
Ukitaja mafanikio ya mshambuliaji wa Brighton ya England, Aisha Masaka ni kwamba amepita kwenye mikono ya kocha huyo anayeamini kukuza vipaji ni mafanikio makubwa kwake.
“Unaweza kupitia changamoto nyingi kuwasaidia mabinti hao.Kuna muda mchezaji anatamani kucheza, lakini mzazi hapendi akiamini mpira ni kwa watoto wa kiume kumbe mwanamke anaweza kufanya mambo makubwa,” anasema Chobanka.
“Muda mwingine vipaji vinapotea kwa sababu ya ukosefu wa fursa, kukatishwa tamaa na jamii au ugumu wa kuwashawishi watu waione thamani ya vipaji vya watoto wa kike. Lakini pamoja na hayo naendelea kupata motisha kubwa nikiangalia baadhi yao waliofanikiwa.
“Mfano leo hii kama kuna mzazi alimkataza binti yake kucheza akimuona Masaka yupo Uingereza anavyoishi vizuri mwingine haweza kukataa. Kwa hiyo ni jambo ambalo najivunia sana.”
Chobanka anasema Masaka ni miongoni mwa washambuliaji wachache Watanzania wenye uwezo wa kufunga akitaja sifa zake kuwa ni hatari ndani ya boksi.
“Amecheza Yanga kwa mafanikio makubwa sana. Kila kocha anatamani kuwa na mchezaji wa aina yake kwa sababu anajua vizuri namna ya kufunga. Umbo, akili vinambeba anapokuwa langoni,” anasema kocha huyo aliyekivumbua kipaji cha Masaka wakati akiifundisha Alliance Girls ya Mwanza.
“Kwa sasa hapati nafasi England, lakini kuna sababu nyingi nafikiri bado hajaendana na kasi ya ligi hiyo ambayo ni ngumu, lakini anahitaji muda wa kutosha akizoea atakuwa bora sana.
“Wakati anasajiliwa akitokea BK Hacken ya Sweden alikuwa na msimu bora bahati nzuri wachezaji wanaopita kwangu huwa nawafuatilia ndipo hapo Brighton wakamuona.”
Kabla ya Masaka kujiunga na Yanga msimu wa 2019/20 aliichezea Alliance FC ndipo Wananchi wakamsajili baada ya kuonyesha kiwango bora.
Msimu 2020/21 aliibuka mfungaji bora akitupia kambani mabao 35, rekodi ya kufunga mabao mengi ambayo haijawahi kuvunjwa tangu wakati huo hadi sasa ikiwa imepita misimu minne Ligi Kuu ya Wanawake Bara(WPL).
Kocha huyo aliifundisha Alliance Girls misimu zaidi ya mitano, Tiger Queens na sasa Ceasiaa iliyopo nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi.
Chobanka amefanya zungumza na Mwanaspoti mambo mbalimbali ikiwemo kwanini kachangua kufundisha soka la wanawake na sio wanaume.
KWANINI WANAWAKE?
Kocha huyo anasema kabla ya kufundisha wanawake aliwahi kuwa kocha wa timu za wanaume za madaraja ya chini, lakini aliachana nazo na kupambania soka la wanawake. “Niliona kuna fursa kwenye soka la wanawake. Sio kifedha, hapana, lakini kusaidia wachezaji, ila ni kama WPL imenipenda kutokana na mafanikio makubwa niliyoyapata.
“Nilitamani kufundisha Ligi Kuu na sio madaraja ya chini ndio maana nikasema naweza kufundisha timu za kike na nashukuru nimefanikiwa,” anasema kocha huyo.
MASTAA KIBAO
Kama kuna kitu anajivunia Chobanka ni kuwafundisha na kuwatoa nyota wanaocheza soka la kulipwa nchini na nje ya nchi.Ukiachana na Masaka wengine aliowafundisha ni Enekia Lunyamila anayecheza Mazaltan ya Mexico, Aliya Fikirini, Elizabeth John na Janeth Matulanga (JKT Queens), Aisha Mnunka (Simba Queens) na Suzana Adam (TUT FC, Misri).
“Najivunia kutoa vipaji ambavyo vinatamba duniani, barani Ulaya, Afrika na Ligi ya Tanzania kama ulivyoandika Enekia, Aisha na wengine. Napata faraja kubwa kuona natoa wachezaji wakubwa,” anasema Chobanka.
MUUMINI WA VIJANA
Kocha huyo anasema anaamini kwenye vipaji vya vijana ambao wakitengenezwa wanakuwa bora.
“Mabinti wadogo bado damu changa ukiwaamini na kuwatengeneza kidogo wanakuja kuwa bora sana ndio maana napendelea vijana. Kuna wachezaji nakutana nao kwe-nye mechi hadi nimewasahau wananisalimia, unaona namna gani nimefundisha wachezaji wengi,” anasema.
“Ukipita kwenye timu 10 zinazoshiriki (WPL) utakuta kuna wachezaji wawili watatu niliowafundisha kwenye klabu mbalimbali. Hii inanipa motisha kuendelea kuwapambania wengine.”
MAFANIKO SASA
Ukiachana na kufundisha nyota mbalimbali kocha huyo anasema kwake msimu wa 2019/20 ulikuwa bora na alimaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi akiwa na Alliance.
“Mafanikio mengine nafikiri ni kushika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu mwaka 2019. Huo ulikuwa msimu bora sana kwangu. Tulipambana na vigogo wa Simba na Yanga ambao hatukuwapa nafasi. Hivyo tulionyesha ushindani mkubwa.
“Msimu uliofuata kuna nyota kibao wakasajiliwa na timu hizo wale waliofanya vizuri na wengine walipata timu nyingine nafikiri huo siwezi kuusahau,” anasema.
“Mengine msimu uliopita nilifanikiwa kuchukua ubingwa wa mashindano ya FEASSA yaliyofanyika nchini Uganda, vikombe na medali vina maana kubwa.”
CHANGAMOTO
Chobanka anasema pamoja na kukua kwa soka la wanawake, lakini kuna changamoto nyingi zinazoikwamisha Ligi Kuu ya Wanawake inayokua siku hadi siku. “TFF na wadau wengine wamepambana sana kuisogeza ligi ikiwemo kuonyeshwa (kwenye runinga). Watu wanatazama mubashara wakiona vipaji vingi ndio maana sasa hata wachezaji Watanzania wanasajiliwa ligi kubwa na wanaanza kwenye timu hizo na kucheza.. hayo ni maendeleo makubwa,” anasema.
“Lakini changamoto kubwa ni pamoja na uwekezaji wa klabu, ishu ya udhamini ni suala linaloumiza sana. Kuna muda timu zinashindwa kufika kwa wakati uwanjani sababu ya usafiri, lakini kukiwa na udhamini itasaidia kwa kiasi fulani.
“Simba, Yanga hizi ni timu zenye uwekezaji mkubwa wengine wanapata mahitaji yote kupitia mgongo wa timu kubwa... JKT Queens na Mashujaa pia ni za jeshi kuna ahueni fulani sasa kuna nyingine hata kula shida na bado wanacheza.”
Hata hivyo, Chobanka anaiona Ligi Kuu ya Wanawake miaka mitano ijayo itakuwa miongoni mwa ligi bora kiuendeshaji, ukuzaji wa vipaji na uwekezaji kama wadau watawekeza zaidi.
“Kwa sasa changamoto kubwa lakini nafikiri zikitatuliwa mapema itakuja kuwa ligi bora sana, kuna wachezaji kibao sasa wanakuja kuichezea ligi ya Tanzania ukiwauliza wanakwambia huku kuna posho tofauti na nchi wanazocheza.”