Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kibabe zaidi... Yanga na rekodi tamu Kombe la Shirikisho (FA)

YANGA Pict

Muktasari:

  • Katika mechi hiyo iliyoshuhudia kiungo mkabaji wa Yanga, Mukoko Tonombe akilimwa kadi nyekundu sekunde chache kabla ya mapumziko kwa kumchezea vibaya nahodha wa Simba, John Bocco ‘Adebayor’.

UNAIKUMBUKA ile mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC) iliyopigwa Julai 25, 2021 kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, mjini Kigoma?

Katika mechi hiyo iliyoshuhudia kiungo mkabaji wa Yanga, Mukoko Tonombe akilimwa kadi nyekundu sekunde chache kabla ya mapumziko kwa kumchezea vibaya nahodha wa Simba, John Bocco ‘Adebayor’.

Kadi hiyo ni kama iliigharimu Yanga kwani ililala kwa bao 1-0 na kuipa Simba taji la pili mfululizo la michuano hiyo. Bao pekee lililoizamisha Yanga, liliwekwa kimiani na kiungo mkabaji raia wa Uganda, Taddeo Lwanga ‘Injinia’ dakika ya 80 kwa kichwa akimalizia mpira wa kona iliyochongwa vyema na winga, Luis Miquissone.

Sasa kama hujui, tangu ilipopoteza pambano hilo la Lake Tanganyika, Kigoma hadi sasa unaposoma makala haya, Yanga haijapoteza tena mchezo wowote wa michuano ya Kombe la Shirikisho ikiweka rekodi ya kucheza mechi 21 ikiwa tayari ipo robo fainali.

Awali, Simba ndiyo iliyokuwa ikishikilia rekodi ya kucheza mechi nyingi (17) mfululizo bila kupoteza kuanzia msimu ya 2019-2020, 2020-2021 na 2021-2022 ilipotolewa nusu fainali na Yanga kwa kulazwa bao 1-0 lililotokana na shuti kali la mbali la kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’, aliyepo Azam FC kwa sasa.

YANG 01

Mechi hiyo iliyoitibulia Simba ilipigwa Mei 28, 2022 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza na kuivusha Yanga hadi fainali na kubeba ubingwa wa kwanza kati ya mitatu iliyotwaa hadi sasa mfululizo kwa msimu huo wa 2021-2022 kwa kuichapa Coastal Union kwa penalti 4-1.

Mchezo huo wa fainali uliopigwa Julai 2, 2022 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha ulishuhudiwa ukimaliza dakika 90 kwa sare ya 2-2 na kuongezwa dakika 30 na kila timu iliongeza bao moja na kufanya matokeo ya dakika 120 kuwa sare ya 3-3.

Yanga ikipata mabao yake kupitia kwa Feisal Salum Dk 57, Heritier Makambo 82’ na Denis Nkane dk 113, wakati Abdul Suleiman ‘Sopu’ akipiga hat trick kwa kuwafungia Wagosi mabao yote matatu dakika za 10, 87 na 98’


SAFARI ILIVYOANZA

Katika msimu huo ambao Yanga iliinyang’anya taji Simba kwa kuing’oa nusu fainali, safari ya ubingwa kwa Vijana wa Jangwani ilianza kwa kuitoa Ihefu kwa mabao 4-0 katika pambano lililopigwa Desemba 15, 2021 na kutinga 32 Bora ilipokutana na  Mbao FC na kuichapa kwa bao 1-0 siku ya Januari 29, 2022.

Katika hatua ya 16 Bora, wababe hao wa soka nchini, walikutana na Biashara United na kuifunga mabao 2-1 mechi ikipigwa Februari 15, 2022 na kufuzu hatua ya robo fainali na huko ilivaana na Geita Gold na kumaliza dakika 90 kwa sare ya 1-1 kabla ya kuvuka kwenda nusu fainali kwa ushindi wa penalti 7-6 mechi iliyopigwa Aprili 10, 2022.

YANG 02

Ndipo katika nusu fainali bao la kombora la mbali la Fei Toto likaizamisha Simba na kuitemesha taji na kwenda kuvaana na Coastal katika fainali kali iliyopigwa jijini Arusha na Yanga kubeba taji kwa msimu huo ambao pia ilimaliza kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa rekodi ya bila ya kupoteza.


MOTO WA 2022-2023

Katika msimu huu, Yanga ilianza michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho kwa kupangwa kukutana na Kurugenzi FC ya Kagera katika hatua ya 64 Bora na kushindwa kwa kishindo kwa mabao 8-0, mchezo ukipigwa Desemba 10, 2022 jijini Dar es Salaam.

Yanga iliendeleza kugawa dozi nene katika michuano hiyo hatua ya 32 Bora baada ya kuifumua Rhino Rangers ya Tabora kwa mabao 7-0, mechi ikipigwa Januari 29, 2023 na kufuzu hatua ya 16 Bora ambapo ilipangwa kuvaana na Tanzania Prisons ya Mbeya,

Katika mchezo huo wa 16 Bora uliopigwa Machi 3, 2023, Yanga ilishinda kwa mabao 4-1 na kukata tiketi ya robo fainali na ilipangwa kukutana na Geita Gold mchezo uliopigwa Aprili 8, 2023 na kushinda kwa bao 1-0 lililofungwa na Fiston Mayele.

YANG 03

Yanga ilikutana na Singida Big Stars (sasa Fountain) katika mchezo wa nusu fainali uliopigwa Mei 21, 2023 mjini Singida na kushinda kwa bao 1-0 na kufuzu kwenda fainali ambapo ilikutana na Azam FC, mechi ikipigwa Juni 12, kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga.

Bao pekee lililoizamisha Azam liliwekwa kimiani kwa kichwa na Mzambia, Kennedy Musonda dakika ya 13 akimalizia mpira wa krosi ya beki Djuma Shaban ambaye awali alipiga kona fupi kwa Tuisila Kisinda na kunyunyiza mpira uliotendewa haki na mshambuliaji huyo aliyekuwa ametu kikosi dirisha dogo katika msimu huo.

Bao hilo lilidumu na kuifanya Yanga kutetea taji kwa msimu wa pili mfululizo ikifikisha jumla ya mechi 12 bila kupoteza katika michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho.

YANG 04

MSIMU WA 2023-2024

Yanga iliuanza msimu huu kibabe kwa kugawa dozi katika safari ya kutetea taji ikianza hatua ya 64 Bora kwa kuifumua Hausing ya Njombe kwa mabao 5-1 katika mechi iliyopigwa Januari 30, 2024 na kutinga hatua ya 32 Bora.

Katika hatua hiyo ya 32 Bora, watetezi hao walikutana na maafande wa Polisi Tanzania siku ya Februari 20, 2024 na kuwafumua kwa mabao 5-0 na kuvuka salama kwenda 16 Bora na huko ikakutana na Dodoma Jiji siku ya Aprili 10, 2024 kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma na kushinda kwa mabao 2-0.

Hatua ya robo fainali, Yanga ilikutana na Tabora United katika mchezo uliopigwa Mei Mosi, 2024 na kushinda kwa mabao 3-0 na kuvuka kwenda nusu fainali na ilikutana na Ihefu (sasa Singida BS) kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.

Mechi hii ilikuwa dume kweli kweli, kwani ilishuhudiwa zikipigwa dakika 120 na Yanga kushinda bao 1-0 lililopatikana katika dakika za nyongeza baada ya dakika 90 kumalizika kwa suluhu na kufuzu kwenda fainali kukutana na Azam FC.

Mchezo huu wa fainali ulipelekwa mjini Unguja kwene Uwanja wa New Amaan Complex na Yanga kushinda kwa penalti 6-5 baada ya dakika 120 kushindwa kutoa mshindi kwani timu hizo hazikufungana. Mechi hiyo iliyowapa Yanga ubingwa wa tatu mfululizo wa michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho ilipigwa Juni 2, 2024, ikifikisha jumla ya michezo 18 bila kupoteza.


YANG 05

MSIMU HUU SASA

Katika msimu huu wa 2024-2025, Yanga ilianza kutetea taji kwa kupangwa kuumana na Copco FC ya Mwanza inayoshiriki First League na watetezi hao waliibuka na ushindi wa mabao 5-0.

Ushindi huo ulipatikana katika pambano hilo la hatua ya 64 Bora lililopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, siku ya Jan 25 mwaka huu, 2025 na Shekhan Ibrahim alifungua pazia kwa kufunga bao dakika ya 35’.

Prince Dube alifunga bao la pili dakika ya 57 kaabla ya Maxi Nzengeli kufunga kwa penalti dakika ya 68 huku Dube Abuya na Mudathir Yahya kufunga mengine mawili ya mwisho na kuivusha Yanga kwenda hatua ya 32 Bora.

Katika hatua ya 32 Bora, Yanga ilipangwa kuvaana na Coastal Union mchezo uliopigwa pia kwenye Uwanja wa KMC Complex siku ya Machi 12 na watetezi hao kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 yaliyofungwa na Maxi Nzengeli aliyetupia mawili dk 2 na 15, kisha Mfungaji Bora wa michuano hiyo kwa msimu uliopita, Clement Mzize alifunga la tatu dk ya 21 muda mchache baada ya Miraj Abdallah kuifungia bao Coastal dk ya 18.

Yanga ikavuka salama hadi hatua ya 18 Bora na kama kawaida, watetezi wakatoka na ushindi kwenye Uwanja wa KMC Complex dhidi ya Songea United iliyopo Ligi ya Championship.

Yanga ilipata ushindi wa mabao 2-0 na kuifanya ifikishe mechi ya 21 mfululizo katika Kombe la Shirikisho bila kupoteza kwa mabao ya Duke Abuya dakika ya 22 na jingine la Jonathan Ikangalombo ‘Ikanda Speed’ aliyefunga dakika ya 54.

Kwa sasa watetezi hao wanasikilizia watakutana na timu ipi hatua ya robo fainali ili kuona kama itaendelea moto wake au itakatwa stimu na kulitema taji inalolishikilia kwa misimu mitatu mfululizo sasa. Ngoja tuone!